MUIMBAJI nguli raia wa Afrika Kusini na anayetikisa
kwenye muziki wa Injili Afrika, Rebecca Malope ni mmoja wa waimbaji wa
Kimataifa waliochomoza kwenye Tamasha la Pasaka linalotarajia kufanyika baadaye
mwaka huu hapa Tanzania.
Kwa mujjibu wa Mwenyekiti wa
Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo Alex Msama
hivi sasa wanaendelea na mchakato
wa maandalizi ya tamasha hilo ambalo linatimiza miaka 15 tangu kuasisiwa
kwake.
Msama alisema sambamba na Malope,
Afrika Kusini wanatarajia kutoka waimbaji wengine wawili ambao ni Solly
Mahlangu na Keke Phoofolo ambao ni moto wa kuotea mbali. Msama alisema waimbaji hao ni
muendelezo wa waimbaji waliokubali kutumbuiza kwenye tamasha hilo ni pamoja na
Ephraim Sekeleti, Solomon Mukubwa na wazawa akiwemo Upendo Nkone na Bonny
Mwaitege.
Aidha Msama alisema tamasha la
mwaka huu litakuwa ni la aina yake kwa sababu kutakuwa na matukio mengi ambayo
yataendana na maadhimisho ya miaka 15 ya Tamasha hilo lililoasisiwa mwaka 2000.
“Hivi sasa tunaendelea na
mchakato kuelekea Tamasha la Pasaka mwaka huu ambalo litakuwa ni la aina yake
kwa sababu tutakuwa na mambo mengi ambayo yatafanana na miaka 15 ya tamasha letu pendwa linalowalenga wenye uhitaji
maalum ambao ni walemavu, yatima na wajane,” alisema Msama.
Naye Mjumbe wa Kamati ya
Maandalizi, Khamis Pembe alisema wako katika mipango mikubwa ya kufanikisha
miaka 15 ya Tamasha la Pasaka ambako wako katika mipangilio ya kuimarisha
ulinzi siku hiyo. Pembe alisema tamasha la mwaka huu litakuwa ni
tofauti na yaliyopita kwa kuongeza ukaribu zaidi na jamii yenye uhitaji maalum.