Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limepiga marufuku ulipuaji wa fataki wakati wa sherehe za mkesha wa Mwaka Mpya, kutokana na sababu za kiusalama.
Imeelezwa kwamba zuio hilo, linatokana na sababu za kiusalama na matishio mbalimbali ya kigaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Hayo yameelezwa na Kamisha wa Polisi Kanda, Suleiman
Kova wakati akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Alieleza kuwa ikiwa itaruhusiwa, inawezekana kutumika kama mwanya kwa wahalifu, kutenda uhalifu wao.
“Kwa wale ambao wanapenda kusherehekea Mwaka Mpya kwa kulipua fataki au fashi fashi, safari hii watafute mtindo mpya wa kusherehekea, lakini fataki ni marufuku. Ieleweke hatufanyi kwa kumkomoa mtu, bali ni kwa kuchukua tahadhari, sababu mtu anaweza akalipua fataki na mwingine akatumia muda huo kufanya mambo yake na hasa kwa kuzingatia matishio yaliyopo,” alisema Kamanda Kova.
Akizungumzia kuhusiana na usalama katika sherehe za Krismasi, alisema ulinzi ulikuwa mkali na hakuna matukio makubwa ya uhalifu, yaliyotokea, bali ni madogo ambayo hata hivyo waliweza kuyadhibiti.
Alisema kuwa askari wa kituo cha Kigamboni, walitilia shaka gari aina ya Toyota Cresta, lenye namba za usajili T607 BNE lililokuwa likiendeshwa na Michael Joseph, mkazi wa Mjimwema, Kigamboni katika Manispaa ya Temeke.
“Tukio hili lilitokea Desemba 24 ambapo baada ya askari kutilia shaka walilisimamisha na kuanza kulipekua, ambapo walifanikiwa kupata shotgun yenye mitutu miwili na namba za usajili TZCAR 90774 iliyotengenezwa China ikiwa imefichwa katika boneti ya gari karibu na injini,” aliongeza.
Ndani ya gari hilo ilipatikana bastola moja aina ya Revolver, yenye namba za usajili 393304379, ikiwa na risasi tano ndani ya kasha la kuhifadhia risasi, iliyotengenezwa nchini Marekani.
Alisema pia zilipatikana risasi nyingine 11, ambapo risasi tisa kati ya hizo ni za bunduki aina ya G-3 na risasi mbili za shotgun.
Alisema bastola nyingine yenye namba za usajili TZCAR 101489, iliyotengenezwa Jamhuri ya Czech ilikamatwa juzi katika eneo la Madale Kontena baada ya kutokea mtafaruku baina ya watu wawili.
“Huyu jamaa mtoa taarifa (Andrew Simon) alijeruhiwa na mtu anayemfahamu kwa sura, akiwa anaendesha gari kisha kumsukuma nje ya gari lake.
Baada ya mtoa taarifa kuhoji kilichotokea ndipo mtuhumiwa alikwenda nyumbani kwake kisha muda mfupi alirudi na bastola mkononi. “Alipiga risasi moja hewani na mbili zilimjeruhi mtoa taarifa katika ubavu wa kushoto. Lakini tumeshajua bastola ni ya nani na tunafuatilia ili aweze kukamatwa,” alisema.
Aidha, aliongeza kuwa kwa sasa polisi wanashirikiana na kampuni ya ulinzi ya Kiwango ili kudhibiti wizi wa miundombinu katika minara ya simu, ambapo kwa mwananchi atakayetoa taarifa atapata zawadi kuanzia Sh 100,000 mpaka Sh milioni moja, kulingana na uzito wa mafanikio yaliyopatikana.
Alisisitiza wananchi waendelee kushirikiana na jeshi la polisi, ambapo alitaja namba za Makamanda wa Mikoa ya Kipolisi ili wawape taarifa moja kwa moja.
Kwa Dar es Salaam aliwataja Makamanda na namba zao za simu kuwa ni Kamanda Marietha Minangi wa Ilala (0715 009 980), Kamanda wa Temeke Engelbert Kiondo (0715 009 979) na Kamanda wa Kinondoni, Camillius Wambura (0715 009 976).
HABARI NA HABARI LEO