Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe akishuka kwenye ndege
mojawapo baada kuzindua rasmi ndege mbili mpya aina ya Bombadier Q400
zilizonunuliwa na serikali kwa ajili ya Shirika la Ndege la Tanzania
(ATCL) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es salaam leo Jumatano
Septemba 28, 2016.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 28 Septemba, 2016
amezindua ndege mpya mbili aina ya Bombardier Dash 8 Q400 zilizonunuliwa na
Serikali kwa ajili ya kutumiwa na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).
Uzinduzi wa ndege
hizo za kisasa zilizotengenezwa nchini Canada, umefanyika katika uwanja wa
ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na
Viongozi mbalimbali wakiwemo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Job Ndugai, Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Ian Myles, Mawaziri,
Wabunge, Viongozi wa Wafanyabiashara, Taasisi mbalimbali na wadau wa usafiri wa
anga.
Kabla ya kuzindua
ndege hizo zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja, Rais Magufuli ameshuhudia
makabidhiano ya mkataba wa ukodishaji wa ndege hizo kutoka kwa Katibu Mkuu
Kiongozi Balozi John Kijazi kwa niaba ya Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA)
kwenda kwa Katibu Mkuu Uchukuzi Dkt. Leonard Chamriho kwa niaba ya Kampuni ya
Ndege Tanzania (ATCL).
Taarifa ya ununuzi
wa ndege hizo iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza
kuwa ndege hizo ni mali ya Serikali na zitakodishwa kwa Kampuni ya Ndege
Tanzania (ATCL) kwa lengo kutoa huduma za usafiri wa anga ndani na nje ya nchi.
Imeongeza kuwa
ndege hizo zimenunuliwa kwa kuzingatia kuwa zinafaa kufanya kazi katika
mazingira ya Tanzania ikilinganishwa na ndege nyingine za jamii yake, na imetaja
manufaa hayo kuwa ni pamoja na uwezo wa kuruka na kutua katika viwanja vya lami
na visivyo vya lami, matumizi madogo ya mafuta, kuwa na injini zenye nguvu
zaidi na kubeba mzigo mkubwa.
"Ni dhairi
kuwa ndege hizi zitaimarisha mtandao wa huduma za usafiri wa anga kwa soko la
ndani, lakini pia zitaongeza ushindani na kuleta unafuu wa bei kwa watumiaji wa
usafiri wa anga, vilevile zitaimarisha sekta za biashara na uwekezaji na
kuwezesha watalii kutembelea vivutio vya ndani ya nchi"
ameeleza Balozi Kijazi.
Kwa upande wake
Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa na kutimia kwa ahadi aliyoitoa ya kununua
ndege mpya ili kufufua usafiri wa anga kupitia ATCL na ameahidi kuwa Serikali
imeanza mazungumzo ya kununua ndege nyingine mbili zitakazofanya safari za
ndani na nje ya bara la Afrika ambapo moja itakuwa na uwezo wa kubeba abiria
160, na nyingine itakuwa na uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 240.
"Kwa sababu
fedha za kununulia ndege hizo zote mbili kubwa zipo, tukinunua ndege ya kubeba
watu 240 itakuwa inatoka hapa Dar es Salaam hadi Marekani bila kutua popote,
itaondoka hapa Dar es Salaam mpaka China bila kutua popote ili watalii
wanaotoka China, Marekani, Urusi, Ujerumani na nchi nyingine wasifikie nchi
nyingine, watue hapa moja kwa moja na waangalie maliasili zetu tulizonazo,
utalii wetu upande, na huo ndio mwelekeo wa nchi yetu tunaoutaka"
amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli
amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuleta
mabadiliko yenye manufaa kwa nchi na kuwapuuza watu wanaobeza juhudi hizo
wakiwemo waliobeza ununuzi wa ndege hizo kwa kujenga hoja zisizo za msingi.
Aidha, Dkt.
Magufuli ameitaka Bodi na Menejimenti ya ATCL kufanya kazi kwa weledi na
ufanisi huku akiisisitiza kuondoa kasoro zote zilizosababisha kampuni hiyo
kudorola ikiwemo kuchuja na kuwaondoa wafanyakazi watakaoshindwa kuendana na
mwelekeo unaostahili, wasio waadilifu na waaminifu, wasaliti na wahujumu.
Rais Magufuli pia
amewataka Watanzania wote wafanyabiashara, wakulima na wafanyakazi kusafiri kwa
kutumia ndege hizo ili Kampuni ya ATCL ijiimarishe na iweze kujiendesha badala
ya kutegemea ndege za Serikali.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es
Salaam
28
Septemba, 2016