Shirika la ndege la Rwanda,
Rwandair, limezidisha ushindani katika uchukuzi wa ndege Afrika
Mashariki na Kati kwa kununua ndege aina ya Airbus A300-200.
Ndege hiyo itawezesha shirika hilo kufika masoko ya Ulaya na bara Asia.Ndege hiyo ilizinduliwa kwa mara ya kwanza kwenye uwanja wa kimataifa wa Kanombe, Kigali.
Mkuu wa shirika la Rwandair John Mirenge amewaambia waandishi wa habari kuwa ndege hiyo yenye nafasi ya abiria 244 ndiyo ya kwanza katika ukanda huu na ina teknolojia ya kisasa na ya hali ya juu.
"Ukiwa angani ndani ya ndege hii unaweza kupiga simu, kupata ujumbe wako wa simu, ujumbe wa barua pepe, ujumbe wa WhatsApp na mawasiliano mengine. Haya hayakuwepo katika ndege nyingine tulizo nazo," amesema.
"Hata katika ukanda huu na kwingineko barani afrika hakuna shirika lenye ndege iliyo na uwezo huo."
Ni ndege iliyotengenezwa nchini Ufaransa na kununuliwa kwa kitita cha dolla milioni 200 za marekani.
Bw Mirenge, anasema safari za shirika la ndege la Rwandair zilikuwa zinajikita sana Afrika magharibi na kati na kwamba ndege hii sasa inakuja kuongeza uwezo wa kuvamia masoko ya Ulaya, Asia na kusini mwa Afrika.
Safari ya kwanza ya ndege hiyo inatarajiwa kufanyika wikendi ijayo tarehe 8 kuelekea mjini Dubai.
Shirika hilo sasa linalenga kusafirisha abiria laki 750 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2017.
source:bbcswahili