Afisa
michezo mkoa wa Mwanza, James William, akimkabidhi zawadi ya kitita cha
shilingi milioni moja na nusu mshindi wa kwanza wa mbio za km 21 upande
wa wanawake Alice Mogire kutoka Kenya baada ya kutumia muda wa saa 01:14:42 kumaliza
mbio hizo. Wanaoshuhudia ni Meneja Mkuu kampuni ya Capital Plus
International Limited ambao ni waandaaji wa mashindano hayo, Erasto
Kilawe (kushoto), Meneja Kiongozi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya
Jamii (NSSF) mkoa wa Mwanza, Hamis Faki (wa pili kushoto), mjumbe wa
shirikisho la riadha Tanzania (RT), Peter Mwita (wa pili kulia) na
Mwenyekiti wa chama cha riadha mkoa wa Mwanza, Silas Lucas.
Washindi
wa nafasi tatu za juu katika mbio za km 21 upande wa wanaume
wakionyesha medali na pesa taslimu walizopokea kama zawadi baada ya
kuibuka washindi katika mbio hizo.
Mwenyekiti wa chama cha riadha mkoa wa Mwanza Silas
Lucas akiwapa maelekezo wakimbiaji wa km 21 wakati wa mbio za Rock City
Marathon kabla ya mbio kuanza kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini
Mwanza jana.
Wanariadha
katika kundi la km 21 wakikatiza katika mitaa ya jiji la Mwanza
kuelekea katika viwanja vya CCM Kirumba kumaliza mbio hizo.
Festus
Taram kutoka Kenya akimaliza katika nafasi ya kwanza kwenye mbio za
Rock City Marathon zilizofanyika jijini Mwanza jana baada ya kutumia
muda wa saa 01:04:40, akifuatiwa kwa karibu na mshiriki mwenzake kutoka
nchini humo Evancy Kiplagan aliyetumia muda wa saa 01:04:55
Raia wa kigeni nao walijitokeza kuchuana vikali katika mbio hizo.
Wanariadha
wakianza kukimbia mbio za km 21 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini
Mwanza jana, wakati wa mbio za Rock City Marathon 2015.
Wanariadha katika kundi la kilomita tano wakipasha kabla ya kuanza kwa mbio hizo.
Mwandishi wetu, Mwanza
Festus
Taram kutoka Kenya aliibuka mshindi wa kwanza kwenye mbio za Rock City
Marathon zilizofanyika jijini Mwanza jana baada ya kumaliza kwa muda wa
saa 01:04:40, akifuatiwa kwa karibu na mshiriki mwenzake kutoka nchini
humo Evancy Kiplagan aliyetumia muda wa saa 01:04:55
Mbio
hizo za kilomita 21 zilianzia Uwanja wa CCM Kirumba kupitia Barabara ya
ikulu ndogo hadi mzunguko wa samaki na kuelekea Buzuruga kisha kutokea
barabara ya pasiansi na kumalizikia uwanjani Kirumba.
Nafasi
ya tatu upande wa wanaume ilichukuliwa na Mtanzania Fabian Joseph
aliyetumia muda wa saa 01:05:00, ikiwa dakika chache nyuma ya mpinzani
wake.
Akizungumzia
siri ya ushindi wake, Talam alisema hii ni mara ya pili kushiriki
mashindano hayo ambapo mwaka jana alishika nafasi ya tatu jambo
lililompa chachu ya kujituma kufanya mazoezi zaidi na kukaa kambini muda
mrefu jambo lililopelekea kufanya vizuri katika michuano ya mwaka huu.
“Maandalizi
ya mwaka huu ni mazuri na washiriki wameendelea kuongezeka mwaka hadi
mwaka jambo linalotufanya wanariadha kujiwekea mikakati mizuri ili
kuweza kukabiliana na ushindani mkali uliopo katika mbio hizi,” alisema.
Upande
wa wanawake mshindi wa kwanza ni Mkenya Alice Mogire aliyetumia muda wa
saa 01:14:42 akifuatiwa na Mtanzania Natalia Elisante aliyetumia saa
01:15:16 huku Raia mwingine wa Tanzania Angelina Isere akishika nafasi
ya tatu baada ya kutumia saa 01:15:35
Washindi
wa kwanza katika mbio hizo zilizofanyika kwa mara ya saba jijini Mwanza
waliibuka na kitita cha Sh1.5 milioni kila mmoja, washindi wa pili
Sh900,000 na washindi wa tatu Sh700,000 kila mmoja.
Mashindano
hayo ya kila mwaka yaliyo katika kalenda ya RT yaliandaliwa na Kampuni
ya Capital Plus kwa udhamini wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii
(NSSF), Bank M, Precision Air, New Mwanza Hotel, Bodi ya Utalii Tanzania
na PPF.
Wakati
huohuo, Katibu tawala mkoa wa Mwanza alipongeza waandaaji wa mbio hizo
na kutoa wito kwa wadau mbalimbali kushirikiana kwa pamoja ili kurejesha
hadhi ya mchezo wa riadha nchini.