Jan 26, 2014
Vijana tumieni mitandao kwa maendeleo
Kukua kwa teknolojia duniani kumefanya dunia sasa kuwa kama kijiji. Siku hizi unaweza kupata taarifa kutoka sehemu mbalimbali za dunia bila kulazimika kuwa sehemu husika. Pia unaweza kuwasiliana na mtu aliye sehemu yoyote ya dunia kwa haraka na rahisi zaidi, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Hii yote ni kutokana na kukua kwa teknolojia, hasa ya mawasiliano. Hii inahusisha vitu kama vile televisheni, redio, simu na matumizi ya mitandao ya kompyuta. Kukua huku kwa teknolojia kuna manufaa makubwa sana katika jamii yoyote pale matumizi yake yanapokuwa kwa namna stahili yaani matumizi chanya na siyo matumizi hasi.
Hivi sasa tunashuhudia kukua kwa matumizi ya mitandao ya kompyuta, hasa kwa vijana. Kuna aina nyingi za mitandao iwe inayotoa taarifa mbalimbali, iwe mitandao ya kijamii na mengine mingi. Kuna mitandao kama vile facebook, twitter, instagram, linked in na mingine mingi ambayo watu tofauti huweka taarifa zao na kuweza kushirikisha wengine.
Imekuwa kawaida siku hizi kwa vijana wengi, hasa waliopo vyuoni kujiunga katika mitandao niliyoitaja na hii imekuwa rahisi zaidi, ikizingatiwa kwamba simu nyingi sasa zina uwezo wa kuunganishwa na huduma ya internet, hivyo siyo lazima mtu uwe na kompyuta ndipo aweze kupata huduma ya internet. Wakati wowote, mahali popote kupitia simu yako ya mkononi unaweza kupata mawasiliano.
Hilo ni jambo jema, kwani tunajua kabisa teknolojia ni muhimu katika maendeleo ya mwanadamu, lakini swali la kujiuliza ni je, ni namna gani tunatumia mitandao hiyo?
Kama tujuavyo, kila kitu kizuri kina faida na hasara zake. Hivyo, hata matumizi ya mitandao hii hasa ya kijamii ina faida na hasara zake. Katika mitandao hii, kila mtu ana uhuru wa kuandika kile anachojisikia pasipo usimamizi wa mtu yeyote yaani hapa ni tofauti na redio, magazeti au televisheni. Mitandao hii haina usimamizi wa aina yoyote, mtu anaweza kuandika kile anachojisikia, hivyo mtu yeyote anaweza kusoma mambo yote katika mitandao hii ya kijamii, hata yale yasiyofaa au yanayopotosha. Hivyo ni jukumu la mtumiaji mwenyewe kuwa mwangalifu na kila anachokipata katika mitandao hii.
Cha muhimu zaidi ni mtumiaji kujiuliza nini anataka katika maisha kwa maendeleo yake na akitafute hicho kwenye mitandao.
Mitandao hii inaweza kutumika kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwa watu tofauti na inaweza kuwa na manufaa makubwa kwa mwanafunzi, endapo ataitumia ipasavyo. Lakini pia, inaweza kutumika kujifunzia mambo mabaya na hivyo kuwa na matokeo hasi kwa mtumiaji, kwani inaweza kumwathiri kwa kiasi kikubwa asipokuwa mwangalifu.
Kwenye mitandao hii watu wanatuma kila aina ya uchafu kwani kama niliposema hapo awali kwamba hakuna uangalizi wa aina yoyote, hivyo kuna watu hutumia mwanya huo kuandika na kuingiza kadri wanavyojisikia huku wakijidai kuwa hakuna anayeweza kuwashghulikia kwa namna yoyote.
Wapo wanaoweka vitu vilivyo kinyume na maadili na utamaduni wetu wa Kitanzania na mara nyingi, watu hawa utakuta wamejipa na majina ya kipuuzi yanayofanana na yale wanayofanya; hawatumii majina yao halisi wanaogopa ndugu zao watagundua ujinga wanaofanya hivyo hujipa majina ya ajabu na kuweka picha za ajabu.
Siyo hivyo tu, bali pia mitandao hii isipotumika vizuri, inaweza kuwa kikwazo kwa maendeleo. Mfano; mtu anatumia muda mwingI kuwasiliana kwenye facebook kuliko muda anaotumia kufanya kazi, hasa kwa wale walioko kazini. Kuna watu unawaona wakiwa katika mtandao mara wanapoamka asubuhi mpaka jioni, wewe unabaki kujiuliza; huyu mtu anafanya kazi saa ngapi?
Yaani mtu akiingia tu ofisini, badala ya kujiandaa na kuanza kazi kwa siku hiyo, kitu cha kwanza anaingia kwenye facebook ndipo mambo mengine yanafuatia.