Na Mathias Canal,Mjengwablog-Iringa
Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeanza mikutano yake ya nchi nzima
kama ilivyotangazwa na katibu mkuu wa chama hicho Dkt Wilbroad Slaa,
hivi karibuni alipozungumza na vyombo vya habari ofisini kwake Jijini
Dar es Salaam.
Chadema
kimeridhia kufanya mikutano nchi nzima ambapo katika mkoa wa
Iringa
mkutano huo ulianza jana katika viwanja vya Mlandege kwa kuhutubiwa na
viongozi mbalimbali wakiongozwa na Makamu mwenyekiti wa CHADEMA Prof
Abdalla Safari
Akizungumza
na mamia ya watu waliojitokeza katika mkutano huo ambao imeelezwa kuwa
haujawahi kutokea mkutano kuwa na wimbi la watu kama hao, amesema kuwa
ukombozi wa nchi ya Tanzania umetokana na damu ya watanzania hivyo
hakukuwa na sababu ya watanzania kuishi maisha ya umasikini kama ilivyo
kwa nchi kama hii yenye rasilimali nyingi ikiwa ni pamoja na misitu,
madini na ardhi ya kutosha.(P.T)
Safari
alisema kuwa wananchi wa Botswana wanafaidika na madini ya nchi yao kwa
serikali kukusanya 70% ya madini huku nchi kama Tanzania ikichukua 5% ya
madini, hivyo ni dhahiri kuwa Uwezo duni wa kufikiri kwa viongozi wa
Tanzania ndio sababu ya umasikini wa Watanzania na utajiri wa wananchi
wachache (Mafisadi).
"Pia
nawaahidi kwamba UKAWA tumeridhia kusimamisha mgombea mmoja kwenye
uchaguzi kuanzia ngazi ya serikali za mtaa hadi Taifa, lakini kubwa
zaidi tunataraji kwenda mahakamani kuzuia mchakato wa katiba kukusanya
maoni ya wananchi" Alisema Safari
Hata
hivyo Katibu mkuu wa CHADEMA Taifa, Dkt Wilbroad Slaa amesema kuwa kuna
daftari la mkazi linapita mtaani hivyo wananchi wanapaswa kujiandikisha
kwa wingi ili wawe na uwezo wa kupiga kura sambamba na kujitokeza
kuwania nafasi za uongozi wa serikali za mitaa.
"Mnapaswa
kutambua kuwa siku 21 kabla ya kupiga kura ni muda wa kujiandikisha
hivyo kila mmoja ajiandikishe na kuhamasisha wengine, nachukua nafasi
hii kuwakumbusha kuwa uzembe wa wanachadema ndio ushindi wa CCM" Alisema
Slaa.
Slaa
alisema kuwa CCM imeshindwa kutoa elimu bure kwa watanzania kuanzia
shule ya msingi hadi chuo kikuu tangu waingie madarakani hivyo
wasitegemee kufanikiwa kwa kipindi kifupi kilichosalia.
Naye
mbunge wa Jimbo la Iringa mjini Mch Peter Msigwa alijibu mapigo ya
Katibu mkuu wa CCM Taifa, Abdulrahman Kinana alipozuru Mkoani Iringa
hivi karibuni, alisema katibu huyo alitumia muda mwingi katika mkutano
wake kumzungumzia badala ya kuzungumzia maendeleo ya nchi.
"Nilishinda
kwa ushindi mnono mwaka 2010 kwenye uchaguzi mkuu hivyo nawaomba
msikubali kupotoshwa na propaganda ya kwamba nilishinda baada ya CCM
kujichanganya, tuna mambo mengi ya kuzungumza lakini tutaendelea kuonana
mara kwa mara kwani muda wetu hautoshi, wapo waliosema mimi na Chiku
Abwao tuna ugomvi hivyo ni rahisi kukomboa Jimbo la Iringa Mjini, hilo
lisahaulike naamini mmemsikia wenyewe Chiku alichokisema"
Msigwa
alisema kuwa kuhusu mfuko wa jimbo ameanza kupita kila Kata ili kutoa
ufafanuzi kwa kina kwa kile kilichofanyika hatimaye watanzania
kutopotoshwa na baadhi ya wanasiasa.
Kwa
upande wake Salumu Mwalimu ambaye ni Naibu Katibu mkuu wa Chadema
Zanzibar amesema kuwa, Chadema kinaamini katika vijana ndio maana wengi
wao ni viongozi na ufanisi wa hoja unaonekana.
Mwalimu
alitumia nafasi hiyo pia kumuomba ruhusa Katibu mkuu wa chama hicho ili
kurejea tena mkoani Iringa kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa lengo
ikiwa ni kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kujiandikisha na
kujitokeza katika kuwania nafasi za serikali za mtaa.
Viongozi
wengine waliohudhuria katika mkutano huo ni pamoja na Patrick Ole Sosopi
Makamu Mwenyekiti BAVICHA Taifa sambamba na Chiku Abwao Mbunge wa viti
maalum Mkoa wa Iringa