Jan 6, 2014
MWISHO WA ZITTO CHADEMA LEO?
HATIMA ya safari ya kisiasa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe huenda ikaanza kuonekana leo pale Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi katika shauri alilolifikisha.
Zitto, alifungua kesi katika mahakama hiyo akiitaka iizuie Kamati Kuu (CC) ya CHADEMA iliyokutana kwa siku mbili jijini Dar es Salaam isijadili juu ya uanachama wake hadi rufaa yake aliyoikata kwa Baraza Kuu la chama hicho itakaposikilizwa.
Jaji John Utamwa anayeisikiliza kesi hiyo, mwishoni mwa wiki alitoa zuio la muda kwa CHADEMA kutojadili uanachama wa Zitto hadi leo atakapotoa hukumu.
Mwishoni mwa mwaka jana, CHADEMA iliwavua nyadhifa zote Zitto, Dk. Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, kwa madai ya kukisaliti na kukihujumu chama kwa kuandaa waraka wenye mikakati ya mapinduzi.
Hata hivyo, Mwigamba na Kitila, juzi walivuliwa uanachama baada ya CC kusikiliza utetezi wao na kujiridhisha na tuhuma zilizokuwa zikiwakabili makada hao.
Kuvuliwa uanachama kwa makada hao wawili kumezidisha hofu kwa wapenzi, mashabiki wa Zitto ambaye kama isingekuwa zuio la mahakama, uanachama wake pia ungejadiliwa kikao cha CC kilichomalizika juzi.
Kitendo cha Zitto kukifikisha mahakamani chama chake, kimemjengea chuki miongoni mwa wapenzi, wanachama na mashabiki wa chama hicho waliokuwa wakimuona shujaa siku za nyuma.
Tayari wanachama wa chama hicho wiki iliyopita walipigana mahakamani baada ya kuzuka kwa pande mbili moja iliyokuwa ikimuunga mkono, na nyingine ikimpinga.
Pande hizo zilikuwa na mabango yaliyokuwa yakionyesha kupinga na mengine kuunga mkono hatua hiyo ya Zitto kukifikisha chama chake mahakamani.
Tanzania Daima limedokezwa kuwa leo idadi kubwa ya watu inatarajia kufurika mahakamani kujua hatma ya Zitto.
Zitto, anaweza kuingia katika historia ya kuwa mbunge wa mahakama iwapo uamuzi utakaotolewa utakuwa ni kuendelea kuizuia CHADEMA isijadili uanachama wake.
Mbunge huyo anaweza akaungana na David Kafulila (NCCR-Mageuzi) na Hamad Rashid Mohamed (CUF) ambao vyama vyao viliwavua uanachama kwa madai ya kukiuka taratibu za chama ikiwemo kuwashutumu viongozi wakuu hadharani.
Kafulila na Hamad walikimbilia mahakamani ambako walipata ahueni ya kuendelea kuwa wabunge wakati suala lao likitafutiwa ufumbuzi.
Baadhi ya makada waliozungumza na Tanzania Daima, waliweka bayana kushangazwa na hatua ya Zitto kupeleka suala hilo mahakamani wakati alishawasilisha utetezi kwenye chama chake.
Hoja waliyoijenga makada hao ni kuwa mbunge huyo anapata hofu gani ya kusikiliza majibu ya utetezi aliouwasilisha katika chama chake.
Habari zilizolifikia Tanzania Daima, zinabainisha kuwa Zitto alifikia uamuzi wa kwenda mahakamani baada ya kudokezwa kuwa wajumbe wengi wamedhamiria afukuzwe uanachama kama ilivyotokea kwa Dk. Kitila na Mwigamba.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, baadhi ya wajumbe walikuwa wakifanya ushawishi kwa wenzao ili waunge mkono hoja ya kumvua uanachama Zitto pindi wakianza kumjadili.
Inadaiwa kuwa wajumbe hao walichoshwa na vitendo vya mbunge huyo kukiumiza chama na viongozi wakuu katika mikutano aliyoifanya mkoani Kigoma hivi karibuni.
Kwamba wajumbe hao waliona ni heri CHADEMA ikose Jimbo la Kigoma Kaskazini kuliko kuendelea kuwa na Zitto ndani ya chama hicho.
Vyovyote inavyokuwa, uamuzi wa mahakama leo ndio utakaotoa hatima ya uanachama na hatimaye ubunge wa Zitto.
CHANZO NI TANZANIA DAIMA