Muonekano wa nje wa Bohari Kuu ya dawa Zanzibar iliyopo maeneo ya Marughubi
nje kidogo ya Mjini wa Zanzibar.
Shehena ya dawa zilizoagizwa na S erikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zikiwa
zimehifadhiwa kwenye Bohari kuu Maruhubi kabla ya kusambazwa katika hospitali
na vituo vya Afya.
Wafanyakazi wa Bohari kuu wakisambaza dawa katika Hospitali ya Wilaya
Makunduchi ikiwa ni jitihada za serikali kuwapatia wananchi huduma hiyo bila
malipo .
Mkurugenzi wa Bohari Kuu ya dawa
Zanzibar Zahran Ali Hamad akimkabidhi dawa
Daktari msaidizi wa Hospitali ya Wilaya
Makunduchi Asha Salum Hassa (wa pili kulia) kwa ajili ya Hospitali hiyo.
Picha na
Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar.
Na Ramadhan Ali/Maelezo Zanzibar 03.10.2016
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya imesema itahakikisha kwamba Hospitali na Vituo vyote vya afya vinapatiwa dawa zote muhimu kwa ajili ya wananchi.
Mkurugenzi wa Bohari kuu ya dawa Zanzibar Zahran Ali Hamada amesema Serikali tayari imeidhinisha shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya kununulia dawa na Wizara imeshatumia shilingi milioni 600 kununua dawa ambazo zitatosha katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.
Amesema katika mwaka wa fedha 2016/17 Serikali imetenga shilingi bilioni tano kwa ajili ya kununulia dawa ambazo zinakidhi mahitaji ya wananchi katika kuendeleza azma ya Serikali ya kutoa huduma za afya kwa wananchi bila malipo.
Akisambaza dawa hizo katika Hospitali na vituo vya afya, Zahran amewaeeleza wafanyakazi kuwa Serikali imetumia fedha nyingi kununua dawa hivyo amewataka kuzitunza na kuwapa wananchi kwa mujibu wa mahitaji yao.
“Hakuna haja ya kuweka akiba dawa wapeni wananchi, dawa zipo zakutosha na utaratibu wa kuagiza nyengine umeshaanza, ”alisisitiza Mkurugenzi wa Bohari Kuu.
Alisema Wizara itaandaa utaratibu wa kufuatilia matumizi ya dawa hizo ili kuhakikisha zinawafikia wananchi na amewashauri viongozi shehia na wananchi kwa jumla kuwa walinzi wa dawa hizo.
Daktari Msaidizi wa Hospitali ya Makunduchi Dkt. Asha Salum Hassan amesema hali ya dawa hivi sasa inaridhisha na dawa nyingi muhimu zinapatikana isipokuwa dawa za maumivu na Anti biotic zinatumika kwa wingi hivyo baadhi ya wakati zinakwisha bila ya kuingizwa nyengine. Ameahidi kuwa dawa hizo zitatumika kama zilivyokusudiwa kwa ajili ya wananchi na atahakikisha kuwa hakutatokea ubadhirifu wowote ulio nje ya utaratibu uliopangwa na Wizara.