Jan 26, 2014
Lini tutaona kaulimbiu ya maana kama vile ULEVI KWANZA?
Ndiyo. Tumezoea sana kuimba Kilimo Kwanza, Elimu Kwanza, matokeo ya ajabu kwanza, bila kutambua ni akina nani wanaosukuma gurudumu la maendeleo, bila hata kudai kutambuliwa. Siku hadi siku, usiku hadi usiku wanajitolea kuchangia maendeleo, lakini badala ya kuwatambua na kuwaheshimu tunawalaani, hadi hata marais walitishia kujiuzulu iwapo hawa wapenda maendeleo, hawataacha kuchangia.
Kweli ni ajabu; siongelei wanavyolipa kodi ya ziada kila siku bila kinyongo. Najua hawa wanalipa kodi kuliko hata hawa wanaokwapua mabilioni, lakini hata siku moja hawafikiriwi unafuu wa kodi. Lakini siongelei hayo. Nawasifia vitu vingine kabisa.
Hebu angalia. Enzi za kinywaji kimoja, au tuseme kiwanda kimoja cha kinywaji hiki cha dhahabu, walikuwa na umoja usiotingishika. Walikaa pamoja kila jioni na kuongelea mambo ya maendeleo, hata ya kawaida, lakini daima walikuwa na umoja. Labda mmoja mmoja alizidisha ulipaji kodi, jambo ambalo lilisababisha vurumai kidogo, lakini wenzake walijua jinsi ya kumshughulikia na kesho yake ukawakuta wamekaa pamoja, tena kama kawaida.
Haya, enzi za kinywaji kimoja ikaisha, ukaingia mfumo wa vinywaji vingi. Majina ya vinywaji yaliongezeka mara dufu na kila mmoja akaanza kunywa alichopenda zaidi. Lakini, umoja wao haukuvurugika hata chembe. Kila mtu alikaa na chupa yake, lakini bado waliongelea mambo ya maendeleo, wakabishana, hadi hata kununiana, lakini umoja wao haukutingishika. Maana umoja ulikuwa muhimu kuliko vyote. Ndiyo chanzo cha sebule ya waishiwa.
Hata mahali ambapo mtu alionekana kusaliti umoja wao, bado walijua jinsi ya kukaa naye. Nakumbuka siku ambayo nilikuwa msaliti mimi mwenyewe. Nilikuwa nimeamua kupumzika kulipa kodi hizi zisizo na kikomo, kwa hiyo nilipofika kwenye umoja wetu, watu walianza kama kawaida.
‘Aaaah Makengeza, karibu bwana, hebu sema utakunywa nini?’
Akaonyesha chupa za aina mbalimbali zilizosimama pale kama kitambulisho cha walipa kodi.
‘Ah leo, utanisamehe. Nataka soda tu.’
Watu wote walishtuka. Kumbe kosa kubwa kuliko yote ndani ya jamii ya wanywa bia ni kuomba kitu ambacho hakina kilevi ndani yake. Hata aliyetoa ofa hiyo akahamaki.
‘Ah; wewe bwana, nilifikiri wewe ni mtu wa maana, kumbe …: Kama unataka mambo ya kitoto, hebu kajinunulie mwenyewe.
Akageuka na kuongea na wenzie. Nilisikia kunyanyapaliwa kweli, lakini baada ya kununua soda yangu; bado nilikaribishwa kwenye kikundi na michango yangu ya mawazo ilipokelewa bila shida.
Ndiyo maana, iwe ni mfumo wa kinywaji kimoja au mfumo wa vinywaji vingi, watumiaji wa vile vinywaji wanajua umoja maana yake ni nini? Maana yake siyo wote kunywa aina moja tu ya kinywaji, umoja ni kuwa na dhamira moja na kutafuta namna ya kuhakikisha wenye dhamira moja wanaweza kufikia dhamira ile, hata kama hawakubaliani.