Jan 18, 2014
MWANAMKE ALIYETAPELI KWA AIRTEL MONEY JELA MIEZI 6
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, imemhukumu mkazi wa hapa kwenda jela miezi sita, kwa kosa la utapeli wa fedha kwa njia ya mtandao wa Airtel Money kwa mawakala mbalimbali wilayani humo.
Akitoa hukumu hiyo, Hakim Mkazi Mfawidhi, Joseph Ngomelo, alisema mshitakiwa Helena Alexandria, atakwenda jela miezi sita baada ya kukiri kufanya utapeli huo.
Mshitakiwa huyo alikiri kutapeli mawakala mbalimbali wa Airtel Money waliopo Nzega mjini kwa njia ya mtandao na kujipatia fedha kwa njia isiyo halali.
Alisema kifungo cha mama huyo kitakuwa fundisho kwa wanawake wangine wenye tamaa, kwani makosa kama hayo yakiachiwa yanaweza kuleta madhara makubwa kwa jamii.
Awali Mwendesha Mashitaka wa Polisi Mkaguzi Msaidizi, Melito Ukongoji, aliiambia Mahakama hiyo kuwa Januari mosi mwaka 2014, mshitakiwa ambaye ni mkazi wa Nzega mjini, aliiba kwa kutumia mtandao wa Kampuni ya Airtel Money.
Alidai kuwa Hellena alikuwa akitumia ujumbe mfupi wa maneno wenye muamala wa kutoa pesa Sh 40,000 Airtel Money na kujipatia Sh 40,000 kwa kila wakala kwa nyakati tofauti.
Akijitetea, mshitakiwa alikiri kuhusika na tuhuma hizo kwa nyakati tofauti na kuongeza kuwa lengo lilikuwa ni kutafuta fedha za kujikimu kimaisha kutokana ugumu wa maisha.
Kabla ya kutoa hukumu hiyo Mwendesha Mashitaka aliiomba Mahakama hiyo itoe adhabu kwa mshitakiwa huyo ili iwe fundisho kwa watu wenye tabia kama hizo za wizi wa utapeli kwa njia ya mtandao.
CHANZO HABARI LEO