GEITA: Katika hali ambayo inazidisha mashaka juu ya Usalama wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Mtu mmoja ambaye hajatambulika nia yake, amefanikiwa kujipenyeza katika msafara wa Rais na kujifanya miongoni mwa walinzi wa msafara.
Mtu huyo ambaye baada ya kunaswa amekutwa na vitambulisho bandia, alifanikiwa kujipenyeza katika mkutano wa kwanza wa ziara ya Rais wilayani Bukombe mkoani Geita, ambapo kulikuwa na sherehe za uzinduzi wa barabara ya Lami ya Bwanga hadi Uyovu Lunzewe yenye urefu wa km 45 ambayo ujenzi wake ulizinduliwa na Rais Jakaya Kikwete siku hiyo Novemba 9 mwaka huu.
Akiwa kama afisa usalama alikuwa akizuia baadhi ya watu kufika maeneo maalum yaliyoandaliwa mahususi kwa ulinzi, lakini pia alikuwa akipitapita kukagua baadhi wa watu wakiwamo na waandishi wa habari huku akiwapanga namna ya kukaa vyema kabla msafara wa Rais kuwasili eneo la tukio.
Katika mkutano huo wa kwanza alifanikiwa kupita salama kwani baada ya mkutano huo kumalizika, aliweza kupata usafiri na kuondoka na msafara umbali wa km 53 na kufika Ikulu ndogo ya Bukombe, ambako msafara uliitulia kwa muda na wageni kupata chakula, kisha kuelekea katika mkutano wa pili wa hadhara mjini Ushirombo.
Hata hivyo, huko hakuweza kufanikiwa, Jeshi la Polisi mkoani Geita kwa shirikiana na Maofisa Usalama wa Taifa, lilifanikiwa kumtia mbaroni mtu huyo kama inavyoonyesha (Pichani Juu) akiwa ameshikwa chini na Ulinzi wa Askari polisi na afisa usalama akitolewa katika ya mkutano wa Rais Kikwete uliofanyika katika Uwanja wa Kituo cha mabasi Ushirombo.
Mtu huyo ametambulika kwa jina la Kwamani Juma anakadiriwa kuwa na umri kati ya 43-46, alikamatwa Novemba 9 mwaka huu, eneo la Ushirombo katika mkutano wa hadhara akiwa amejipanga kama maaofisa Usalama karibu na jukwaa kuu alilokuwa amekaa Rais Jakaya Kilwete.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita Leonard Paul amethibitisha kukamatwa kwa afisa huyo bandia, alisema "Ndiyo… amekamatwa, si umeona kwenye mkutano kilichotokea, sasa unataka nieleze nini zaidi," alielza Kamanda Paul