Jan 26, 2014
Tido Mhando:Mambo magumu zaidi
Tido Mhando kwenye simulizi zake hizi za kila wiki kwenye gazeti hili la Mwananchi Jumapili, anaelezea kwa muhtasari baadhi ya mambo kati ya mengi aliyokabiliana nayo kipindi kirefu alichofanya kazi ya utangazaji wa redio. Katika simulizi yake iliyopita, Tido alihadithia kuhusu siku zake za mwanzo nchini Kenya alikokwenda kufanya kazi mpya, baada ya kuondoka Redio Tanzania (RTD) mapema mwaka 1980, ikiwa ni pamoja na Serikali ya nchi hiyo kukataa mpango wa kuunda Chama cha Kijamii cha Watanzania waishio Nairobi. Sasa endelea......
Sikuamini hatua hii ya kutukataza kuunda chama chetu cha kusaidiana wenyewe kwa wenyewe, lakini hatukuwa na uamuzi mwingine zaidi ya kutii amri hiyo. Kwa kweli makachero wa ‘Special Branch’ ya Kenya walipokutana nami na kunitaarifu kuhusu uamuzi huu, walionyesha wazi kwamba hawataki masihara yoyote.
Kilichoniudhi zaidi ni kwamba; ndiyo kwanza nilikuwa nimefika Kenya, hivyo hatua hii ikazidi kuniongezea wasiwasi. Nikaamua kupuuzia hayo na kujizatiti kwenye kazi yangu mpya pekee.
Tayari nilikuwa nimeanza kupewa vipindi kadhaa vya kutayarisha na kutangaza. Utaratibu uliokuwepo ni kwamba, vipindi hivyo vilivyotoka nje, yaani tofauti na vya pale Sauti ya Kenya (VOK), vilikuwa vinapitia hatua kadhaa, kabla ya kukubaliwa kwenda hewani.
Kwa kiasi kikubwa vipindi hivyo huwa tayari vimepata udhamini, kwa hiyo ilikuwa lazima kuelezea kuhusu udhamini husika na huku pia ukitakiwa kuandika wazo lote la kipindi chenyewe na baadaye kutengeneza kipindi cha mfano, kitakachokwenda kufanyiwa usaili na wakuu wa VOK, kabla ya kukubaliwa au kukataliwa.
Katika siku zangu hizo za mwanzo, nilikuwa nimepewa kipindi changu cha kwanza, kilichokuwa kimedhaminiwa na Kiwanda cha Kutengeneza Nguo cha mjini Kisumu, kilichokuwa kikijulikana kwa jina la Kikomi.
Baada ya kukamilisha hatua zote zile, tukawa tumekiwasilisha kipindi kile VOK kwa usaili stahiki, lakini muda ukawa unapita bila ya kupatiwa jibu. Kila tukiulizia tuliambiwa tusubiri tu. Ukapita mwezi mmoja, hakuna jibu, zikapita wiki mbili zaidi hakuna jibu. Tukaanza kuwa na wasiwasi.
Hata hivyo, baada ya kama wiki moja zaidi hivi, tena baada ya kuwepo kwa juhudi za bosi wangu Mzee Simon Ndesandjo, ndipo tukapokea jibu lililotuarifu kuwa hatukufanikiwa, sababu: “Mtangazaji huyo mpya ameshindwa kutamka vizuri jina la nchi, yaani badala ya kutamka Kenya amesema Kinya. Hili ni kosa kubwa sana,” tulitaarifiwa hivyo.
Kwa hiyo ilibidi wakuu kuanza kuhangaika huku na huko, maana hata wao hawakuweza kuamini kwamba sababu hiyo tu, ilikuwa pekee ya kukitupilia mbali kipindi chote. Kwa kweli ilifanyika juhudi za ziada hatimaye kipindi hicho kuruhusiwa hewani.
Baadaye nilifahamishwa kwamba, sababu kubwa ya kipindi kukataliwa ilikuwa ni mimi. Kwamba jamaa pale VOK hawakuona mantiki ya mimi kuajiriwa huko Kenya na kufanya kipindi, ambacho wapo wengine wengi nchini humo wangeweza kukitangaza. Nikatambua kwamba nitawajibika kufanya kazi kweli kweli ikiwa ninataka kujenga umaarufu hata huko Kenya.
Wakati nikiitafakari mara kwa mara hali hii, siku moja wakaja watangazaji wawili wa VOK waliokuwa maarufu sana enzi hizo, pale ofisini kwetu Pioneer House nao ni Leonard Mambo Mbotella na Daniel Gatei.
Watangazaji hawa walikuwa mastaa kupindukia. Sidhani kama kulikuwa na mtu yeyote siku zile nchini Kenya ambaye hakuwa akiwafahamu watangazaji hawa. Maana walikuwa wakitangaza vipindi kadhaa vilivyokuwa vikipendwa sana siku hizo, ikiwa pamoja na kuwa wasomaji wazuri wa taarifa ya habari, pia watangazaji wazuri wa mpira.