Nembo ya Freemason.
DAR ES SALAAM: Ona hawa! Huku Serikali ya Rais John Magufuli ‘JPM’
ikidhibiti kila aina ya upigaji fedha serikalini, kuna watu wanaojiita
‘wajanja wa mjini’ wanajipatia mkwanja bila kutoka jasho kwa kuuza fomu
wanazoziita za utajiri. Ishu hiyo inafanyika nje ya Jengo la Freemason,
Posta jijini Dar.Iko hivi; siku za karibuni kikosi cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) cha Global Publishers kilipokea malalamiko kutoka kwa watu ‘waliopigwa’ kutokana na tamaa ya utajiri kwa kuuziwa ‘fomu za kujiunga na Freemason’. Watu hao wakaiomba OFM kuufichua uozo huo.
“Jamani OFM, hapo Posta nje ya Jengo la Freemason watu wanaibiwa pesa. Wanauziwa fomu na watu wakisema ni kujiunga na Freemason ili wapate utajiri.“Hilo ni tatizo sasa, watu wengi wanalia, tunaomba mlitumbue hilo jipu,” alisema msomaji mmoja.
Baada ya malalamiko kutoka kwa walalamikaji hao kuzidi kwenye dawati, OFM waliamua kuingia mzigoni kuchunguza ili kubaini ukweli wa malalamiko hayo.
Makamanda wa OFM walifunga safari hadi kwenye jengo hilo na kuchuna sehemu huku wakimfuatilia kila mmoja aliyekuwa akipita ambapo waliweza kugundua kuwepo kwa jambo hilo lakini kwa siri kubwa.
Kamanda mmoja wa OFM alishika bahasha yenye fomu ndani na kuweka maelezo kuwa ni za Freemason ambapo katika watu watano waliopita eneo hilo, wanne walitaka kununua kwa kuulizia bei. Wengine walifika na kuuliza jinsi ya kuingia kwenye ofisi hizo ili wakapewe maelekezo ya kujiunga na taasisi hiyo.
Baadaye, OFM walifika kwenye geti la jengo hilo na kutaka kuzungumza na uongozi, lakini walinzi waliokuwepo walisema uongozi wote upo kwenye mapumziko hadi Machi 15, mwaka huu.
Walinzi hao walipoelezwa kuhusu madai ya baadhi ya watu kupigwa pesa nje ya jengo hilo kwa madai ya kuuziwa fomu za kujiunga na Freemason, walisema mazito.
“Mimi nawashangaa sana Watanzania. Kama kweli kuna fomu kwa nini mtu akuuzie nje. Viongozi wenyewe wakishaingia ndani hatujui wanachofanya. Kama ni fomu si tungekuwa tunaona watu wakiingia na kutoka nazo.
“Juzijuzi hapa, kuna mtu alikuja analia. Akasema amelizwa shilingi milioni ishirini (20,000,000) kwa kuuziwa fomu na mtu nje. Tukamuuliza uliingia ndani, akasema hapana, sasa Freemason inahusikaje hapo?” alihoji mlinzi mmoja akiomba asiandikwe jina.
Baada ya kuligundua suala hilo kuwa ni kweli linafanyika nje ya jengo hilo, OFM inatoa tahadhari kwa watu wote wanaopita katika eneo hilo kuwa makini na matapeli hao.
Imeandaliwa na: Boniphace Ngumije, Gabriel Ng’osha na Mayasa Mariwata