Sauti za Busara ni tamasha lililojipatia umaarufu ndani na nje ya
mipaka ya Tanzania, ni tukio la kila mwaka ambalo limefanikiwa kuwekwa
katika kalenda ya matamasha Afrika. Sauti za Busara huwaleta watu
pamoja kusheherekea muziki wa Afrika bila ya kujali dini, rangi,
tamaduni na wala wanapotoka.
Busara Promotions inathamini na kushukuru Tanzania kama moja ya nchi
zenye amani kuliko zote Duniani. Huku mwaka 2015 ukiwa ni mwaka wa
uchaguzi Tanzania, taasisi hii isiyo ya kiserikali inaamini ili
maendeleo yaendelee bila kizuizi, tunahitaji kuimarisha umoja, heshima
katika utofauti na kufanya kazi ili kutunza na kulinda amani hii yenye
thamani. Kama mwanamziki mwenye tuzo Baaba Maalkutoka Senegal
anavyosema, ‘Njia kuelekea amani ya dunia inapatikana katika muziki na uwezo wake wa kuleta watu pamoja.’
Huku likiwaleta pamoja wasanii tofauti na watazamaji kusherekea
muziki wa Kiafrika, Sauti za Busara inahodhi shindano, kukiwa na zawadi
ya pesa taslimu ambayo ni pesa ya kurekodi kwa washindi wa Nyimbo za Amani.
Mkurugenzi wa Tamasha, Yusuf Mahmoud anasema “Sauti za Busara 2015
litaisaidia kukuza amani kwa kutumia muziki; ambapo vikundi 15 kutoka
Tanzania, sambamba na vingine vya Kimataifa vitatoa sauti za ujumbe wa
amani, umoja na mshikamano katika maonesho yao. Tunatarajia kwamba
(sauti) hizi zitasikika kwa nguvu na uwazi”
Wasanii wa Kitanzania katika shindano hili ni pamoja na Leo Mkanyia, Msafiri Zawose, Mohamed Ilyas, Zee Town Sojaz, Ifa Band, Mgodro Group, Mabantu Africa na wengine wengi. Shindano la Nyimbo za Amani linadhaminiwa na Busara Promotions, kwa msaada wa Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam.
Shindano la Nyimbo za Amani litafanyika katika
tamasha la Sauti za Busara Mji Mkongwe, Zanzibar kati ya saa 10:00 jioni
siku ya Alhamisi tarehe 12 na saa 2:00 usiku siku ya Jumapili tarehe
15 Februari 2015. Shindano liko wazi kwa Wakazi wa Tanzania au Wazawa
wa Tanzania.
Vikundi vyote vya Kitanzania vinavyoshiriki kwenye tamasha
vinaalikwa kutunga nyimbo maalum yenye dhima ya amani na umoja na
kuifanyia onesho katika mida yao ya kutumbuiza katika tamasha. Fedha
taslimu zitazawadiwa kwa ajili ya uzalishaji wa rekodi kitaalamu wa
nyimbo zenye ubunifu: 4m/- TSh (Mshindi wa 1), 3m/- TSh (Mshindi wa 2)
na 2m/- TSh (Mshindi wa 3)