Nchini Tanzania mtikisiko wa matokeo ya kashfa ya Akaunti ya Tegeta
Escrow umeendelea baada ya Katibu Mkuu wa wizara ya Nishati na Madini
Eliakim Maswi kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi dhidi yake. Maswi
anakuwa kiongozi wa tatu wa ngazi ya juu kukumbwa na upepo huo
akitanguliwa na Mwanasheria mkuu wa serikali ambaye alijiuzulu mwenyewe
na Waziri wa Ardhi aliyetimuliwa kazi hadharani na Rais Jakaya Kikwete.
Licha ya kuondoka kwa viongozi hao bado baadhi ya wananchi na vyama vya
upinzani wameendelea kulalamika kuwa juhudi za kutekeleza maazimio ya
Bunge ni ndogo. Kuhusiana na hilo Baruan Muhuza wa BBC alizungumza na
Neville Meena, katibu wa Jukwaa la wahariri Tanzania.