Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
HATIMAYE Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima,
ameshitakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa makosa mawili ya
kutoa lugha ya matusi na uzembe wa kuhifadhi silaha yake.
Askofu Gwajima ameshitakiwa pamoja na wenzake watatu, waliotajwa mahakamani hapo kuwa ni Yekonia Behanaze,
Jofrey Andrew na George Mzava.
Mbele ya Hakimu
Mkazi Wilfred Dyansobera, wakili upande wa Serikali, Joseph Maugo,
alidai kuwa Askofu Gwajima anakabiliwa na shtaka la kumtukana Askofu
Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali
Polycarp Pengo.
Wakili Maugo alidai kuwa Askofu Gwajima alitenda kosa hilo kati ya
Machi 16 hadi 25, katika Viwanja ya Tanganyika Peckers, vilivyoko Kawe,
Jijini Dar es Salaam, mahali ambako kanisa lake lipo.
Katika shitaka
la pili, Wakili Maugo alidai kuwa Askofu Gwajima anashtakiwa kwa uzembe
wa kuhifadhi silaha ya moto anayomiliki kisheria.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima akiongea na wanahabari.
Akisoma mashitaka hayo, Wakili Maugo alidai Askofu Gwajima alitumia
lugha ya matusi na kumfedhehesha Askofu Pengo kwa kumuita mpuuzi na
asiyekuwa na akili.
Hata hivyo, Askofu Gwajima alikana mashtaka yote mawili.
Wakili Maugo alidai mbele ya Hakimu Dyansobera kuwa washitakiwa
wengine watatu katika kesi hiyo walitenda kosa la kukutwa na silaha
kinyume cha sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alidai kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Machi 29, katika Hospitali ya TMJ Mikocheni, iliyopo Kinondoni, Dar es Salaam.
Aliendelea kudai kuwa washitakiwa Behanaze, Andrew na Mzava walikutwa na risasi tatu za bastola, 17 za shotgun na bastola moja.
Baada ya kusoma mashitaka hayo, Wakili Peter Kibatala ambaye
anamtetea Askofu Gwajima, aliiambia mahakama kuwa shitaka linalomkabili
mteja wake linadhamika kisheria, hivyo aliiomba mahakama iridhie
kumpatia dhamana.
Wakili huyo alieleza kuwa mshtakiwa ni Askofu wa
Kanisa la Glory’s of Christ Tanzania (Kanisa la Ufufuo na Uzima) na
anafahamika nchi nzima, lakini mbali na tuhuma hizo, nyumba yake jana
ilizingirwa na polisi.
Aliendelea kueleza kuwa mteja wake amekuwa nje kwa dhamana tangu
Machi 27 na awali hata alipokuwa akihojiwa na polisi na kuzimia ghafla
amekuwa mwaminifu kwa kuripoti mwenyewe polisi kila alipohitajika, hivyo
pamoja na kuzingatia wasifu wake, aliiomba mahakama ikubali ajidhamini
mwenyewe.
Akijibu hoja hizo, Mwanasheria wa Serikali, Shedrack Kimario, alisema
hoja zilizotolewa na wakili wa mshtakiwa hazina mashiko, kwa sababu
mshitakiwa alionekana kutaka kukwepa mkono wa sheria.
Hata hivyo,
alisema iwapo mahakama itaona anastahili kupata dhamana na iwapo
atatimiza masharti, basi upande wa mashitaka hauna pingamizi.
Hakimu Dyansobera baada ya kuzingatia hoja za pande zote mbili
alisema Askofu Gwajima ajidhamini mwenyewe kwa bondi ya Sh milioni moja
na washitakiwa wenzake aliwataka kuwa na mdhamini mmoja akila mmoja
ambaye atasaini bondi ya Sh milioni moja.
Washtakiwa wote walitimiza masharti ya dhamana na kuachiwa hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Mei 4, mwaka huu.
Awali Askofu Gwajima aliwasili katika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam saa 9:10 akiwa ndani ya gari lake lenye namba
za usajili T. 159 DDH, akiwa ameongozana na mawakili wake.
Alikwenda
kuripoti kwa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kabla ya
kupelekwa Mahakama ya Kisutu kwa kutumia gari lenye namba za usajili Z
322 FN, lililoingia kwenye viunga vya mahakama ya Kisutu majira ya 9:27
alasiri.
(PICHA: DEOGRATIOUS MONGERA/GPL)