Rais
Magufuli akimsalimia Mkuu wa Mkoa baada ya kuwasili katika Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ajili ya uzinduzi wa ndege
mbili.
Kikundi cha ngoma kikitoa burudani mbele ya Rais katika hafla hiyo.
JWTZ wakitoa saluti wakati wimbo wa Taifa ukiimbwa.
Ndege za serikali zilizozinduliwa leo na Rais Dk.Magufuli.
Rais Magufuli akisoma hotuba yake kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam waliohudhuria hafla hiyo na watanzania kwa ujumla.
Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi (kushoto) na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano wakitiliana sahihi.Nyuma yao ni baadhi
ya viongozi wa Bodi ya ATCL.
Rais
Dk.Magufuli (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa ndege
mbili za serikali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
Dar.
Magufuli akishuka katika ndege ya pili kuishuhudia ilivyo ndani baada ya uzinduzi huo kukamilika.
Rais Dk.Magufuli (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mawaziri na Manaibu waziri wa sekta mbalimbali.Rais Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Makatibu wakuu wa idara mbalimbali baada ya kumalizika kwa uzinduzi.
Bras Bendi ya Polisi ikifuatilia hotuba ya rais Magufuli iliyokuwa ikisomwa mbele. Baadhi ya wananchi waliofika kushuhudia tukio hilo. Marubani wa ndege hiyo (kushoto) wakiwa na baadhi ya watumishi wa umma.
RAIS John Magufuli amesema serikali yake imejipanga kununua ndege
nyingine mbili ambapo moja itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 160 na
nyingine abiria 242.Hayo ameyasema leo wakati akizindua ndege mbili za serikali kwenye hafla iliyofanyika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere uliopo jijini Dar es Saalam.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Mama Janeth Magufuli; Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Profesa Makame Mbawara; Mkuu wa Mkoa wa Dar es Saalam Paul Makonda; Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Saalam Isaya Mwita na viongozi wengine mbalimbali.
Vilevile rais aliwananga watu wote wanaobeza ununuzi wa ndege hizo na kuziita zina kasi ndogo ya Bajaj akawataka wawe na moyo wa kupenda vitu vyao wenyewe.
Pia amewahakikishia Watanzania kwa ujumla kwamba ndege hizo ni mpya na zimenunuliwa kwa pesa taslimu na kwamba malipo yake yalifanyika kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza serikali ililipa asilimia 40 na baada ya kukamilika utengenezaji wake ilimalizia asilimia 60 iliyobaki.
Rais pia ametoa onyo kwa bodi mpya ya ATCL kuhusu dhamana waliyokabidhiwa na kuwaambia wanatakiwa kulisimamia shirika hilo kwa weledi ili liweze kujitegemea.
Ndege hizo zitakuwa mali ya serikali na zitakodishwa kwa ATCL kwa mkataba maalum ambapo amesema lazima uwepo mkataba wa makabidhiano.
Mkataba huo utakuwa kati ya katibu mkuu kiongozi, katibu mkuu wizara ya uchukuzi na mawasiliano na mtendaji mkuu wa ATCL ambao ndiyo wamepewa dhamana ya kuzisimamia ndege hizo.
Ndege hizo zenye sifa ya matumizi madogo ya mafuta zitakuwa suluhisho la kupanda kwa bei ya usafiri wa anga nchini na pia zitasaidia kukuza sekta ya utalii nchini.
“Ndege hizi zinatumia wastani wa mafuta ya shilingi milioni moja kutoka hapa hadi Songea, wakati ndege za Jet zinatumia mafuta ya shilingi milioni 28.1 kwa safari kama hiyo,” alisema Magufuli.
Mwisho rais amesisitiza umuhimu wa Watanzania kuwa wazalendo na kujituma kufanya kazi. Pia amezungumzia kitendo cha kuwasimamisha kazi mkurugenzi na afisa tawala mkoa wa Kagera ambao walikuwa wanahujumu hela za mafao ya waathirika wa tetemeko la ardhi Kagera ambao tayari wamekamatwa na kufikishwa mahakamani.
Alitumia pia wakati huo kutangaza kukabidhiwa pesa taslimu za Kitanzania shilingi bilioni sita kutoka kwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, ili kusaidia wahanga wa tetemeko mkoani Kagera.
Na Leonard Msigwa