Chacha akiongea na wageni wake Saleh Ally (kulia) na Makongoro Oging' (kushoto).
UNIA ina maajabu yake ndiyo maana wakasema, “tembea uone”. Katikati ya Jiji la Dar es Salaam, binadamu ameamua kuishi ndani ya handaki kwa miaka minne.
Chacha Makenge (36), ameishi katika handaki lililo katika eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa kipindi chote hicho na hana hofu na maisha yake ni mazuri tu
Makenge ambaye alikuwa anajulikana kama Kadogo Charles wakati akiwa mtoto, aliamua kubadili jina hilo kwa madai sasa ni mtu mzima. Makala yake ya kwanza kuhusiana na maisha yake hayo, yaliandikwa na gazeti kongwe la Uwazi.
Pamoja na mfumo huo wa maisha, Makenge baba wa mtoto mmoja ni shabiki mkubwa wa timu ya Chelsea ya England ambayo inanolewa na Kocha Jose Mourinho.
Ushabiki wake wa soka ulitokana na kushawishiwa na rafiki yake aliyekuwa akiitwa Benny, baada ya hapo ameamua kuishabikia timu hiyo pekee
“Naifuatilia Chelsea peke yake, napenda kuwaona wanacheza. Uchezaji wao ni tofauti kidogo, naweza kusema wanalingana na wachezaji wengine wa Ulaya. Hata kama wanakuwa hawana mpira lakini bado utaona wako karibu na wanafuatilia kinachofanyika.
“Hakuna anayesimama na kubaki sehemu moja tu akisubiri hadi mpira umfikie. Ingawa nilishawishiwa na rafiki yangu, baadaye nikajikuta naipenda timu hiyo. Sijawahi kuwa shabiki wa wachezaji fulani badala yake napendelea zaidi uchezaji na mafanikio ya timu
chacha makenge akikaribisha wageni
“Kila ninapoangalia mpira lazima nifaidike na kujifunza, mfano kinachonivutia katika mchezo wa soka zaidi ni suala la ushirikiano katika timu. Watu wanapiga pasi, zinafika. Maisha yanatakiwa yawe hivyo, watu wapasiane mambo ili kutengeneza kitu kimoja kwa faida ya wote.
“Soka ndiyo mchezo ninaoupenda zaidi kama nitaamua kuzungumzia michezo. Ingawa mpira wa hapa nyumbani huwa haunivutii sana,” anasema Chacha.
Alipoulizwa kuhusiana na Yanga na Simba, anasema: “Kwanza nikuambie sijawahi kwenda kuangalia mpira Uwanja wa Taifa, sitaki kuwa mshabiki wa upande mmoja lakini napenda kufuatilia nani amefungwa zinapokutana. Mfano nilisikia Simba imeifunga Yanga mabao 3-1, bahati mbaya nikawa sijauangalia
“Siwezi kuuchambua kwa kuwa sikuuona. Lakini bado ningependa timu hizo ziwe zinatoka sare kuepusha tafrani na ikitokea sare basi wawe wameifanyia kazi kweli. Wacheze mpira unaoonekana na atakayezembea, basi afungwe.”
Lawama:
“Mimi sina mchezaji anayenivutia sana, napenda kuwaona watu wakiwa sawa, siangalii jina la mtu, naangalia aliyefanya kazi. Ingawa naweza kushauri kwa wale wanaolaumu sana ikitokea timu zao zimefungwa basi wajaribu kuangalia kwanza mazingira.
“Inawezekana maandalizi hayakuwa ya kutosha, hakukuwa na nidhamu katika maandalizi na hili ni tatizo kubwa. Unajua mwili ukiutumia vibaya pia ni tatizo, hauwezi kuwa katika hali nzuri na kukupa matokeo mazuri,” anasema Chacha.
Makazi yake:
Makazi yake yako kando ya barabara ya Sam Nujoma upande wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na anaishi mwenyewe tu kwa kuwa alishatengana na mkewe.
Chacha anasema mkewe amekuwa akishangaa kila anapokwenda katika eneo analoishi na wakati mwingine anadhani amechanganyikiwa.
“Kwa kuwa niliwahi kuzushiwa nimechanganyikiwa, nikafikia hadi kulazwa kwa nguvu hadi nilipoweka mgomo wa kula, basi mkewe wangu hudhani kweli bado naumwa kitu ambacho si sahihi. Mimi ni mzima wa afya kabisa,” anasema.
Eneo analoshi lina ukubwa wa takribani mita 500. Ametengeneza barabara nzuri kwenda kwake na ameigawa mara mbili kama ilivyo Sam Nujoma Road. Maana ina upande wa kushoto na kulia na katikati kuna majani ambayo yametenganisha.
“Ukiwa hapa upande huu ni wa kwenda na huu ni wa kurudi, ni kama zilivyo barabara nyingine tu,” anasema.
Ulinzi:
Kabla ya kuifikia barabara hiyo, unalazimika kuyapita majani yaliyotengenezwa vizuri kama geti na ukivuka tu unakuta kiti kilichotengenezwa kwa ubunifu kwa kutumia majani.
“Hii ni sehemu ya ulinzi shirikishi, wakati mwingine nalazimika kukaa hapa na kulinda. Ninafanya ulinzi shirikishi.”
Ujenzi:
“Niliijenga kwa miezi saba, ilikuwa ni taratibu na nimekuwa nikiliboresha eneo hili kila kukicha hadi kufikia hapa. Hakukuwa na ramani badala yake ni ubunifu wangu tu. Kabla ya kuchimba handaki nilikuwa nikilala nje tu (anaonyesha sehemu).”
Kitabu:
Unapofika kwake kuna kitabu kwa ajili ya wageni kama ilivyo katika sehemu mbalimbali maarufu ambayo wageni hulazimika kusaini wanapotembelea.
“Nimekuwa na wageni wakiwemo watu maarufu. Hivyo nimeandaa kitabu ili wasaini kwa ajili ya kumbukumbu hapo baadaye,” anasema.
Ndani:
Ndani ya handaki kuna kitanda kimoja kidogo usawa wa urefu wa futi nne na upana futi moja na nusu. Sehemu maalum ya kuhifadhi vitabu, mafaili, magazeti, vyakula na kopo la huduma ya kwanza.
Wanaweza kuingia hadi watu kumi na kukaa kwenye ngazi. Lakini kuna nyuki wa aina zaidi ya nne ambao wanazunguka mule ndani.
“Mimi nimewazoea na hawawezi kuniuma, unajua nao ni viumbe na hawana matatizo kabisa na mimi na tumekuwa tukiishi pamoja,” anasema Chacha.
Lakini anapolala, kawaida hafungi mlango na siku zote hana hofu na wanyama hata kidogo kwa kuwa ameishi miaka minne bila tatizo hilo.
“Kufunga kwangu labda kuwe na mvua au nikiwa natoka,” anasema na baadaye kuonyesha mlango wa majani na miti ambao hutumika kufunga.
Kwake hakuna taa ya aina yoyote na wala hataki kibatari, hivyo ikifika usiku ni kiza kinatawala naye anaona sawa.
“Macho yanafanya kazi mchana kutwa kwenye mwanga, unapofika usiku vizuri kuyaacha kwenye giza yajijenge upya. Kama kuona nafanya hivyo kwa hisia,” anasisitiza.
Chakula:
Anakula vyakula kadhaa kama ulezi, ufuta na vinginevyo. Lakini mara moja moja anaweza kwenda kununua vyakula katika maduka yaliyo kwenye jengo la kibiashara la Mlimani City ambalo liko karibu kabisa na anapoishi.
“Ninapokwenda Mlimani City kununua vitu, kodi inanikera sana. Maji ya shilingi mia tisa, nalipa kodi zaidi ya shilingi 150. Swali langu hawa jamaa nao wanalipa kodi, au wao wanasubiri waniuzie mimi ndiyo inakuwa kodi waliyolipa.
“Kama wanalipa, vipi kwenye lisiti inaonyesha kodi niliyolipa mimi tu. Wao wamelipa wapi na kwa nini isionyeshwe. Nimesikia kodi ya simu imefutwa lakini maji bado tunalipishwaa kodi kubwa sana. Hii ni ajabu!”
Uamuzi wa Chacha kukaa katika eneo hilo ulitokana naye kuchomewa nyumba yake na rafiki yake aliyekuwa amempa eneo kwa ajili ya kujenga.
Rafiki yake huyo kwa mujibu wa Chacha alichoma nyumba yake wakati akiwa mahabusu katika kituo cha Polisi cha Sitakishari. Baadaye akafikishiwa mahakamani kwa madai ya kuwashambulia watu waliomvamia usiku na akahukumiwa jela miezi tisa hadi alipotoka kwa msamaha we Rais Kikwete Desemba 10, 2009.
“Nikaamua kuepuka majungu na tafrani za wanadamu, baada ya kutoka jela niliendelea na kazi zangu za sanaa za mikono lakini nikatafuta sehemu yenye utulivu ikiwa ni pamoja na kuchimba handaki kama nyumba yangu, sasa naishi kwa amani,” anasema Chacha.