Jan 17, 2014
KOCHA MPYA YANGA APEWA MASHARTI
Kocha mkuu wa Yanga SC, Hans van Der Pluijm.
Na Amisa Mmbaga
UONGOZI wa Klabu ya Yanga umempa masharti kocha mpya wa timu yao, Hans Van Der Pluijm kuhusu kudhibiti nidhamu ya wachezaji pindi wanapokuwa kambini na uwanjani ili kuweza kukifikisha mbali kikosi hicho.
Yanga waliondoka nchini hivi karibuni kuelekea Uturuki kwa ajili ya maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, amesema ili kuweza kutoa wachezaji bora na kufanya vizuri kwenye mzunguko ujao, lazima kocha adhibiti nidhamu ya wachezaji.
“Ni kweli tumempa masharti kocha mpya ili aweze kudhibiti nidhamu na kuweza kukijenga kikosi kwa lengo la kufanya vizuri kwenye michuano ijayo.
“Siku zote tunapenda kutoa tahadhari mapema ili tuweze kumuadhibu mchezaji au kocha anapokiuka masharti ya klabu,” alisema Sanga.
Kocha Ernie Brandts ambaye alikuwa akiinoa timu hiyo, alitimuliwa huku sababu kubwa ikiwa ni kushuka kiwango cha timu hiyo pamoja na kushindwa kudhibiti nidhamu kwa wachezaji.