Feb 3, 2014
Kigogo wa zamani BOT atupiwa vyombo nje
Mkurugenzi wa zamani wa Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Elisa Issangya, akiwa ameduwaa baada ya vyombo vyake kutolewa nje ya nyumba na Kampuni ya Udalali ya Mwafrika jana. Picha na silivan Kiwale
Dar es Salaam. Mkurugenzi wa zamani wa Fedha wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Elisa Issangya amejikuta akitupiwa vyombo vyake nje na Kampuni ya Udalali ya Mwafrika kwa kile kilichoelezwa kutakiwa kuondoka kwenye nyumba aliyokuwa akiishi.
Nyumba hiyo iliyoko Mtaa wa Ruhinde Block 2 Plot 294 eneo la Ada Estate wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, inaelezwa kuwa inamilikiwa na BoT.
Akizungumza nyumbani kwake baada ya kutupiwa nje vifaa vyake, Issangya alisema: “Nimeshtukizwa na maofisa wa Kampuni ya Udalali ya Mwafrika kuingia ndani kwangu na kuniomba nishirikiane nao kutoa vitu vyangu nje.
“Maofisa hao wa Kampuni ya Mwafrika walifika nyumbani kwangu asubuhi na kunionyesha barua kutoka BoT ya kunitaka kuvitoa vyombo vyangu nje, sikukubaliana nao, nikaamua kwenda polisi kutoa taarifa,” alisema.
Alisema wakiwa polisi na ofisa mmoja wa kampuni hiyo aliyemtaja kwa jina moja la Gama ambaye alikuwa akimweleza kuwa, watamuelewesha suala hilo baada ya kuondoa vyombo hivyo , lakini waliporejea nyumbani kwake, walikuta vyombo vyote vimetupwa nje.
Issangya alisema kitendo cha kutupiwa vifaa nje ni udhalilishaji kwani walitakiwa kwenda nyumbani kwake wakiwa na barua ya mahakama ya kuwaruhusu kufanya hivyo.
“Nimeshangaa hatua hiyo wakati mpaka sasa kesi yangu ya kudai haki zangu ipo mahakamani, wangesubiri mpaka hukumu ikitolewa ndipo waje na uamuzi huu,” alilalamika Issangya aliyeteuliwa kushika nafasi ya Mkurugenzi wa Fedha wa BoT mwaka 2000 kabla ya kusimamishwa 2008.
Alipoulzwa sababu za kufanya hivyo wakati suala la mlalamikaji bado liko katika vyombo vya sheria na uamuzi wa shauri haujafikiwa, Ofisa wa Kampuni hiyo ya Udalali, Joseph Gama alisema kuwa wanatekeleza maagizo ya tajiri wao na si vinginevyo.
“Sisi tunafanya kazi kwa amri ya tajiri wetu, hatuwezi kufanya mambo kinyume na maelekezo, tumeelekezwa na huu ni utekelezaji wake,” alisema.