Jan 26, 2014
Msekwa, Kisumo wakoleza moto
Dar es Salaam. Wakati mjadala wa uteuzi wa mawaziri ukiendelea kupamba moto nchini, makada wakongwe wa CCM, Pius Msekwa na Peter Kisumo wamesema Rais Jakaya Kikwete ndiye mwenye mamlaka ya kuteua na habanwi na chama, wala mtu yeyote.
Wamesema chama kinaweza kumshauri Rais kuhusu uteuzi, lakini hakiwezi kumbana atekeleze uteuzi wa mawaziri kinaowataka.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Msekwa alisema mwenye mamlaka ya kufanya uteuzi wa mawaziri nchini ni Rais Jakaya Kikwete peke yake.
“Uteuzi wa mawaziri ni kazi ya Rais na katika hilo, hana ubia na mtu na ndiyo mfumo uliopo na unaeleweka na kila mtu na unatumiwa na karibu nchi zote duniani,” alisema Msekwa ambaye ni Makamu wa Mwenyekiti mstaafu wa CCM Tanzania Bara.
Msekwa ambaye pia amewahi kuwa Spika wa Bunge alisema haoni tatizo la mfumo katika suala zima la utendaji kazi wa Serikali na kusisitiza kuwa Rais mpaka anafikia hatua ya kumteua mtu ni wazi kuwa anajua utendaji wake wa kazi.
Alipoulizwa kama haoni uteuzi wa Rais ni kinyume na maagizo ya Kamati Kuu ya chama hicho alisema: “Mawaziri waliitwa mbele ya kamati na kilichozungumzwa ndani ya kikao hicho mimi na wewe hatujui, pengine walijieleza vizuri na ikaonekana kuwa hawana tatizo na kuamua kuwarejesha bila kuwapa adhabu yoyote.”
Kisumo
Naye Kisumo ambaye ni Mdhamini wa CCM, alisema, Rais anaweza kutekeleza au kutokutekeleza uamuzi unaotolewa na chama chake.
Alisema: “Siyo kila linalosemwa na chama lazima Rais alitekeleze, hapana, kwani sijapata kuona mahali popote duniani Rais akatekeleza matakwa ya chama. Urais siyo chama.”
Aliongeza: “Kazi ya kubadili Serikali ni kazi ya Rais, kama chama kimeona kuna mawaziri mizigo hicho ni chama, lakini Rais anaweza kuteua yeyote anayeona anafaa.”
Alisema chama kinapotaka kusema au kutoa maoni yake juu ya jambo lolote hakiombi kibali kwa Rais kutokana na majukumu ya vyama vya siasa kuwa ni kuwatetea wananchi wake.
“Rais anapofanya mabadiliko yake ya Serikali, nje wananchi wanaweza kusema huyu anafaa au huyu hafai, lakini hiyo ni kazi ya Rais kuona kama wanafaa au hawafai.”