Mtoto mmoja wa kiume huko India aliwahi kuwaacha hoi wazazi wake baada ya kuanza kudai aliwahi kuishi kabla ya kizaliwa
Mtoto huyo wa kiume, Taranjijt Singh anasema aliwahi kuishi miaka
michache nyuma, ambapo alifariki kwa ajali ya pikipiki akiwa bado mdogo.
Mtoto huyo akiwa na umri wa miaka miwili alianza kusema kuhusu maisha
yake ya nyuma na alikuwa akitoroka sana nyumbani . Alikuwa akiwaambia
wazazi wake kwamba anakumbuka kijiji alichokuwa akiishi na hata jina la
shule aliyokuwa akisoma.
Alikumbuka pia jina la baba yake wa zamani {kabla hajafa}. Awali
ilionekana kama aina fulani ya kisirani cha mtoto, lakini ilibidi wazazi
wake waanze kuwa na wasiwasi kwa kadiri alivyokuwa akiongezeka kiumri.
Mtoto huyo alikumbuka pia siku aliyokufa . Aliwaambia wazazi wake
kwamba, alikufa September 10,1992. Alikufa baada ya kugongwa na pikipiki
wakati akiwa kwenye baiskeli akiwa anakwenda shuleni asubuhi. Baada ya
ajali hiyo alipata majeraha kichwani na alifariki siku ya pili baada ya
ajali.
Baba yake wa sasa hivi, Ranjit Singh, anasema, mtoto wake alipozidi
kusisitiza kuhusu maisha yake ya zamani, waliamua na mkewe kumpeleka
huko kijijini anakodai kwamba, ndiko alikoishi kabla hajafa. Awali
hawakuweza kumpata mtu ambaye alikuwa anafanana na maelezo ya mtoto
huyu. Mkazi mmoja wa kijiji hicho aliwaomba waende kijiji cha jirani
kinachofuata.
Kwenye kijiji hicho walikwenda kwenye shule ya kijiji ambapo mwalimu
mkuu wa shule hiyo alithibitisha kamba, September 10, 1992 alikufa
mwanafunzi wa shule hiyo kwa ajali ya pikipiki. Kupitia shuleni hapo,
walibaini mahali wazazi wa mtoto yule aliyekufa kwa ajali ya pikipiki,
walipokuwa wakiishi.
Ni kweli waliwakuta wazazi ambao walithibitisha kufiwa na mtoto katika
tarehe na njia iliyoelezwa. Baba wa sasa wa mtoto huyu, Tanjit Singh
alieleza kwamba, mtoto wao aliwaambia kwamba madaftari aliyokuwa nayo
wakati wa ajali yalilowa damu baada ya ajali ile na alitaja kiwango cha
fedha ambazo zilikuwa kwenye mkoba wake wa shule.
Mama wa zamani wa mtoto huyu ambaye kwa maana hiyo ni mama wa mtoto
aliyefariki mwaka 1992 aliposikia hivyo aliangua kilio kikubwa , kwani
maelezo hayo yalikuwa sahihi bila doa la kosa. Alisema vitabu na fedha
hizo bado vipo, kwani aliviweka kwa kumbukumbu ya kifo cha mwanaye .
Baadae mtoto huyu alirudi na wazazi wake wa sasa nyumbani kukiwa na
maswali yasiyo na majibu. Wazazi wake wa zamani pamoja na ndugu zake,
walikwenda kumtembelea kwao baadae. Mtoto huyu aliibaini picha ya siku
ya ndoa ya wazazi wake, ambayo walikuja nayo wakati walipokwenda
kumtembelea kwa wazazi wake wapya.
Awali mwanasayansi, Vikram Chauhan, alikataa kukubaliana na maelezo
kuhusu mtoto huyu , lakini baadae alijipa moyo wa kuanza uchunguzi.
Alitembelea vijiji vyote viwili , cha zamani alikozaliwa na kufa na hiki
cha sasa alipozaliwa.
Alizungumza na wazazi wote na kupata maelezo ambayo yalimfanya kuona
kuna jambo la maana kuhusiana na kifo na ‘kufufuka’ kwa mtoto huyu.
Kwenye kijiji alichozaliwa na kufa mtoto huyu, muuza duka mmoja alikiri
kwamba ni kweli , mtoto kama huyo alikuwepo na yeye alimkopesha
madaftari jana yake na alipogongwa alikuwa akielekea dukani kwake
kumlipa madaftari hayo.
Chauhan alichukua sampuli ya mwandiko wa mtoto huyu na ule wa kwenye
madaftari ya marehemu. Ilipokwenda kupimwa na wataalamu wa mwandiko,
ilibainika kwamba, ilikuwa ni ya mtu mmoja.
Kumbuka kwamba mwandiko wangu hauwezi kuwa sawa na wa mtu yeyote, kama
ilivyo alama za vidole. Kila mwandiko una sifa zake maalum ambazo
haziwezi kupatikana kwenye mwandiko wa mtu mwingine.
Wataalamu wana uwezo wa kubaini mwandiko wa kughushi hata kama umefanywa na mtaalamu wa kiasi gani wa kughushi miandiko.
Kubwa zaidi ni kwamba mtoto huyu ambaye alishaanza kusoma kwenye maisha
yake ya kabla ya kifo, hivi sasa hajapelekwa shule, kwa sababu familia
yake ya sasa ni maskini. Hata hivyo katika jambo la kushangaza zaidi
alipotakiwa kuandika alifabeti za kiingereza na ki-punjabi aliweza
kufanya hivyo bila tatizo. Kama hajasoma ingewezekana vipi kufanya
hivyo? Anatumia akili ya zamani ya kabla hajafa.
Familia yake ya zamani imeomba kukabidhiwa mtoto wao, lakini familia
yake ya sasa imesema hapana, huyo ni mtoto wao. Kisheria, bila shaka,
familia yake ya sasa ambayo ni maskini sana, wakati ile ya zamani
ilikuwa na uwezo, ndiyo yenye uhalali wa kuishi na mtoto huyu.
Huenda baada ya sayansi kuthibitisha kwamba watu hufa na baadae kurudi
wakiwa wanamiliki miilia tofauti, familia kama hii ya zamani ya mtoto
huyu, ndipo itakapoweza kupata haki.
Hata hivyo, bila shaka kila familia kati ya hizo mbili, itakayoishi naye, itakuwa na mashaka ya aina fulani.
Ni vigumu kupingana na maelezo ya mtoto huyu, ambaye tangu akiwa na umri
wa miaka miwili, alikuwa akizungumzia kuhusu kumbukumbu alizonazo juu
ya maisha yake ya nyuma. Ugumu wa kupinga unatokana na ukweli kwamba,
hatimaye maelezo yake yalithibika
Jambo hili linathibitisha maisha baada ya kifo
Lakini sio maisha baada ya kifo peke yake bali pia kukubali kwamba
huenda binadamu ataendelea kuwepo, kwa sababu uwepo {being} haujapotea
na hauwezi kupotea. Mwili wako utaharibika, lakini uwepo wa binadamu
hauwezi kupotea.
Karibuni kwa maoni ndugu zangu woote!