Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma,Kamishna Msaidizi wa Polisi SUZAN S. KAGANDA akionyesha baadi ya vitu walivyokutwa navyo watu saba wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani humo kwa makosa mbalimbali.
Na: Sylvester Onesmo wa Jeshi la Polisi Dodoma.
Jeshi la Polisi mkoani Dodoma linawashikilia watu saba kwa makosa mbalimbali waliokamatwa katika harakati za kufanya uhalifu.
Akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake Kamishna Msaidizi wa Polisi SUZAN S. KAGANDA amesema tukio la kwanza limetokea tarehe 20/12/2013 majira ya saa 23:00 usiku eneo la Kizota Manispaa ya Dodoma ambapo watu sita wamekamatwa wakiwa wamevunja ghala kwa kung’oa bati moja la paa na kuingia ndani.
Kamanda KAGANDA amewataja watu hao amabao ni:
1. MSABAHA S/O KHALID, mwenye umri wa miaka 21, muha, mkazi wa Kizota.
2. SIX S/O JOHN, mwenye umri wa miaka 26, mfipa, mkazi wa Kizota.
3. ELIUDI S/O JULIUS, mwenye umri wa miaka 31, mgogo, mkazi wa Kizota.
4. KAIMBA S/O KHALID, mwenye umri wa miaka 24, muha, mkazi wa Kizota.
5. PETRO S/O SAMWELI, mwenye umri wa miaka 24, mgogo, mkazi wa Chang’ombe.
6. ZAWADI S/O DANIEL, mwenye umri wa miaka 20, mgogo, mlinzi, mkazi wa Kizota.
Aidha Jeshi la Polisi lilifanikiwa kuokoa mali yote iliyokuwa imeibiwa yenye thamani ya Tsh. 3,567,700/= mali ya METESH s/o BENSELAL, mali hiyo ni viti vya Plasitc 143, mop buckets dazani 2, mabeseni makubwa 48, meza za plastic 20, rock 236 na spiral beseni 72.
Upelelezi wa tukio hili unaendelea na watuhumiwa watafikishwa mahakamani.
Katika tukio la pili lililotokea tarehe 22/12/2013 majira ya saa 17:00 jioni katika nyumba ya kulala wageni iitwayo SWEETLAND iliyoko eneo la Bahi road Manispaa ya Dodoma, alikamatwa SALUM s/o ISAACK KABANGILA, mwenye umri wa miaka 33, Msukuma, fundi selemala, mkazi wa Mwanza. Alikamatwa akiwa na Television sita flat screen na nne kati ya hizo ziliibiwa Mbeya.
Hata hivyo Kamanda KAGANDA amesema mtuhumiwa huyo alifika katika nyumba hiyo ya kulala wageni na kupanga chumba namba saba ambapo baada ya kuiba alikuwa akihifadhi vitu hivyo katika mifuko.
Pia mtuhumiwa huyo alikutwa na funguo nyingi za aina mbalimbali alizotumia kufungulia milango na kufanikisha wizi huo. Mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa ili kubaini mtandao wake wa uhalifu na atafikishwa mahakani mara upelelezi utakapokamilika.
Sanjari na hayo Kamanda KAGADA amesema katika kipindi cha mwaka 2013 Jeshi la Polisi mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na wadau wa Polisi jamii liliimarisha ulinzi maeneo mbalimbali katika kukabiliana na uhalifu. Kiwango cha uhalifu hasa kwa makosa makubwa ya unyang’anyi wa kutumia silaha yameshuka kwa asilimia 4% ukilinganisha na mwaka 2012 ambapo jumla ya makosa yote kwa mwaka 2013 ni makosa 1745 ni pungufu kwa makosa 80 sawa na 4% ikilinganishwa na makosa 1825 ya mwaka 2012.
Jedwali la makosa dhidi ya biadamu, kuwania mali na makosa dhidi ya maadili ya jamii kwa kipindi cha Jan-Dec 2012 na Jan- Nov 2013.
Kamanda KAGADA amesema wakati tunaelekea Sherehe za X - Mass zinazotegemewa kuanza usiku wa tarehe 24/12/2013 kuamkia tarehe 25/12/2013 hadi tarehe 26/12/2013 na hata baada ya sikukuu hiyo itafuata sikukuu ya mwaka mpya itakayokuwa tarehe 01/01/2014.
Jeshi la polisi tunakumbusha kuwa sikukuu zote hizo zitasherehekewa kwa shamrashamra nyingi kifamilia, kirafiki, kidini na kadhalika.
Ni mategemeo ya Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Dodoma kwamba wananchi watasherehekea sikukuu hizo kwa amani na utulivu wakizingatia mambo muhimu ya usalama kwa ushirikiano wa dhati na Jeshi lao la Polisi ambalo litaimarisha ulinzi kwa kipindi chote cha sikukuu.
Mambo ambayo Jeshi la Polisi lingependa kuona na kuzingatia katika kipindi hicho cha sikukuu ni pamoja na:-
1. Kuendelea kuimarisha utaratibu wa Ulinzi Shirikishi katika mitaa na vitongoji chini ya wenyeviti wa Serikali za Mitaa.
2. kuhakikisha nyumba hazibaki tupu bila watu/mtu atakayekuwa muangalizi wa nyumba.
3. Kuhakikisha usalama wa watoto wadogo wanapotoka kwenda na kurudi katika maeneo yenye shamrashamra.
4. Madereva wa magari na vyombo vingine vya usafiri wawe makini na waangalifu ikiwa ni pamoja na kuepuka ulevi ili wasihatarishe usalama wa watu wengine barabarani.
5. Wenye kumbi za starehe wasiwaruhusu watu kujazana katika kumbi zao kwa kiwango cha kusababisha hatari,kama disco toto.
6. Wenye baa wazingatie sheria kuhusu muda wa kufungua na kufunga baa zao.
7. Kwa tukio lolote ambalo siyo la kawaida tafadhali tuma ujumbe kupitia namba 0767 – 750191 na taarifa hiyo itashughulikiwa mara moja.
Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limetoa onyo kuwa kwa wale wote ambao watakiuka sheria watakamatwa na kuchukuliwa hatua.Jeshi la polisi linawatakia heri ya x-mass na mwaka mpya kwa kuzingatia utii wa sheria bila shuruti.