Katibu
Mkuu wa Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es salaam kabla ya kukabidhi mabasi 6 kwa wakuu wa vyuo
vya Afya kutoka katika maeneo mbalimbali .Mabasi hayo yatasaidia
kuaondoa upotevu
wa muda na adha ya usafiri waliyokuwa wakiipata wanafunzi,watumishi na
wakufunzi wa vyuo hivyo kufika kwenye maeneo ya mafunzo kwa vitendo.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo akikata utepe kwenye basi moja
kati ya sita yaliyonunuliwa kwa ufadhili wa Mradi wa Mfuko wa Dunia
mzunguko wa 9 ambayo yamekabidhiwa kwa wakuu wa vyuo vya afya leo jijini
Dar es salaam.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo akikagua mabasi hayo yaliyonunuliwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Dunia mzunguko wa 9
ambayo yamekabidhiwa kwa wakuu wa vyuo 6 vya afya leo jijini Dar es
salaam.
Sehemu ya ndani ya mabasi hayo yaliyotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Mradi wa Mfuko wa Dunia.
Picha na Aron Msigwa -MAELEZO.
======== ======= =========
WIZARA YA AFYA
YAKABIDHI MABASI 6 KWA VYUO VYA AFYA NCHINI.
Na. Aron Msigwa –
MAELEZO
25/9/2014. Dar es
salaam.
Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii imekabidhi mabasi 6 kwa vyuo vya elimu ya Afya kwa lengo la kurahisisha
huduma ya usafiri kwa wanafunzi na wakufunzi wanaokwenda kwenye mafunzo kwa vitendo
katika maeneo mbalimbali nchini.
Vyuo vilivyokabidhiwa
mabasi hayo ni Chuo Kikuu cha Hurbert Kairuki Memorial (HKMU) kilichopo jijini
Dar es salaam, Chuo cha Uuuguzi Bagamoyo,Chuo cha Uuguzi Mirembe mkoani Dodoma,
Chuo cha Uuguzi Tanga na Chuo cha Tabibu kilichopo mkoani Mtwara.
Akikabidhi mabasi hayo
kwa wakuu wa vyuo hivyo leo jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo amesema mabasi hayo yatasaidia kuaondoa upotevu
wa muda na adha ya usafiri waliyokuwa wakiipata wanafunzi,watumishi na
wakufunzi wa vyuo hivyo kufika kwenye maeneo ya mafunzo kwa vitendo.
“Ninakabidhi magari
haya kwenu leo hii yakafanye kazi za kuwahudumia watumishi na wakufunzi wa
maeneo yenu ya kazi, Ni wajibu wenu kuhakikisha mnayatunza na kuyafanyia
matengenezo kulingana na miongozo iliyopo ili yaweze kudumu” Amesisitiza.
Amesema mabasi hayo 6
yamenunuliwa kwa gharama ya shilingi
milioni 344 kupitia ufadhili wa Mradi wa Mfuko wa Dunia mzunguko wa 9 ambao
pamoja na mambo mengine unaisaidia Wizara katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya
uzalishaji wa rasilimali watu wa kutoa huduma za afya nchini.
Bw.Pallangyo ameeleza
kuwa serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeendelea kujenga
uwezo kwa wataalam wa sekta ya afya hapa nchini ,kuongeza udahili kwa wanafunzi
kwa lengo kuzalisha rasilimali watu wa kutoa huduma za afya katika maeneo
mbalimbali nchini .
Amesema kutokana na
kuongezeka kwa kasi ya udahili wa wanafunzi wa fani za afya, Serikali
imeendelea kuvijengea uwezo vyuo hivyo kwa kujenga majengo mapya na kupanua yaliyopo
ili yaweze kutumiwa na wanafunzi wengi zaidi wa fani za afya.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Mafuzo wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Otilia Gowelle
akizungumza kabla ya makabidhiano ya magari hayo amesema kuwa Serikali imekuwa
ikifanya juhudi ya kuhakikisha kuwa wanafunzi walio katika mafunzo ya kada
mbalimbali za afya wanajengewa uwezo kwa kuboreshewa miundombinu, majengo,
vifaa vya mafunzo vya maabara ili kurahisha mafunzo yao kwa vitendo.
Amesema kupatikana kwa
mabasi hayo 6 ni sehemu ya mpango wa Wizara wa kuwawezesha wanafunzi wa vyuo
hivyo kwenda kwenye maeneo ya mafunzo kwa vitendo nje ya vyuo wanavyosoma kwa urahisi zaidi.
Nao baadhi ya wakuu wa
vyuo hivyo vilivyopokea mabasi hayo Prof. Boniface Msamati wa Chuo Kikuu cha
Hubert Kairuki cha jijini Dar es salaam na Mkuu wa Chuo cha Uuguzi Tanga ,Thomas
Marato wakizungumza kwa niaba ya wenzao mara baada ya kupokea mabasi hayo wameishukuru
serikali kwa kuwaondolea kero ya usafiri wanafunzi katika vyuo vyao.
Wamesema mabasi hayo
yatatumika kuwasafirisha wanafunzi na wakufunzi kwenda katika maeneo mbalimbali
nchini na kuwaondolea adha ya kukodi magari kwa fedha nyingi kwa lengo la kuwapeleka wanafunzi wao kwenye
mafunzo kwa vitendo katika maeneo yaliyo nje ya vyuo hivyo.
NA JIACHIE BLOG/WAMBURABABU BLOG