MY ADVERT EA SHOWBIZ

MY ADVERT EA SHOWBIZ

SIX OFFICE SOLUTION

MOCHRISPO

DARDY FASHION

Feb 19, 2014

ENDELEENI KUFICHUA UNYANYASAJI KWA WANAWAKE, WATOTO – TAMWA



                                         Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Dk. Valery Msoka.

Na Walusanga Ndaki
VYOMBO vya habari vimetakiwa kuandika zaidi habari zinazohusu unyanyasaji wa kijinsia hususan dhidi ya wanawake na watoto ili kuiamsha zaidi jamii inayowafanyiwa vitendo hivyo na mamlaka husika ziweze kuchukua hatua za kisheria dhidi ya vitendo hivyo.

Msisitizo huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) kwa wahariri wa vyombo vya habari ambapo vyombo hivyo viliombwa kuendelea kufichua habari hizo hususan kwa wanaofanyiwa vitendo hivyo ili waweze kuelewa kwamba sheria dhidi ya ukatili huo zipo na kwamba kuna taasisi za kuwatetea.

Akizungumza na wahariri hao kuhusu mpango wa kutokomeza manyanyaso ya aina hiyo kwa kuwawezesha kihali na mali wanawake na watoto (GEWE), Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Dk. Valery Msoka,  alisema licha ya kufanikiwa kwa mpango huo ambapo kiwango cha ukatili huo ni dhahiri kimepungua kutokana na wanaofanya ukatili huo kuelewa, na watendewa pia kuzidi kuamka, juhudi zaidi zilitakiwa kujipenyeza zaidi dhidi ya imani za kimila ambazo bado zinashikiliwa katika sehemu mbalimbali za nchi.

“Endeleeni kutumia kalamu zenu na vifaa vyenu vyote kupiga vita vitendo vyote vinavyotokana na manyanyaso ya kijinsia ambayo hasa hutokana na mfumo dume,” alisema Msoka akiwaomba wahariri kufanya hivyo kwa ajili ya kuendeleza juhudi za kuungwa mkono kwa taasisi hiyo kutoka kwa watu wanaoiunga mkono ndani na nje ya nchi.

Msoka ambaye ni mmoja wa wajumbe wa bunge maalum litakalojadili rasimu ya katiba, aliwataka wahariri –hususani wanawake – kupaza sauti zao zaidi kwa kuunga mkono juhudi za wajumbe wengine na wananchi kwa jumla ili kupatikana kwa katiba ambayo italeta heshima kwa wanawake wote, hususan wale walioko pembezoni mwa jamii na wasioelewa haki zao.

Mpango wa GEWE umekuwa ukiendesha harakati na utafiti wake katika  wilaya kumi nchini kuhusiana na  masuala ya ubakaji, ndoa za utotoni, ukeketaji, utelekezaji wa watoto na vipigo kwa wanawake na watoto ambavyo kwa kiasi kikubwa hufanywa na wanaume.