Mratibu
wa kituo cha TFGM na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Mtakatifu Catherine
Laboure ya Kijiji cha Masanga kilichopo wilayani Tarime mkoani Mara,
Thomas Maruga akiwatembeza maeneo mbalimbali ya shule hiyo na Mratibu
Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (kulia) na
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya
watu duniani (UNFPA), Dkt. Natalia Kanem (kushoto) wakati wa sherehe ya
mahafali ya sita ya mabinti waliokwepeshwa msimu wa ukeketaji (Waiseke
wa Kisasa).(Picha za Zainul Mzige wa MOblog).
Na Mwandishi wetu, Tarime-Mara
SERIKALI imeombwa kuhakikisha inakomesha ubabe unaotumika kukeketa mabinti wa koo za Kikuria nchini.
Kauli
hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Kituo cha kupambana na ukeketaji cha
Masanga, Tarime Sista Germaine Baibika akizungumza na waandishi wa
habari baada ya kukamilika kwa sherehe ya mahafali ya sita ya mabinti
waliokwepeshwa msimu wa ukeketaji. Alisema jumla ya mabinti 634
wamehitimu mafunzo ya miezi miwili yanayogusa haki za binadamu, haki
zao, masuala ya afya na kuzitambua na kuezinzi mila nzuri.
Aidha wamejifunza kazi za sanaa na usanii.
Alisema
adha kubwa wanayokumbana nayo mabinti hao waliotoka katika kituo hicho
ni kukamatwa kwa nguvu na kupitishwa kisu cha Ngariba bila wao wenyewe
kuafiki kwa dai la kuendeleza mila. “Hii sio mila” anasema sista
Germaine na kuongeza kuwa hakuna mila inayotengenezwa kunyanyasa watu
wengine au kulazimisha mambo yasiyofaa katika jamii, mila hiyo ikiwepo
lazima ipigwe vita.
Mgeni
rasmi Waziri wa Kazi na Ajira, Mh. Gaudentia Kabaka (wa pili kushoto)
akiwasili kwenye mahafali hayo pamoja na Mratibu Mkazi wa mashirika ya
Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa
Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (kushoto) aliyeambatana na
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya
watu duniani (UNFPA), Dkt Natalia Kanem.
Alisema
serikali isiache kuwatetea mabinti hao kwa dai la kuwa hiyo ni mila kwa
kuwa wanaofanyiwa vitendo hivyo hulazimishwa na haifanyiki kwa ridhaa
yao. Alisema wapo mabinti walioletwa na wazazi wao kuepushwa na janga
hilo, wapo waliotoroka kwa wazazi wao na wapo walioletwa katika kituo
hicho na polisi kutoka makwao.
Mafunzo
hayo ya mwezi mmoja yamelenga kukabiliana na msimu wa ukeketaji ambao
sisita huyo alisema mwaka jana ulianza mapema Novemba na unaendelea hadi
mwaka huu wakati kimila mwaka huu si wa ukeketaji. Kwa mujibu wa mila
za Kikuria ukeketaji hufanyika katika mwaka unaogawanyika, mwaka 2015
haugawanyiki.
Mhashamu
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma Mkoani Mara, Michael
Msongazila akiwasili kwenye sherehe za mahafali ya sita ya kituo cha
kupambana na ukeketaji Masanga wilayani Tarime mkoani Mara.
Mafunzo
hayo ambayo yamelenga kuwatoa mabinti wa kisasa wenye mwelekeo wa
maisha yenye hali bora mabinti wanaofika hapo huwa hawataki kukeketwa na
ndio maana mwaka huu walipata tatizo la binti mmoja kuzimia wakati
alipomuona baba yake katika maeneo ya kituo hicho.
Alisema
wapo wazazi wakorofi wanaokuja kudai watoto wao lakini pia ipo jamii
korofi inayotumia ubabe baada ya wasichana hao kutoka hapo wanakeketwa
kwa lazima. Katika hafla hiyo iliyoendeshwa na masista wa shirika la
Daughters of Charity of St. Vincent De Paul, Waziri wa Kazi na Ajira Mh.
Gaudentia Kabaka aliwapongeza wasichana hao na kuwataka kuwa mfano
katika jamii na kutekeleza wajibu wao. Alisema wamekuwa mabinti wa
kisasa kwa kukataa ukeketaji na hivyo wao wanastahili kuwa walimu kwa
wenzao.