Alijiandaa na haikushangaza kusikia akiwa miongoni mwa wagombea
watano waliovuka katika mchujo wa Kamati Kuu (CC) na kuingia katika
hatua ya kupigiwa kura na Halmashauri Kuu (NEC).
Tangu alipotangaza nia, January Makamba (41),
amekuwa katika hekaheka za kujitangaza na kujinadi siyo kwa wanaCCM
pekee, bali hata wananchi kupitia machapisho mbalimbali.
Hata hivyo, hadi mwaka 2012, Naibu Waziri huyo wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, hakuwa na mipango ya kugombea urais.
Aliwahi kuhojiwa katika kipindi cha mikasi cha Televisheni ya EATV na
kusema hana mpango huo kabisa.
Pengine Mbunge huyo wa Bumbuli alikuwa na lake
moyoni kwani Julai 2, mwaka jana aliweka bayana nia yake wakati
alipohojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC na kusema atagombea urais kwa
sababu Tanzania inamhitaji mtu mwenye sifa kama zake, wa kizazi cha
sasa.
Tangu wakati huo, January amefanya mambo mengi ya
kujizatiti kwenye nia yake hiyo ikiwamo kutoa kitabu maalumu cha maswali
40, kilichoandikwa na mwandishi Privatus Karugendo kikionyesha kikijibu
maswali mbalimbali kuhusu namna mwanasiasa huyo kijana atakavyoweza
kupambana na changamoto za urais iwapo chama chake kitampa ridhaa na
Watanzania wakamchagua.
Wakati akiendelea na harakati zake Februari, 2014
yaliibuka mambo yasiyotarajiwa baada ya vikao vya CCM kutoa “onyo” dhidi
yake na wanachama wengine watano kuwataka wasiendelee na “mchezo
mchafu” wa kampeni za urais kabla chama hicho hakijaanzisha mchakato huo
rasmi, hapo ndipo wengi wakang’amua kwamba January anausaka urais wala
hatanii.
Mtoto huyo wa Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Mzee
Yusuph Makamba, aliingia rasmi kwenye siasa mwaka 2010 alipoomba ridhaa
ya CCM kuwa Mbunge wa Bumbuli, wilayani Lushoto na katika kura za maoni
za chama hicho, alimshinda mbunge mzoefu, William Shelukindo kwa kupata
kura 14,612 dhidi ya 1,700. Baada ya kushinda ndani ya chama chake,
January hakukutana na mpinzani yeyote kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010
na hivyo akaingia kwenye rekodi ya wabunge waliopita bila kupingwa.
Katika Bunge la 10, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na mwaka 2011, CCM ilimteua kuwa
Katibu wa Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa akichukua nafasi ya
Benard Membe. Alitumikia wadhifa huo ndani ya chama chake hadi mwaka
2012 alipomuachia Dk Asha-Rose Migiro.
Katika Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM, January
alichaguliwa kuwa kati ya wajumbe 10 wa Kamati Kuu ya chama kutoka
upande wa Tanzania Bara akipata kura 2,093.
Atangaza nia mara ya pili
Juni 7, akiwa Dar es Salaam, January alitangaza
nia kwa mara nyingine ya kuwania urais akiahidi kwamba Serikali yake
itaunda baraza la mawaziri wasiozidi 18 wasiotiliwa shaka na wananchi
juu ya uwezo na uadilifu wao.
Alisema ametafakari kwa kina kuhusu changamoto zinazoikabili
nchi na aina mpya ya uongozi inayohitajika na kuamua kuomba ridhaa ya
urais ili azitatue.
“Sijagombea kugombana na watu, nimegombea
kupambana na changamoto za watu. Naiomba nafasi huku nikiifahamu kiu ya
Watanzania kupata aina mpya ya uongozi wa zama za sasa utakaotoa
matumaini mapya yatakayozaa Tanzania mpya. Naelewa misingi iliyojenga
nchi yetu ya haki, umoja, amani, upendo na mshikamano… inayotakiwa
kulindwa kwa gharama zote.”
Alisema kiongozi atakayechaguliwa Oktoba anapaswa
awe na majawabu mapya ya changamoto za Watanzania yatakayomtofautisha na
wengine.
“Sitaunda Serikali ya waporaji na wabinafsi.
Nitaunda Serikali yenye utu, inayowasikiliza watu, itakayotimiza wajibu
wake bila chembe ya uonevu wala ulegevu… nitaunda Serikali ya mawaziri
18 ambayo haitakuwa na mtu hata mmoja anayetiliwa shaka uadilifu wake au
uwezo wake,” alisema Makamba huku akishangiliwa.
Alisema Serikali yake itakuja na vipaumbele vitano
vya kukuza vipato vya watu kwa shughuli zote, huduma bora na za uhakika
za kijamii; utawala bora, utawala wa sheria, usimamizi wa uchumi na
kulinda amani, umoja na usalama wa nchi.
Alichukua fomu Juni 10 na kusisitiza kuwa
hakuingia katika kinyang’anyiro cha urais kujaribu na wala hajajipanga
kwa ajili ya miaka ijayo, bali kushinda sasa na atafanya jitihada zote
ndani ya kanuni kuwashawishi wana-CCM wamchague.
Alisema anataka kuleta mabadiliko nchini na
atainadi ilani kuhakikisha analeta nguvu mpya na chachu ili CCM iendelee
kuaminiwa na kuwa tumaini la kweli kwa Watanzania.
“Maarifa ninayo, upevu ninao, ukomavu ninao, dira
ninayo na nitahakikisha kwamba ndani ya kanuni za chama ninafanikiwa ili
nipate fursa na heshima ya kukiongoza.” Alisema ana imani na viongozi
wakuu wa CCM katika kuongoza mchakato wa kupata mgombea mmoja, katika
hekima, busara na upevu wao.
Alisema uzee wala ujana siyo sifa, bali uzalendo, uadilifu, maarifa, ukomavu, utulivu, hekima na uwezo wa kuongoza nchi.
Alisema akiwa Rais, atafanyia kazi taarifa za
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na watumishi ambao
taasisi zao zitabainika kuwa na matumizi mabaya ya fedha watasimamishwa
kazi na hatua za kisheria zitafuata.
Alirejesha fomu Julai 2 na kusema kuwa ana imani
vikao vya kuwachuja wagombea wa urais vitafanya uamuzi kwa kujiamini na
siyo kwa hofu.
“Tumepata nafasi ya kupitia michakato mingi migumu
kuliko hata huu, tumefanya uamuzi katika mambo mengi na makubwa na bado
tumeendelea kubaki kuwa wamoja. Nina imani hata katika hili pia
tutavuka salama,” alisema.