INAKADIRIWA kiasi cha watu milioni 1.6 watapatwa na ugonjwa wa saratani mwaka huu nchini Marekani na inakadiriwa kuwa kati ya hao, watu laki 5 watapoteza maisha kutokana na ugonjwa huo hatari. Pia kiasi cha watu laki 6 hufariki kwa ugonjwa wa moyo nchini humo kila mwaka.
Licha ya maendeleo ya kisayansi yaliyopatikana kwa nusu karne iliyopita, lakini makampuni ya kimagharibi yanayotengeneza dawa za binadamu, yameshindwa kuvumbua dawa madhubuti ya kudhibiti magonjwa haya mawili yanayouwa watu wengi zaidi duniani.
Inaelezwa na watafiti wa masuala ya afya nchini Marekani kuwa hivi sasa imedhihirika kuwa mikakati mingi ya kisasa, kuanzia kwenye vipimo hadi matibabu ya magonjwa ya moyo na saratani, imeshindwa kufanya vipimo na kutoa matibabu sahihi, wakati mwingine kwa kukosea, tiba ya magonjwa haya huwa na madhara zaidi kwa mgonjwa kuliko ahueni.
Soda na hatari ya saratani
Kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni, wanawake wenye umri kuanzia miaka 40, ambao hunywa kwa wingi soda au vinywaji vingine baridi vyenye sukari nyingi, wako katika hatari kubwa ya kupatwa na saratani ya kizazi.
Imeelezwa kuwa utafiti huo ni wa uhakika kwa sababu matokeo hayo yamepatikana baada ya kuwafanyia utafiti wanawake waliofikia ukomo wa hedhi (postmenopausal) wapatao 23,000 kwa kuwafuatilia kwa muda wa miaka 14.
Katika utafiti huo, ilibainika kuwa wanawake waliokuwa na matumizi makubwa ya sukari walikuwa katika hatari kubwa ya kupatwa na saratani ya kizazi kwa asilimia 78. Kwa mujibu wa mwandishi wa utafiti huo, Bw. Maki Inoue-Choi, hakushangazwa na matokeo ya utafiti huo kwani imekuwa ikisemwa kwa muda mrefu kuwa sukari nyingi ina madhara.
Aidha, utafiti mwingine unaonesha kuwa ‘fructose’ (aina ya sukari) huimarisha ukuaji wa chembechembe hai za saratani na kuharibu mifumo kadhaa mwilini kwa njia mbalimbali, ikiwemo kuharibu mfumo wa usagaji chakula tumboni, ukuaji wa seli za DNA na kinga ya mwili.
Baada ya utafiti huo, wagonjwa wa saratani za aina zote hushauriwa kutotumia kabisa vyakula vyoyote vyenye sukari, kwani kwa kufanya hivyo huwa wanauimarisha zaidi ugonjwa badala ya kuudhibiti. Sukari ni miongoni mwa vyakula vinavyoimarisha chembechembe hai za saratani, hivyo kuvinyima sukari ni njia moja wapo ya kuviua na kuvipa sukari ni sawa na kuvifuga.
Pamoja na utafiti huo kuonesha kuwa chakula cha seli za saratani ni ‘fructose’, haikukatazwa watu kula matunda ambayo huwa na ‘fructose’, badala yake wameshauriwa kupendelea kula matunda zaidi kuliko juisi yake. Kimsingi ‘fuctose’ asilia iliyomo kwenye matunda haiwezi kuwa na madhara kwa mwili wa binadamu kama ilivyo kwa ‘fructose’ za kutengeza zinazotumika zaidi kwenye vyakula na vinywaji mbalimbali baridi.
Mwisho, pamoja na kuwa kwamba sukari ni bidhaa muhimu kwa matumizi ya binadamu ya kila kila siku na kwamba sukari pia ina faida mwilini, lakini ni vyema ikaeleweka siyo bidhaa salama unayoweza kuitumia utakavyo. Pale ambapo hatuna budi, basi tuitumie kwa uchache sana na pale ambapo tunaweza kuiacha kuitumia kabisa, bora tukafanya hivyo.