WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali imeamua kutafuta soko la utalii
kutoka nchi za Ghuba na Mashariki ya Kati ili kuongeza idadi ya watalii
nchini na kukuza pato la Taifa kupitia sekta hiyo.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumatano, Desemba 17, 2014) wakati akizungmuza
an waandishi wa habari mara baada ya kufungua Kongamano la siku mbili la
Utalii na Uwekezaji lilionza leo kwenye hoteli ya Le Meridien, jijini
Dubai, Falme za Kiarabu.
“Tunao
mkakati wa kukuza utalii nchini lakini wengi wameskuwa wakitoka Ulaya
na Marekani. Eneo ambalo tumeona tuwekeze kwa nguvu kwa maana ya
kuongeza idaidi ya watalii ni hili la nchi za ghuba na Mashariki ya
Kati,” alisema.
Waziri
Mkuu alisema kimahusiano Tanzania iko karibu na nchi hizi za ghuba
lakini pia wanao uwezo wa kifedha wa kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali
ya utalii. “Amani ya nchi yetu ni kivutio kingine kikubwa cha uwekezaji,
sisi tuko tayari kuwasaidia wafike huko tunakotaka,” alisema.
Alitoa
wito kwa makampuni yanayotaka kuwekeza nchini yaangalie fursa zilizopo
kwenye ujenzi wa hoteli za kawaida, hoteli za mahema (tented camps) na
hoteli zenye kutoa huduma za vyakula (special cuisine restaurant).
Hata
hivyo, aliwataka wawekezaji watakaokuja wafanye juhudi ya kushirikiana
na Watanzania wazawa ili nao wajione ni sehemu ya uwekezaji huo.
Mapema,
akifungua mkutano huo, Waziri Mkuu alisema katika kipindi cha miaka
mitano, Tanzania imeweza kuongeza idaidi ya watalii kutoka 714,367 mwaka
2009 hadi kufikia watalii 1,095,884 kwa mwaka 2013.
“Kiwango
cha mapato ya watalii hao kiliongezeka kutoka dola za Marekani bilioni
1.2 hadi kufikia dola za Marekani bilioni 1.8 katika kipindi hicho hicho
cha miaka mitano,” alisema na kuongeza kuwa sekta hiyo inaajiri watu
zaidi ya 400,000 kuchangia asilimia 17 kwenye pato la Taifa.
Naye
Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu akizungumza na
washiriki wa kongamano hilo kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu alisema
Tanzania ni nchi ya pili duniani kwa kuhifadhi rasilmali zake na
kuzitumia kwa utalii. “Nchi inayoongoza duniani ni Brazil,” alisema.
Akiainisha
fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi
ya Utalii nchini (TTB), Bi. Devothe Mdachi alisema Tanzania ina fursa
nyingi za uwekezaji kupitia sekta ya utalii zikiwemo uendelezaji wa
fukwe, michezo ya majini na utalii wa mikutano (conference tourism).
“Kwenye
kumbi za mikutano, Tanzania inahitaji kumbi kubwa zenye uwezo wa
kuchukua watu kati ya 5,000 na 10,000 na hasa kwenye miji mikubwa kama
Arusha, Dar es Salaam na Mwanza,” alisema.
Naye
Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Bibi Julieth Kairuki
aliwaeleza washiriki wa kongamano hilo kwamba utalii una fursa kubwa ya
uwekezaji kama ilivyo kwenye sekta nyingine za madini na uchumbaji gesi.
“Uwekezaji
hivi sasa umepanuka, na soko la utalii nchini Tanzania ni fursa kubwa
sana ya kuwekeza. Tunawasihi watu wenye mitaji mikubwa waangalie fursa
hiyo na kuichangamkia kama njia mojawapo ya kuwekeza nchini Tanzania,”
alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, 17 DESEMBA, 2014.