Meneja Uhusiano wa Vodacom
Tanzania, Matina Nkurlu (kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo
pichani) kuhusiana na mchuano wa nusu
fainali ya shindano la Dance 100% 2015
litakalofanyika jumamosi katika viwanja vya Don Bosco Oysterbay jijini Dar es
Salaam,Kundi litakaloibuka mshindi wa shindano hilo litaondoka na kitita cha
shilingi Milioni 5. Anayeshuhudia kushoto ni mratibu wa shindano hilo
linaloandaliwa na EATV chini ya udhamini
wa Vodacom Tanzania, Happy Shame.
Moja ya kundi linaloshiriki katika
kinyanganyiro cha nusu fainali ya shindano la
Dance 100% 2015 litakalofanyika jumamosi katika viwanja vya Don Bosco
Oysterbay jijini Dar es Salaam,Likionesha umahiri wake wa kucheza tayari kwa
kukabiliana na makundi mengine kwenye kinyanganyiro hicho.Kundi litakaloibuka
mshindi wa shindano hilo linaloandaliwa na EATV na kudhaminiwa na Vodacom
Tanzania litaondoka na kitita cha shilingi Milioni 5.
Mwandishi wetu.· Ni nusu fainali ya kukata na shoka ya Dansi 100%
PATAKUWA hapatoshi katika kinyang’anyiro cha kukata na shoka cha mashindano yanayokuwa kwa kasi hapa nchini ya Dance 100% yanayoandaliwa na kituo cha televisheni cha East Africa(EATV) chini ya udhamini wa kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania,yanaendelea ambapo hapo jumamosi ijayo hatua ya robo fainali inafanyika katika uwanja wa Don Bosco oysterbay jijini Dar es Salaam na kushirikisha makundi 15 kutoka wilaya 3 za mkoa wa Dar es Salaam.
Makundi ya wachezaji wa miondoko mbalimbali ya muziki ambao yatachuana nusu fainali ni The W-T,Team Makorokocho,The W-D,Best boys kaka zao,Mad squared,Mavuno Crew,The winners crew,The heroes crew,Majoka Crew,Cute babies,Quality boys,Wazawa crew,The best,Dream team na Team ya shamba.
Mmoja wa washiriki wanaounda kundi la Cute babies ambalo ndiyo kundi pekee la wasichana Zuwena Karimu,alisema wao kama kundi la wasichana pekee kati ya makundi yote wapo ngangari kupambana na kundi lolote lile kwani wana uwezo wa hali ya juu na ndiyo maana waliingia 15 bora kwa sasa tupo kambini tunajifua ipasavyo na tupo tayari kuingia vitani alisema Karimu.
Mratibu wa mashindano hayo,Happy Shamte,alisema kuwa katika kinyang’anyiro hichi cha nusu fainali watapata makundi 10 yatakayoingia moja kwa moja ngazi ya fainali itakayofanyika hapo baadaye.
“Huu ni mwaka wa nne East Africa Televisheni tunaandaa mashindano haya chini ya udhamini wa Vodacom Tanzania mwaka hadi mwaka yamekuwa yakiongezeka kupata imaarufu na kuwavutia vijana wengi nchini ambao hujitokeza kushiriki”Alisema Shame.
Shame, aliongeza kwamba kundi litakaloibuka na ushindi katika mashindano haya ambayo pia yamekuwa yakionyeshwa na kituo cha televisheni cha East Afrika kila jumatano saa moja kamili usiku,litajishindia kitita cha shilingi milioni 5 zitakazokabidhiwa na Vodacom Tanzania ambao ndiyo wadhamini wakuu.
Naye Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania ambao ni wadhamini wakuu wa mashindano haya,Matina Nkurlu alisema kuwa Vodacom inatoa udhamini kwa kutambua kuwa muziki na michezo ni maeneo ambao yanaweza kutoa ajira kwa vijana na kuweza kuwakwamua kimaisha.
Alisema kuwa Vodacom inatambua kuwa jukumu la kukabiliana na tatizo la ajira hapa nchini sio la serikali peke yake bali pia ni la watu wote ikiwemo makampuni,taasisi za umma na za binafsi na ndio maana siku zote imekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono jitihada za kupambana na tatizo la ajira kupitia nyanja mbalimbali ikiwemo michezo , burudani na huduma mbalimbali zinazotolewa na kampuni hiyo.
“Vodacom tunaamini kuwa vijana wanaweza kuleta mapinduzi makubwa katika sekta mbalimbali iwapo watawezeshwa,hivyo tunadhamini mashindano haya tukiamini kuwa vijana wenye vipaji wanaoshiriki wataweza kujitangaza na kujulikana ambapo katika siku za usoni ni rahisi kujiajiri kupitia katika sanaa”Anasema Nkurlu.