Kamanda wa polisi mkoani Mwanza Valentino Mlowola
Nchini Tanzania katika Kijiji cha
Ndami, tarafa ya Mwamashimba wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza watu
wasiofahamika wamevunja nyumba na kumteka mtoto mwenye ulemavu wa ngozi
maarufu kama albino na kutoweka naye.
Watu hao walivamia nyumba ya
wazazi wa mtoto Pendo Emmanuel, mwenye ulemavu wa ngozi wakiwa na
mapanga na kisha kutoweka naye gizani baada ya kuwazidi nguvu wazazi
wake.Emmanuel Shilinde mzazi wa mtoto huyo ameieleza polisi kuwa majira ya saa nne usiku watu wawili waliuvunja mlango wa nyumba yake kwa jiwe wakamchukua mtoto kwa nguvu kisha wakakimbilia gizani kwa pikipiki.
Kamishina msaidizi mwandamizi wa polisi mkoani mwanza Valentino Mlowola , ameitaarifu BBC kuwa leo ni siku ya tatu na polisi bado ina matumaini ya kumpata akiwa hai motto huyo, kwa kuwa bado hawajaupata mwili wake akiwa amepoteza uhai. Msako unaendelea na tayari kuna watu watano wanazuiliwa na polisi ili kusaidia kufahamu mtoto huyo yuko wapi.
Takwimu za kuanzia mwaka 2006 zinaonyesha kuwa Albino 74 wameshauawa kikatili, huku 56 wakinusurika kifo, na kati yao 11 wamepata ulemavu mwingine wa kudumu.