Wakati Rais Jakaya Kikwete wa
Tanzania na Rais wa Zanzibar, Dr Ali Mohammed Shein, leo jioni
wakitarajiwa kukabidhiwa rasimu ya katiba iliyopitishwa na Bunge Maalum
la Katiba, nchi hiyo inajikuta ikiwa katika mgawanyiko wa kisiasa ambao
haujashuhudiwa kwa muda mrefu.
Hassan Mhelela anatathmini mchakato mzima wa kusaka katiba mpya na changamoto zake.Rasimu hiyo ya katiba ilipitishwa kwa kura ya ndiyo ya wajumbe wengi wa chama tawala CCM na wale wa kundi maalum, huku wajumbe wa vyama vya upinzani wakisusia na wala hawakushiriki katika kupiga kura ya
mwisho
Kwa sasa imeweza kuvuka hatua kuu mbili, kinachofuata baada ya Rais Kikwete kukabidhiwa itakuwa ni kupigiwa kura ya maoni na wananchi, lakini bado barabara ya kuifikia katiba kamili imejaa visiki na utelezi.
Katika hatua hiyo bado hakuna uhakika endapo itafanyika ndani ya miezi sita iliyopangwa kwa mujibu wa sheria, au kazi hiyo itasogezwa mpaka mwaka 2016 baada ya uchaguzi mkuu wa 2015.
Lakini kizingiti kingine ambacho katiba itakabiliwa nacho ni kuoanisha katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kuendana na katiba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar – zinazounda Muungano wa Tanzania.
Ikumbukwe kuwa kabla ya mabadiliko haya kuanza mwaka jana, Zanzibar ilikuwa imefanya mabadiliko ya katiba yake mwaka 2010 kama hatua mojawapo ya maridhiano ya amani yaliyomaliza uhasama kati ya chama tawala CCM na upinzani CUF.
Swali la kujiuliza ni kwamba kutokana na msimamo wa wajumbe kutoka Zanzibar kupinga rasimu hiyo, je watakubali kufanya mabadiliko katika katiba ya Zanzibar ili iendane na rasimu inayopendekezwa, na lini litafanyika hilo?
Kimsingi ili mabadiliko ya katiba ya Zanzibar yafanyike inatakiwa ipitie katika Baraza la Wawakilishi (sawa na Bunge la Zanzibar) na baada ya hapo iidhinishwe kwa theluthi tatu ya kura ya maoni ya wananchi wa Zanzibar.
Kwa upande mwingine, maswala makubwa yaliyosababisha mgawanyiko ni muundo wa serikali – ziendelee kuwa mbili kama ilivyo sasa au ziwe tatu kama rasimu ya kwanza na ya pili zilivyopendekezwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania Jaji Joseph Warioba?
Hapo katikati kumetokea mvurugano ambao umeacha maswali mengi zaidi kuliko majibu yanayotoa ufumbuzi – hata tume iliyokusanya maoni imekuwa imepuuzwa na wajumbe wake kurushiwa vijembe kutoka nje na ndani ya Bunge Maalum la Katiba kuwa iliegemea upande mmoja.
Rais wa Zanzibar Dr Ali Mohammed Shein amemfukuza kazi aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman kutokana na msimamo wake wa kupinga rasimu hiyo ya katiba.
Nafasi yake imechukuliwa na Said Hassan Said, aliyetangazwa siku moja kabla ya rasimu kukabidhiwa kwa Rais Kikwete na Rais Shein wa Zanzibar.
Huo ni msimamo ambao ni nadra sana kujitokeza hadharani katika siasa za Tanzania, na wachambuzi wa mambo wanasema haishangazi kuona hatua zilizochukuliwa.
Vile vile waliokuwa wajumbe wa tume hiyo wamekanusha kupendelea upande wowote, badala yake wameeleza kuwa walichowasilisha ni maoni ya watanzania.
Ingawa chama kikuu cha upinzani CHADEMA kimejaribu kuhamasisha maandamano ya nchi nzima kupinga mchakato huo wa katiba, hakijapata mafanikio makubwa kutokana na serikali kutumia vyombo vya dola kudhibiti maandamano hayo.
Jambo la kusubiri kwa hamu ni kuona kama Rais Kikwete atatoa hotuba itakayojaribu kuwaunganisha watanzania wakijiandaa na hatua inayofuata ya katiba, au atawapuuza wapinzani na wananchi wanaopinga rasimu hiyo.
Ikumbukwe kwamba mwezi uliopita Rais Kikwete na viongozi wa vyama vya siasa Tanzania ikiwemo chama chake cha CCM, walikubaliana kuwa mchakato wa kupata katiba mpya usimame baada ya hatua hii ya Bunge hadi baada ya uchaguzi mkuu.
Hata hivyo suala hilo pia linategemea kuzua mvutano mwingine wa kisheria kwakuwa sheria ya kuanzisha mchakato wa katiba inataka rasimu ikitoka Bungeni ipelekwe kwa wananchi ndani ya miezi sita.
CHANZO BBC