Serikali ya Jamuri ya Muungano wa Tanzania imewasilisha bajeti yake kwa
mwaka wa fedha 2017/18, huku ikiwa imetangaza kufuta na kupunguza tozo,
ushuru na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye sekta mbalimbali
hapa nchini.
Bajeti hiyo imewasilishwa leo Juni 08, na Waziri wa Fedha na Mipango,
Dkt. Philip Mpango ambapo amependekeza kusamehe Kodi ya Ongezeko la
Thamani (VAT) kwenye bidhaa za mtaji ili kupunguza gharama za mashine na
mitambo kwa ajili uanzishwaji wa viwanda vidogo na vya kati,
kwenye bidhaa zinazosafirishwa nje ya nchi kuifanya Tanzania iwe njia
bora ya kupitisha bidhaa na kuongeza mapato kupitia bandari pamoja na
kwenye vyakula vya mifugo vinavyotengenezwa nchini.
Waziri Mpango pamoja na kupunguza kodi za kampuni kutoka asilimia 30
hadi 10 kwa miaka mitatu ya uzalishaji, pia amefuta rasmi ada ya mwaka
ya leseni ya magari huku akisema kwamba uamuzi huo umechukuliwa ili ada
hii ilipwe mara moja pale gari linaposajiliwa na baada ya hapo iendelee
kulipwa katika ushuru wa bidhaa kama mafuta ya petroli na dizeli.
Katika bajeti iliyowasilishwa, Waziri huyo amependekeza kuondolewa kwa
ushuru wa huduma unaotozwa na halmashauri kwenye mabango na vibao vya
matangazo vinavyoelekeza mahali zilipo huduma muhimu za kijamii kama
vile shule na hospitali huku akitangaza rasmi kuwa kuanzia mwezi Julai
mwaka huu, na kwamba Mamlaka ya Mapato (TRA) ndiyo watakaokuwa
wakihusika na ukusanyaji wa ushuru wa mabango katika halmashauri zote
nchini.
Vilevile bajeti hiyo ya Waziri Mpango imegusa kupunguza ushuru wa mazao
kutoka 5% hadi 3% kwa mazao ya biashara na 2% kwa mazao ya chakula na
kufuta kabisa ushuru kwa mazao yasiyozidi tani moja yanayosafirishwa
kutoka halmashauri moja kwenda nyingine, ikiwa ni pamoja na kupendekeza
kutoza ushuru wa forodha kwa 0% badala ya 25% kwenye malighafi kwa ajili
ya vifaa vya watu wenye ulemavu, na kufuta ushuru wa huduma kwenye
nyumba za kulala wageni 'Guest House'
Dkt. Mpango ametangaza rasmi ukusanyaji wa kodi ya majengo katika miji
na vijiji vyote nchini ambapo amesema majengo/nyumba ambazo
hazijafanyiwa uthamini kodi yake itakuwa Shilingi 10,000 kwa nyumba ya
kawaida na 50,000 kwa nyumba za ghorofa.