Jan 26, 2014
PROFESA BAREGU AFICHUA SIRI YA USALITI CHADEMA
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Profesa Mwesiga Baregu, amefichua siri ya madai ya usaliti ndani ya chama hicho.
Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu yaliyofanyika jijini Dar es Salaam wiki hii, Profesa Baregu alisema kiini cha tuhuma na madai ya usaliti ndani ya Chadema ni kutoaminiana na kukosekana kwa uvumilivu.
Alisema kitendo cha wanachama na viongozi kunyoosheana vidole vya usaliti kinakiangusha chama na kwamba Chadema kimefeli katika mambo matatu, ambayo ndiyo yanapaswa kuwa msingi wa chama na kama yangezingatiwa mapema, hoja ya usaliti isingezungumzwa leo.
Aliyataja mambo hayo yanayozalisha hoja nzito ya usaliti iliyosababisha baadhi ya wanachama wa chama hicho kuvuliwa uanachama kuwa ni kusikilizana, kuvumiliana na kuaminiana.
“Kukosekana kwa mambo hayo ndio kiini cha kuibuka kwa hoja ya usaliti, hatua hii ni mbaya katika maendeleo ya chama kinachojijengea uaminifu kwa wananchi,” alisema.
Alisema kuendelea kwa hali ya kushutumiana ndani ya chama kunasaidia kukitafuna na ipo siku Chadema haitakuwa na mtu msafi, kwani wote wataitana wasaliti.
“Chadema ni chama kizuri cha siasa, lakini kimefeli kabisa katika kuyadhibiti mambo hayo matatu muhimu, nadhani hili ni tatizo kubwa linalokiandama chama hiki.
“Matokeo ya hali hii ndiyo yanayozalisha mivutano isiyokuwa na tija, huyu kasema hivi yule naye anasema vile, hakuna mtu wa kumsikiliza mwenzake na kibaya zaidi watu ndani ya chama hawaaminiani, utasikia leo huyu katajwa msaliti, kesho yule, utafika wakati chama hakitakuwa na msafi, wanachama wote watakuwa wasaliti,” alisema Profesa Baregu.
Akizungumzia mgogoro wa hivi karibuni ndani ya chama hicho uliosababisha Samson Mwigamba na Dk. Kitila Mkumbo kuvuliwa uanachama, huku Zitto Kabwe akikimbilia mahakamani, Profesa Baregu alisema hayo ni madhara ya kutotumia hekima na kukosekana kwa busara ya kumaliza tofauti kwa mazungumzo.
“Kama hamsikilizani wala kuaminiana, lazima athari ziwepo, tena kubwa tu, kwa sababu matukio ya namna hiyo yanakuwa endelevu, leo kashutumiwa huyu ni msaliti, huwezi kujua mwingine atashutumiwa lini …na mvurugano uliotokea hivi karibuni ndio uhalisia wa kile nilichokisema hapo awali, kwamba ndani ya Chadema kumekosekana utamaduni wa kumaliza tofauti kwa mazungumzo, kwa ujumla watu hawavumiliani wala kusikilizana,” alisema Profesa Baregu.
Aidha alitahadharisha kwa kusema, usaliti utakidhoofisha chama kwa kiasi kikubwa, ambapo alikitolea mfano Chama cha NCCR-Mageuzi, ambacho kilikumbwa na mazingira kama hayo na mwisho wake kikaparaganyika ovyo kwa sababu kila mtu alijikuta anatazamwa kuwa msaliti.
Wakati huo huo, imebainika kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini haijatoa mwongozo wowote juu ya barua iliyoandikiwa na Mwigamba, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Arusha. Mwigamba aliitaka ofisi hiyo iingilie kati suala la kunyofolewa kinyemela kwa kipengele cha ukomo wa madaraka kwenye katiba ya chama hicho.
Inaelezwa kuwa Mwigamba alifikia hatua ya kuandika barua hiyo kabla hajavuliwa uanachama, ambapo alifanya hivyo baada ya kutokea sintofahamu baina ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto, Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na wafuasi wanaomuunga mkono Mbowe.
Akithibitisha madai hayo, Mwigamba alisema ni kweli kuwa alimwandikia barua Msajili, ambayo ilikuwa ikihoji ukiukwaji wa katiba ya chama pamoja na kuondolewa kwa kipingele cha ukomo wa muda wa uongozi, hata hivyo mpaka sasa hajapatiwa majibu.
Alisema mara baada ya kuandika barua hiyo, Msajili aliwaandikia Chadema ili kupata ufafanuzi wa madai hayo, ambapo walijibu kuwa walisambaza waraka kwa makatibu wa chama hicho wa mikoa ili kupata uungwaji mkono kabla ya kukiondoa.
Hata hivyo, Mwigamba alilalamikia hatua hiyo kwa madai kuwa inakiuka katiba na utaratibu wa chama hicho na kwamba barua iliyosainiwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Shaibu Akwilombe, Julai 13, 2006, kwenda kwa makatibu hao ilikuwa ikiwaarifu kuwa yanapelekwa mapendekezo ya ziada.
Kwamba waunge mkono pendekezo kuwa Katibu Mkuu na manaibu wawili wateuliwe na Mwenyekiti, wasipigiwe kura na majina yao yapelekwe Baraza Kuu kwa ajili ya kupiga kura kuchagua mmoja.
“Katiba ya mwaka 2006 isomeke pia kiongozi anaweza kuchaguliwa tena na ndiyo walileta mapendekezo na mwanzo mpaka mwisho wa barua ilikuwa inaongelea mapendekezo tu. Msajili alinitumia nakala ya majibu yao ili nitoe maelezo ya ziada, ambayo pia nilishafanya hivyo tangu Desemba 30 mwaka jana,” alisema Mwigamba.
Alisema kuwa katika majibu ya Chadema ya Desemba mwaka jana kwa Msajili, yalionesha wazi kwamba Mwigamba alishavuliwa uanachama wa chama hicho, wakati alikuwa bado hajafukuzwa, ambapo walidai kwamba kipengele hicho kilifanyiwa marekebisho.
“Nilimweleza Msajili kuwa katiba ya Chadema, inataka mapendekezo ya katiba yapelekwe kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu, siku 30 kabla ya mkutano huo, ukizingatia kikao cha Mkutano Mkuu kilifanyika Agosti 13, 2006 na kufanya mabadiliko ya Katiba Julai 13, mwaka huo huo ndiyo iliandikwa barua, sasa hata kama barua ingesafirishwa kwa ndege ama kwa usafiri wowote lazima zingeanza kupokelewa kuanzia Julai 14 mpaka 16, hapo tayari siku zimepungua, si 30 tena,” alisema Mwigamba.
Alisema kuwa waraka huo uliosambazwa kwa wajumbe ulitakiwa kuwafikia siku 30 kabla na kwamba haukueleza iwapo mapendekezo hayo yaliandaliwa na Baraza Kuu ambalo linatoa mapendekezo kwa Mkutano Mkuu au la!
Alisema waraka huo, ambao alibahatika kuuona, ulikuwa hauna uzito unaostaili, kwani ulikuwa sawa na barua ya uchumba ambayo ni tofauti na cheti cha ndoa unachoweza kupeleka ushahidi Mahakamani.
Anasema wakati barua ya Akwilombe ikisambazwa ilikuwa pamoja na rasimu, ambapo yeye (Mwigamba) akiwa mmoja wa Makatibu wa Wilaya hakuona nakala yake.
Gazeti hili lilimtafuta Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, ili kupata ufafanuzi, hata hivyo hakuweza kupatikana, kutokana na kuwa katika vikao, huku simu yake ya kiganjani ikiwa haipatikani.
Alipotafutwa Msemaji wa Chadema, Tumaini Mkene, alishindwa kujibu moja kwa moja swali aliloulizwa, ambapo alisema suala hilo lilishazungumzwa katika mkutano wa waandishi wa habari na majibu yake yanajitosheleza.