KIUNGO wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyewai kuichezea Yanga,
Geoffrey Bonny (37) imeelezwa yupo mahututi nyumbani kwao Iringa
akisumbuliwa na maradhi ya homa ya matumbo na Malaria.
Dada wa mchezaji huyo ambaye pia aliwahi kuichezea Prisons ya Mbeya,
Neema alisema jana hali ya kaka yake ni mbaya na anahitaji msaada ili
apelekwe hospitali kubwa akapatiwe matibabu kuokoa maisha yake.
Neema alisema Bonny aliyewahi kuichezea Taifa Stars chini ya kocha
Marcio Maximo, alifanyiwa vipimo katika hospitali ya Makandana Wilayani
Rungwe na kuambiwa Bonny anasumbuliawa na Malaria na homa ya matumbo.
"Kwa sasa anapatiwa matibabu nyumbani kwa sababu hatuna tena uwezo wa kifedha wa kumpeleka hospitali kubwa," alisema Neema.
Aidha, alisema anaomba wadau wa soka wenye moyo wa kumsaidia kuwasiliana naye kwa simu ya mkononi (0 765 359 290).
Bonny aliichezea Yanga chini ya kocha Dusan Kondic na hata alipoondolewa
kocha huyo, aliendelea kuichezea timu hiyo chini ya Kocha mpya Kostadin
Papic.
Kiungo huyo anakumbukwa kuwa miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Taifa
Stars kufuzu na kushirki fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN)
zilizofanyika Ivory Coast mwaka 2009.