Ariel Sharon,
Na RFI
liyekuwa Waziri Mkuu wa Isreal Ariel Sharon atazikwa leo nyumbani kwake katika jangwa la Negev katika mazishi ya kitaifa yatakayoongozwa na jeshi la taifa hilo. Miongoni mwa wageni mashuhuri watakaohudhuria mazishi hayo ni pamoja na Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden, Waziri wa Mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov, Msuluhishi wa Kimataifa wa maswala ya Mashariki ya Kati Tony blair.
Siku ya Jumapili, maelfu ya raia wa Israel walipata naafsi ya kuuona mwili wa Sharon katika majengo ya bunge mjini Jerusalem.
Ariel Sharon alifariki dunia juzi jumamosi, akiwa na umri wa miaka 85 baada ya kuwa katika hali mahututi kwa miaka minane.
Sharon atakumbukwa sana ndani na nje ya Israel kutokana na ukakamavu wake wa kijeshi na uongozi wa taifa hilo hasa wakati wa makabiliano na Palestina alipokuwa uongozini kati ya mwaka 2001 na 2006.
Wakosoaji wake wanasema kuwepo kwake uongozini kama Waziri Mkuui wa 11 nchini Israel kulisababisha umwagaji damu katika Mamlaka ya Palestina.
Sharon ambaye anasherehekewa na baadhi kama shujaa wa kijeshi, na wengine wakimtambua kama mwanasiasa aliyeendesha siasa za vitendo,huku maadui zake wakimwona kama mhalifu wa makosa ya jinai, Sharon alikuwa mtu wa mgawanyiko nyumbani na nje ya nchi yake.
Viongozi mbalimbali duniani wametuma salamu za rambi rambi kwa taifa la Israel akiwemo rais wa Marekani Barack Obama ambaye amemwelezea Sharon kama kiongozi aliyeyatoa maisha yake kwa ajili ya taifa la Israel.