Mwandishi Wetu
Hatimaye zile mbio za
Kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015 zilizoanza Agosti 23, mwaka huu, leo
zinafikia tamati ambapo wagombea wawili wenye msisimko wa aina yake, Dk.
John Pombe Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Edward Ngoyai
Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wanafunga kazi
katika Majiji ya Mwanza na Dar.
MAGUFULI MWANZA
Baada ya kumaliza kuzunguka mikoa yote
ya Tanzania Bara na visiwani kisha kurejea jijini Dar akiunganisha na
Mkoa wa Pwani, leo atalitikisa Jiji la Mwanza katika Viwanja vya Kirumba
akifunga kampeni zake hizo.
Hadi anafunga kampeni zake hizo,
Magufuli amefanya karibia mikutano 300 katika majiji, miji na vijiji
mbalimbali nchini huku akijinadi kwa ilani ya chama chake aliyoahidi
kuitekeleza kwa dhati kwa kubadili mfumo wa kiutawala.
Huku akitumia msemo wake wa ‘Hapa Kazi
Tu’ na staili ya kupiga push up (Magufulika), kote alikopita alieleza
baadhi ya vipaumbele vya serikali yake kuwa ni pamoja na kujenga umoja
wa kitaifa, kulinda muungano, ulinzi na usalama, kuheshimu mihimili ya
dola, kuanzisha mahakama maalum ya mafisadi na majizi, utawala bora,
kuheshimu mawazo yote ya kuleta maendeleo hata yakitoka upinzani na
kuimarisha vyombo vya usalama.
Vingine alivyoahidi ni vita dhidi ya
ubadhirifu, kodi ilipwe na wote, kuongeza ajira kwa kuimarisha viwanda
vya ndani, kufufua sekta ya kilimo, mifugo na tija kwa kujenga viwanda,
kudhibiti madini, kupeleka maji vijijini na mijini, kujenga zahanati
kila kijiji, hospitali ya rufaa katika kila mkoa na kuboresha maslahi ya
wauguzi.
Vingine ni elimu ya bure kuanzia shule
ya msingi hadi kidato cha nne, kujenga nyumba za walimu, mikopo ya
wanafunzi wa vyuo vikuu, kujenga hosteli za wanavyuo, kuboresha maslahi
ya watumishi na kusimamia gesi, kuboresha barabara, flyovers na reli.
Pia ameahidi kulinda haki za walemavu,
uhuru wa habari, kulinda haki za wasanii na wanamichezo na nyingine
nyingi hasa kulinda rasilimali za Tanzania.
Mheshimiwa huyo anatarajia kufunga
kampeni zake kwa kishindo akiweka msisitizo katika vipaumbele hivyo huku
akiambatana na timu kamili jijini Mwanza wakiwemo wasanii na viongozi
mbalimbali wa CCM.
Kwa upande wake, mgombea wa Chadema,
Lowassa anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
ataisimamisha Dar katika Viwanja vya Jangwani kuhitimisha kampeni zake
alizofungulia kwenye viwanja hivyo. Lowassa na timu yake amezunguka
mikoa yote Tanzania Bara na visiwani huku akikutana na mafuriko ya
Wana-Ukawa waliokuwa wakijinasibu kuwa wanataka mabadiliko.
Katika ziara zake, Lowassa alivitaja
vipaumbele vya serikali yake kuwa ni pamoja na elimu bora na bure
kuanzia shule za awali hadi chuo kikuu.
Vingine ni kuwatoa Watanzania katika
lindi la umaskini kwa kuboresha kilimo, viwanda, ujenzi wa reli na
barabara na miundo mbinu mingine kama ya afya, mawasiliano na biashara.
Lowassa aliahidi kuwa serikali yake
itakuwa rafiki wa watu wa hali ya chini ili kuwainua wamachinga, mama
ntilie, bodaboda na wachimbaji wadogowadogo.
Akiwa Viwanja vya Jangwani, leo Lowassa
na viongozi wengine waandamizi wa Ukawa watahitimisha kampeni zao
kuwaomba wapiga kura wamchague Lowassa na wagombea wengine wote wa
Ukawa.