Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) ambalo ni msimamizi wa sekta ya Sanaa na
burudani nchini linawakumbusha wamiliki na waendeshaji wa kumbi za
burudani kufuata sheria, kanuni na taratibu walizopewa kwenye vibali
vyao vya uendeshaji wa kumbi.
Wanaelekezwa
kuhakikisha wanakuwa na vibali halali vya uendeshaji wa kumbi zao,
kuzingatia muda wa matumizi wa ukumbi, kuepuka kelele zinazosumbua
kwenye maeneo maalum hasa makazi ya watu na kuhakikisha ulinzi na
usalama wa maisha ya watu na mali zao.
Aidha,
BASATA linawakumbusha wamiliki wote wa kumbi za sherehe na burudani
kwamba ni marufuku kukusanya watoto katika kumbi zao kupitia kile
kinachoitwa ‘Disko Toto’ katika msimu huu wa Sikukuu ya Christmas na
Mwaka mpya ili kuepuka maafa yanayoweza kujitokeza.
Uzoefu
unaonesha kwamba, nyakati za sikukuu kama hizi wamiliki wa kumbi
wamekuwa wakijisahau na kuandaa madisko ya watoto hali mbayo imekuwa
ikisababisha maafa ambayo yangeepukika kwa kufuata sheria, kanuni na
taratibu.
Aidha,
baadhi ya wamiliki na waendeshaji wa kumbi wamekuwa wakijisahau na
kuendekeza faida pasi na kujali maelekezo ya vibali vyao, wamekuwa
wakijaza watu kupita viwango vya madaraja waliyopangiwa na BASATA.
BASATA
mamlaka inayotoa vibali vya kumbi za sherehe na burudani linasisistiza
kwamba halitafumbia macho ukumbi wowote utakaokiuka maelekezo haya
sambamba na kuruhusu maonesho machafu yenye kudhalilisha utu wa binadamu
hasa yale yanayoonesha maungo ya ndani. Hatua kali na za kisheria
zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka maagizo haya.
BASATA linawatakia wasanii na wadau wote wa
Sanaa Heri ya Christmas na Mwaka Mpya.
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI, BASATA