WAKATI
wakisubiri matokeo ya uchaguzi ya rais huku Tume ya Uchaguzi ikitangaza
kura za wagombea wabunge na uwakilishi katika majimbo ya uchaguzi
Zanzibar, Jeshi la Polisi limelazimika kuzima fujo na vurugu kutoka kwa
wafuasi wa CUF waliotanda mitaa ya Mji Mkongwe na barabara kuu ya
Darajani.
Vurugu
zimezuka baada ya mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif
Sharif Hamad kufanya tathmini na kutangaza matokeo ya ushindi wa chama
chake katika uchaguzi wa juzi kwa asilimia 52.87.
Maalim
Seif alitoa tathmini hiyo mbele ya waandishi wa habari katika Ofisi Kuu
ya CUF Mtendeni mjini Unguja na kuitaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)
kutangaza matokeo hayo.
Katika
tathmini hiyo inaonesha kwamba mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
kwa tiketi ya urais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amepata ushindi
kwa asilimia 47.13.
Maalim
Seif alidai matokeo waliyonayo yamekusanywa na mawakala waliopo katika
vituo vya uchaguzi vilivyopo Unguja na Pemba kwa kufanya majumuisho.
Hatua hiyo ilizusha shangwe na furaha kwa wafuasi wa CUF na kuanza
kutembea barabarani huku gari zikipiga honi.
Baadhi
ya mitaa ikiwemo Darajani na Mlandege, polisi waliweka vizuizi ambavyo
vilisaidia kuwazuia wafuasi hao kuingia barabarani. Aidha, ofisi za
Serikali zilizopo katika eneo la Mji Mkongwe pamoja na taasisi za
kibenki, zilifungwa baada ya kuibuka kwa mazingira ya fujo na vurugu.
Kamanda
wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mkadam Khamis Mkadam
alithibitisha Jeshi la Polisi kudhibiti maeneo mbalimbali zaidi yaliyopo
Mji Mkongwe pamoja na eneo la Darajani ambalo ni ngome ya upinzani.
“Tumefanikiwa
kudhibiti vurugu za watu waliofanya fujo na vurugu katika maeneo mbali
mbali ya mji wa Unguja na hali ni shwari kwa sasa,” alisema Mkadam. Kwa
mujibu wa Sheria na Kanuni za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ni kosa la
jinai kwa mtu yeyote au mgombea wa chama cha siasa kutangaza matokeo ya
urais. Mapema, CCM Zanzibar ililaani kitendo kilichofanywa na Maalim
Seif kujitangazia ushindi katika uchaguzi huo.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai
Ali Vuai alisema kitendo hicho ni sehemu ya vitendo na matukio ya
uchochezi yanayotakiwa kudhibitiwa kwa ajili ya kuimarisha amani na
utulivu. Vuai aliitaka ZEC kuchukua hatua za kisheria na kinidhamu kwa
mgombea huyo kwa kauli zake ambazo lengo lake kuingiza nchi katika
machafuko katika kipindi hiki kigumu cha uchaguzi.
Hata
hivyo, viongozi watendaji wa ZEC hawakuwa tayari kulizungumzia suala
hilo, ambapo maofisa wote walikuwa wapo katika mchakato wa kupokea na
kutangaza matokeo ya uchaguzi wa majimbo.