Maalim Hassan Yahya Hussein (kushoto) akihojiwa na mwandishi wa habari.
LEO mnajimu maarufu, Maalim Hassan Yahya Hussein amefanya mkutano na waandishi wa habari. Ametabiri mambo zaidi ya kumi, yasome mwenyewe.
Ndugu Wanahabari
UTANGULIZI:
Mwaka huu tulionao hivi sasa wa 2014 umeanzia siku ya Jumatano, siku hii inatawaliwa Na Sayari ya Mercury, Sayari hii iko Mbingu ya 2, na nyota zake ni mbili nazo ni Mapacha (Gemini) ambayo asili yake ni upepo na Mashuke au (Virgo) ambayo asili yake ni Udongo
Hii sayari ya Mercury inahusika na mambo yanayohusiana na Adabu, Malezi mema, Mantiki, Kupata kitu, Fasihi ya lugha, Ufahamu, Uelewa, Elimu, Urafiki, Hila na kudanganya, Hesabu, Vitabu, Sanaa za aina zote, Ukatibu au Ukarani, Shule au Kumpeleka mtoto shule.
Vile vile inahusiana na mambo ya Nakshi, sanaa masuala ya Urembo, kuandaa Majeshi, nidhamu na mapato.
Mwaka 2014 Mwezi utapatwa mara mbili tarehe 15 Aprili ambayo itakuwa siku ya Jumanne na Oktoba 8 ambayo ni siku ya Jumatano na Jua nalo litapatwa mara mbili tarehe 29 Aprili ambayo ni siku ya Jumapili na Oktoba 23 ambayo itakuwa siku ya Alkhamisi
Nimeyaeleza haya kwa sababu katika Elimu ya Unajimu na Utabiri kupatwa kwa Jua na Mwezi kuna athari za moja kwa moja na matukio yanayotokea hapa Duniani.
Mwaka ukianzia siku ya Jumatano, unaashiria shida kubwa na nyingi sana. Unaashiria kuibuka kwa maradhi mengi, uadui kuwa mwingi kati ya watu au nchi, vimbunga na majanga asilia yanayotokana na upepo, vifo vingi hasa wanaume vijana na Viongozi wa kidini na kisiasa. Aidha, wajawazito kupata shida katika uzazi, Jua kuwa kali sana, Njaa kuwa nyingi na ukame.
Pia wanyama kupata magonjwa, watu kulalamikia mifumo ya kiutawala, watu kurukwa na akili, Ajali kuwa nyingi zitakazosababisha vifo vya watu wengi kwa wakati mmoja, safari kutotimia. Pamoja na hayo, uongo na propaganda kutawala waimbaji, wasanii kufa au kupatwa na kashfa.
Jumatano haioneshi kuwako kwa vita, bali mazao yatakuwa kidogo.
Katika hali hii,
1. Natabiri Mwaka huu kinyota unaashiria shida na maafa makubwa. Maradhi kama vile Malaria, Kuhara, Kuhara Damu, Kichocho vitakuwa vingi iwapo watu au jamii haitajihadhari.
2. Natabiri Uadui wa Taasisi au Chama na Chama utakuwa mkubwa na kuna dalili za kupigana kwa wafuasi wa Vyama Pinzani.
3. Natabiri: Nyota pia zinaonesha kuwa Tanzania itakuwa katika mzozo mkubwa na majirani zake lakini uwezekano wa kupiganwa kwa vita kati sisi na wao hauko.
4. Natabiri: Tahadhari ya hali ya juu inatakiwa iwepo kwani Tanzania inaonekana kuwindwa na mataifa ya mbali ili iingie kwenye vita isipokuwa kwa haiba ya Siku ya Jumatano, vita hivyo vitadhibitiwa kitaifa na kimataifa.
5. Natabiri:- Vifo vya Vijana vikiongozana na mauaji ya kupanga vitakuwa jambo la kawaida kwenye Mwaka huu na wahusika zaidi ni Wasanii wa fani zote wakiwemo Waandishi wa Habari.
6. Natabiri:- Wanasiasa wataendelea kuwa walengwa kwa mambo ya kijamii hasa kashfa za ngono na biashara haramu. Nyota zinaonesha kuwa mmoja wa watu mashuhuri sana hapa nchini atatumbukia kwenye kashfa hiyo na itamuangusha kijamii pale atakaposhughulikiwa kwa kufilisiwa mali na kufungwa kitaifa na kimataifa.
7. Natabiri;- Kwa vile siku ya Jumatano ni siku mbaya katika mwaka, kuna dalili za watu kuswekwa kizuizini kwa kashfa za ukiukwaji wa utiii kwa Serikali na vyombo vyake vya dola.
8. Natabiri;- Kuna kiongozi mmoja wa Kisiasa na kijamii mwenye hadhi kubwa hapa nchini atarukwa na akili kuelekea mwisho wa Mwaka huu na itakuwa anguko lake na wafuasi wake kwenye harakati za kuimarisha Ustawi wa Watanzania na dola yake.
9. Natabiri:- Nyota zinaonesha kuwa kinamama wajawazito watakufa kwa uzazi kutokana na tabia ya kutozingatia mafunzo ya uzazi na taratibu zake. Wengi watashindwa kujifungua na kusababisha wao pamoja wa watoto watarajiwa kufa.
10. Natabiri;- Ukame utaigubika nchi kwa kiasi kikubwa na wananchi watakuwa na wakati mgumu katika mwaka huu kulingana na nyota hasa mwaka unapoanza na siku ya Jumatano. Vimbunga na pepo kali zitatawala mwaka huu.
11. Natabiri;- Kutokana na ukame huo wanyama watakuwa katika wakati mgumu na Tanzania itapoteza asilimia kubwa ya wanyama wake mwaka huu na hivyo kusababisha wafugaji na wakulima kuwa kwenye wakati mgumu kimaisha.
12. Natabiri;- Kelele za kudai haki za kibinadamu zitajitokeza kwenye mwaka huu na kusababisha hali ya mpito ya dharura kutangazwa na wakuu wa nchi. Hatua hiyo itampa Rais ushujaa na utasababisha aendelee kuwa kiongozi mwenye mvuto mkubwa duniani kama alivyokuwa kwa mwaka uliopita.
13. Natabiri:- Pamoja na kwamba muda Bado lakini Nyota bado hazioneshi Tanzania kuongozwa na Rais mwanamke ingawa kuna harakati nyingi zinazotaka iwe hivyo. Hata hivyo natabiri Kupatikana kwa viongozi wengi wanawake au wanawake kushika nafasi kubwa katika siasa.
14. Natabiri:- Katiba mpya ya nchi yetu itapita kwa mbinde, kwani kutakuwa na malumbano na utata mkubwa hasa kuhusu agenda ya serikali tatu. Nyota zinaonesha kuwa Rais Kikwete atatumika zaidi kuweka mambo sawa baada ya jamaii nzima kuweweseka katika hili.
15. Natabiri:- Mwelekeo wa nyota za mwaka huu pia zinaonesha kuwa kutakuwako na majaribio ya kiuhalifu katika uongozi ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vitasababisha tafrani lakini vitadhibitiwa na mambo kwenda sawa-bin-sawia.
16. Natabiri;- Warembo, Wana-filamu, Wanamuziki, Wanasoka, Wanahabari na Wanasiasa wako katika hatari ya kuanguka kihali na mali na kutokana na hilo yakawapo mabadiliko ya mwelekeo wa kimaisha kwao katika mwaka huu kuelekea Uchaguzi Mkuu was Rais, Wabunge na Madiwani mwakani. Hatua hiyo itasababisha pia vifo vya kawaida na vya ghafla kwao.
Mwaka 2014 si mzuri kwao hata hivyo muelekeo wa mafanikio makubwa kwa makundi hayo ni mzuri. Wako baadhi kutoka katika katika makundi hayo niliyoyataja wataula kisiasa na kimataifa.
17. Natabiri: Kiongozi mmoja wa Chama cha Siasa hapa nchini atangolewa kwenye uongozi na kitendo hicho kinaweza kumsababishia anguko kubwa la kisiasa kwake au hata kifo.
18. Natabiri:-Baadhi ya chaguzi za awali za Serikali za Mitaa mwaka huu zitakumbwa na na kizungumkuti kiasi cha kuiingiza nchi yetu kwenye mizozo yenye muelekeo wa mapigano ya kijamii.
19. Natabiri: msiba wenye sura ya kitaifa
20. Natabiri :- Kuna Baadhi ya Wabunge watapata dhoruba kubwa majimboni itakayosababisha kupoteza nyadhifa zao siku za usoni
21. Natabiri :-Mwaka 2014 si mzuri kwa viongozi wa Kidini, wako watakaokufa ghafla, huku baadhi yao wakingolewa madarakani au kwenye mamlaka kwa haiba yenye aibu na kashfa.
22. Natabiri;- Rais atafanya Tukio Kubwa la kutikisa nchi lakini tukio hilo litaleta Neema baadae kama vile heshima kwa Taifa, amani uzalendo, uwajibikaji na staha katika Jamii
Alhajj Maalim Hassan Yahya Hussein
Mrithi wa kazi za Sheikh Yahya Hussein, Bingwa wa utabiri nchini na mtaalamu wa nyota
Jumapili tarehe 5/1/2014