Bi.
Maura Mwingira, Charge d' affaires a.i wa Uwakilishi wa Kudumu wa
Tanzania katika Umoja wa Mataifa, akipokea kutoka kwa Mkuu wa Idara ya
Operesheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa ( DPKO ) Bw. Harves
Ladsous, Medali Maalum ya Dag Hammarskjold ambazo wametunukiwa
Mashujaa wanne walinda Amani kutoka JWTZ ambao walipoteza maisha mwaka
2014 wakati wakitekeleza majukumu yao. Umoja wa Mataifa umeitenga Mei
29 kama siku ya Kimataifa ya kuwakumbuka na kuwaenzi walinda amani
ambao walipoteza maisha katika misheni mbalimbali za Umoja wa Mataifa.
Jumla ya walinda amani 126 walipoteza maisha mwaka jana . Medali hizo
zitawasilishwa kwa Familia za Mashujaa hao.
Charge
d' affaires Bi. Maura Mwingira wa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania
katika Umoja wa Mataifa, akiandika katika kitabu maalum, baada ya
kupokea kwa niaba ya familia za mashujaa wanne wa JWTZ waliopoteza
maisha wakati wakihudumu katika misheni za kulinda amani mwaka jana.
Medali hiyo maalum ya Dag Hammarskjold ilitokwa siku ya ijumaa
kama ishara ya kuwaenzi, kutambua na kuthamini mchango mkubwa wa
mashujaa hao.
Katibu
Mkuu Ban Ki Moon, akiwa na Naibu Katibu Mkuu, Jan Eliasson, na
Viongozi wakuu wa Idara ya Operesheni za Ulinzi wa Amani ( DPKO) muda
mfupi kabla ya utoaji wa medali maalum kwa mashujaa 126 walinda amani
ambao walipoteza maisha mwaka jana. katika salamu zake Katibu Mkuu
alieleza kwamba katika maadhimisho yote yanayofanyika katika Umoja wa
Mataifa, adhimisho la kuwakumbuka na kuwaenzi walinda amani ni
adhimisho lenye kutia simanzi na gumu.
Mpiga
Buluji akiimba wimbo maalum wa maombolezo kama ishara ya kuwakumbuka
mashujaa 126 walinda amani waliopoteza maisha mwaka jana. shughuli za
utoaji wa medali maalum zilitanguliwa na uwekaji wa shada maalum la
maua katika eneo ambalo limetengwa katika viunga vya Umoja wa Mataifa
. Pichani anaonekana Katibu Mkuu Ban Ki Moon akitoa salamu za heshima
kwa wahanga hao anaonekana pia Naibu Katibu Mkuu Jan Eliasson
Na Mwandishi Maalum, New York
Mashujaa
Private Ally Salum Jumanne, Private Mohamed John Mbizi, Private Vasco
Adrian Msigala na Sajent Hamis Juma Nyange kutoka Jeshi la Wananchi
wa Tanzania ( JWTZ) ni miongoni mwa mashujaa 126 ambao siku ya Ijumaa,
Umoja wa Mataifa uliwatunuku medali ya Dag Hammarskjold
Ijumaa
ya Mei 29 ya kila mwaka Umoja wa Mataifa umeitenga kama siku maalum ya
kutambua na kuenzi mchango wa walinda Amani ambao wamepoteza maisha
wakati wakitekeleza majukumu ya ulinzi wa Amani kupitia operesheni za
Umoja wa Mataifa.
Katika
adhimisho hilo na ambalo lilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa
mataifa, Ban ki moon, Naibu wake Jan Eliasson, na Wakuu wa Idara
za Ulinzi za Umoja wa Mataifa, jumla ya mashujaa 126 kutoka nchi 38
waliopoteza maisha mwaka jana (2014) walienziwa kwa kutunukiwa medali
maalum ya DagHammarskjold.
Adhimisho
hilo lilitanguliwa na uwekaji wa shada la maua kwa heshima ya
mashujaa hao, shada liliwekwa na katibu Mkuu Ban Ki Moon katika
sehemu maalum ambayo imeandaliwa kwaajili ya kumbukumbu hiyo.
Akizungumza
kwa masikitiko makubwa wakati wa hafla hiyo, Katibu Mkuu, Ban Ki
Moon, amesema, katika maadhimisho yote yanayofanyika katika Umoja wa
Mataifa, hakuna adhimisho lenye kutia simanzi na ngumu kama hili la
kuwakumbuka na kuwaenzi walinda amani ambao wamepoteza maisha yao wakati
wakitoa ulinzi kwa watu wengine.
“
Ninasikitika kusema kwamba, hii ni mara ya saba mfululizo ambapo zaidi
ya walinda amani 100 wamepoteza maisha katika kipindi cha mwaka mmoja.
Hatari wanayokumbana nayo walinda amani wetu inazidi kuongezeka kwa
kasi kubwa, kutoka kushambuliwa na makundi ya wahafidhina na makundi
ya wanamgambo wenye silaha mpaka hatari ya magonjwa ambukizi kama
vile Ebola” amesema katibu Mkuu.
Mkuu
huyo wa Umoja wa Mataifa akaendelea kusema. “ Tumekusanyika hapa
kuwaenzi mashujaa wetu waume kwa wake ambao wamepoteza maisha yao wakati
wakiwalinda wananchi katika maeneo hatari duniani. Kujitoa kwao
muhanga na namna walivyoyaishi maisha yao, wanatufanya sisi tujisikie
fahari na kututia shime ya kufanya kazi kwa bidii zaidi ili kudhihirisha
kwamba maisha yao hayakupotea bure.
Ban Ki
Moon, awaeleza wawakilishi kutoka nchi ambazo zimepoteza mashuja
wake kwamba, operesheni za ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa
zitaendelea kuwa zenye changamoto na hatari kubwa, na cha kusikitisha
ni kwamba adhimisho lililofanyika ijumaa la kuwaenzi mashujaa hao
halitakuwa la mwisho
“
Walinda amani wetu wanabeba jukumu zito kwaajili yetu sote. Natoa
heshima zangu kwa mashujaana salamu zangu za pole kwa familia za
mashujaa hawa” akasisitiza Katibu Mkuu.
Walinda
amani hao 126 na raia 19 wamepoteza maisha wakati wakihudumua katika
misheni zilizopo, Afghanistan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Ivory
Coast, Cyprus, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Haiti, Mali,
Mashariki ya Kati, Liberia, Sudan na Sudan ya Kusini
Pamoja na Tanzania
Nchi
nyingine ambazo zimepoteza mashujaa wake katika misheni mbalimbali za
kulinda Amani katika mwaka uliopita ni Senegal, Afrika ya Kusini,
Uhispania, Togo, Rwanda, Benin, Burkina Faso, Bangladesh,na
Burundi.
Nyingine ni Cambodia, Chad, El Salvador, Ethiopia, Fiji, France,
Ghana, India, Indonesia, kenya , Malawi, Niger, Pakistan,
Philippines, Tunisia na Zimbabwe.
Pamoja
na mashujaa hao ambao ni wanajeshi, wapo pia raia 19 wakiwamo pia
polisi, madaktari, watumishi na watoa misaada ya kibinadamu ambao
wamepoteza maisha wakati wakitoa misaada kwa binadamu wenzao.
Wakati
Umoja wa Mataifa ukiwaenzi mashujaa hao waliopoteza maisha mwaka jana.
Tayari mwaka huu wa 2015 mashujaa wapatao 49 wamekwisha poteza maisha
wakitekeleza majukumu yao ya kuleta Amani , utulivu na ulinzi wa raia
wasio na hatia katika nchi zenye migogoro. Kati ya mashujaa 49 hao
wapo watanzania wawili.
Jumla ya walinzi wa Amani 3,300 wamekwisha kupoteza maisha tangu
kuanzishwa kwa Operesheni za Ulinzi wa Amani chini ya Umoja wa
Mataifa mwaka 1948.