Mwandishi wa BBC Swahili, Humphrey Mgonja alisafiri hadi Arusha na kushuhudia jinsi biashara hiyo inavyokwenda kwenye mji huo wa kitalii. Alizungumza na msichana anayefanya kazi hiyo aitwaye Warda aliyekiri kuwa Kiingereza kina umuhimu mkubwa kwenye biashara yake.
“Sometimes nakutana na wateja ambao hawajui Kiswahili kabisa, unakuta anakuwa ananiongelesha, nasikia lakini nashindwa jinsi ya kumjibu. Kwahiyo nakuwa nakosa hela,” anasema Warda.
“Sehemu kama Dar es Salaam niliona sehemu moja kwa Macheni, niliona kuna mademu waliokuwa wanajua Kiingereza walikuwa wanatoka na wazungu. Mimi sometimes wazungu walikuwa wananipenda lakini kwa colour yangu the way nilivyo lakini tulikuwa tunashindwa yaani ni lugha gongana. Kwahiyo unajikuta mwisho wa siku unapewa dola 100 wakati nilikuwa nipewe 200,” aliongeza.
Warda alikiri kuwahi kuikosa bahati ya mtende ya kuchukuliwa na ‘bwana wa kizungu’ aliyetaka aondoke naye kwenda ng’ambo lakini lugha ilimponza. Anadai kuwa mzungu huyo alikuwa anamtumia mkarimani kuwasiliana naye na ambaye mara nyingi alimfikishia ujumbe tofauti na Warda aliotaka ufike.
“Nilikuwa namsikia anamuambia kabisa yule kijana, ‘mimi niko tayari kumtengenezea passport, watoto wake nitawapangia nyumba kila kitu, namtangulia yeye halafu baadaye atawachukua watoto wake.’ Lakini akifika kwangu mimi anabadilisha maongezi, au mimi nikimtuma anaenda kumwambia vitu tofauti. Kiukweli nilimkosa halafu alikuwa baba mtu mzima anajielewa, anajiheshimu,” Warda alisema kwa uchungu.
“Iliniuma sana, nadhani mpaka sasa hivi nisingekuwa kwenye hii biashara.”
Kituo kimoja kinachofundisha Kiingereza jijini humo kimekiri kuwa na wateja wengi wa kike na kwamba dalili za kuwa na wanawake wanaofanya biashara hiyo kituoni hapo ni kubwa.