MY ADVERT EA SHOWBIZ

MY ADVERT EA SHOWBIZ

SIX OFFICE SOLUTION

MOCHRISPO

DARDY FASHION

Feb 14, 2014

SIKU YA REDIO DUNIANI 2014 KUTUMIA FURSA YA REDIO KUKUZA USAWA WA KIJINSIA NA KUWAWEZESHA WANAWAKE KATIKA UONGOZI, DODOMA HOTEL


Afisa Habari wa Kitengo cha Habari cha Umoja wa Mataifa(UNIC), Bi. Usia Nkhoma Ledama, akisoma Ujumbe kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Bi Irina Bokova katika Maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani.


  Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Rehema Nchimbi akisalimiana na Mkufunzi wa Redio za Jamii kutoka Unesco, Mama Rose Haji Mwalimu meza kuu wakati wa maadhimisho ya siku ya Redio Duniani yaliyofanyika Kitaifa mkoani Dodoma. Katikati ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Bw. Kajubi Mukajanga.
Amesema kwenye hotuba hiyo ya wakuu wa Umoja wa Mataifa kwamba hii ni fursa kwao wote, kusherehekea Siku Ya Radio Duniani kwa kuwatambua wanawake na kufanya yale yaliyo ndani ya uwezo wao kuzilea sauti mpya za kesho.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Bi Irina Bokova amesema na ninanukuu; Katika Siku ya Redio Duniani, tunaadhimisha chombo ambacho kinategemewa zaidi na watu wengi, wanaume kwa wanawake, duniani kote. Redio huwapa sauti wale wasio na sauti, husaidia kuelimisha watu wasio na elimu, na inaokoa maisha wakati wa majanga.
Akisoma taarifa hiyo amesema ikiwa ni chachu ya uhuru wa kujieleza na ushirikishwaji wa wengi, redio ni muhimu katika kujenga jamii yenye uelewa na kukuza heshima na uelewano baina ya watu.


  Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari (MCT), Bw.Kajubi Mukajanga akizungumza machache kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Rehema Nchimbi.
Ujumbe huo wa Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO ulisisitiza kwamba Radio ni muhimu zaidi katika kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.
“Tangu wakati wa watendaji waanzilishi mwanzoni mwa karne ya 20 hadi hawa wa sasa wanaoripoti kutoka kwenye maeneo yenye vita, wanawake wamefanya kazi kubwa katika ukuaji wa redio,Kama waandishi wa habari wa kiraia, maripota, watengenezaji vipindi, mafundi, na watu muhimu wanaofanya maamuzi, wanawake wanafanya kazi katika kila ngazi ya sekta ya utangazaji kuhakikisha ubadilishanaji huru wa maoni, habari na mawazo kupitia masafa,” ilisema taarifa hiyo.
Bi Usia amesema kupitia ujumbe huo kwamba ni kwa sababu hiyo UNESCO inafanya kazi duniani kote kuendeleza radio kama chombo huru na kinachoshirikisha watu wengi kwa ajili ya wanaume na wanawake, na kutengeneza mazingira salama zaidi kwa waandishi wa habari wote, kwa kutambua kwa namna ya pekee vitisho kwa waandishi wa habari wanawake.






  Pichani juu na chini ni Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Rehema Nchimbi akizungumza na wadau wa sekta ya Habari nchini kwenye maadhimisho ya siku ya Redio Duniani yaliyofanyika Kitaifa mkoani Dodoma.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dr.Rehema Nchimbi ambaye aliwaasa waandishi kutangaza vipindi vyenye manufaa kwa jamii ili kusaidia kusukuma maendeleo.
“Tungependa kusikia vipindi vya maendeleo zaidi katika redio kuliko vipindi vya muziki,”alisema
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari (MCT)Kajubi Mukajanga alisema maadhimisho hayo yamewashirikisha washiriki kutoka nchi nzima na yanalenga kuwakumbusha wajibu watangazaji wa redio juu ya nafasi ya radio katika kuelimisha jamii.




 Mchokonozi wa Mada na Mkufunzi wa Redio za Jamii kutoka Unesco Mama Rose Haji Mwalimu akiwasilisha mada inayosema kutumia fursa ya Redio kukuza usawa wa Kijinsia na kuwawezesha Wanawake katika Uongozi.







 Mshehereshaji Meneja wa Maadili wa Baraza la Habari Tanzania( MCT), Bw. Allan Lawa, akiwakaribisha wageni waalikwa kwenye maadhimisho ya siku ya Redio Duniani yaliyofanyika Kitaifa mkoani Dodoma. Maadhimisho hayo yameandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na kufadhiliwa na UNESCO.
Na Mwandishi Wetu, Moblog Tanzania, Dodoma
UMOJA wa Mataifa umesema kwamba bado redio nyingi duniani ziko nyuma katika kuhabarisha habari za usawa wa jinsia na sauti za wanawake na wasichana hazipati nafasi ya kutosha katika matangazo ya kila siku katika vyombo vingi vya habari.
Akisoma ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw, Ban Ki-Moon na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Bi Irina Bokova, katika maadhimisho ya siku ya Radio Duniani jijini Dodoma, Afisa Habari wa umoja wa Mataifa, Bi Usia Nkhoma Ledama amesema mbaya zaidi katika bodi za mashirika ya vyombo vya habari wanawake ni robo tu ya wanabodi.
“Ninavihimiza vituo vya redio kuwatambua kwa usawa wanawake kama wafanyakazi na kama wasikilizaji wake,”
“Maadhimisho ya mwaka huu yanatukumbusha wajibu wa watangazaji wa redio duniani kote kuipaza sauti ya wanawake na kuthamini nafasi ya wanawake katika mashirika ya utangazaji,” akisoma taarifa hiyo
Bi Usia akisoma taarifa hiyo amesema Radio pia inaweza kusaidia sana kumaliza unyanyapaa dhidi ya wanawake na programu zisizozingatia usawa wa kijinsia kwa wote.



Meneja Machapisho, Utafiti na Uhifadhi Hati wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Bw. John Mireny, akitoa maelezo mafupi kuhusu machapisho mbalimbali ya baraza hilo yanayotoa mafunzo mbalimbali ya tasnia ya habari

>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>........... /////////.....>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>

SIKU YA REDIO DUNIANI 2014
KUTUMIA FURSA YA REDIO KUKUZA USAWA WA KIJINSIA NA KUWAWEZESHA WANAWAKE KATIKA UONGOZI, DODOMA HOTEL 13 FEBRUARI 2014
Rose Haji Mwalimu, UNESCO
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Rehema Nchimbi,
Katibu Mtendaji Baraza la Habari Tanzania, Kajubi Mukajanga,
Viongozi na Waandishi kutoka Vyombo vya Habari mbalimbali nchini,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
Habari za asubuhi!
Niliyesimama mbele yenu ni Rose Haji Mwalimu, mwanahabari na mtangazaji nguli. Kwa sasa nafanya kazi na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni(UNESCO), kama mshauri wa masuala ya vyombo vya habari jamii. Maisha yangu na redio jamii yalianza tangu mwaka 2003 nikiwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, (MISA TAN). Miaka ile tulikuwa tukitetea haki ya redio jamii kupunguziwa gharama za leseni, kuanzishwa kwa redio jamii na kupigania
mabadiliko ya Sheria ya Utangazaji. Siku hii ya leo inaadhimishwa kwa kuzishirikisha redio jamii ambazo pia zinahudhuria mafunzo ya kuzijengea uwezo wa kuendesha mijadala inayokuza amani hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, mchakato wa mabadiliko ya katiba na kura za maoni, na Uchaguzi Mkuu; mradi ambao unatekelezwa na UNESCO.
Nasimama mbele yenu kwa unyenyekevu mkubwa kuwasilisha mada inayohusu “ Namna ya Kutumia Fursa ya Redio Kukuza Usawa wa Kijinsia na Kuwawezesha Wanawake Katika Uongozi kwenye redio jamii.”
Utangulizi
Mnamo Mwezi Januari mwaka 2013, Baraza la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio la UNESCO la kuadhimisha Siku ya Redio Duniani. Siku hii huadhimishwa tarehe 13 Februari, tarehe ambayo Umoja wa Mataifa ulianzishwa mwaka 1946.
Leo hii, Umoja huo unatimiza takribani miaka 58 na nimefurhi kuungana nanyi katika ukumbi huu, wanawake kwa wanaume wote duniani, kuadhimisha Siku ya Redio Duniani kama chombo muhimu hususani katika Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania.
Najivunia nchi yangu ya Tanzania kwani ni kielelezo cha nguvu ya redio hususan redio jamiikwani imeongeza upatikanaji wa habari
kwa makundi wahitaji,na kukuza sauti za watu waliosahaulika katika jamii. Redio ina majukumu na itaendelea kuwa na majukumu makubwa katika upatikanaji wa maendeleo nchini, na kuendeleza usawa wa kijinsia.
Redio, Chombo Chenye Nguvu Kukuza Usawa wa Kijinsia
Wakati kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani mwaka huu inaadhimisha, “Kusherehekea Ushiriki wa Wanawake katika Redio na Wote Wanaowawezesha”, ni muhimu kuangalia maendeleo na changamoto zilizopo.
Redio ni chombo ambacho kimechangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya nchi. Redio jamii kwa upande wake bado ni changa hapa nchini. Ikumbukwe kwamba redio jamii ya kwanza ilianzishwa nchiini mwaka 2002 nayo ni Orkonerei Radio Service, Simanjiro.
UNESCO ilianza kutoa msaada kwa redio jamii mwaka 2007, huku kukiwa na redio 2 tu zilizokuwa zimesajiliwa. Tunapozungumzia mwaka 2014, UNESCO inajivunia mafanikio ya kuweza kutoa msaada kwa redio zaidi ya 25 nchi nzima. Vilevile, UNESCO imefanikiwa kuanzisha redio jamii 8 nchini.
Kutokana na matukio mengi yanayoendelea katika kanda, redio hizi zimejipanga katika mtandao – ujulikanao kama Community Media Network of Tanzania kwa kifupi COMNETA. Wakati mitandao
mingine katika ukanda wa Afrika Mashariki ikifuata nyayo hizo, COMNETA inaendela kuonyesha uwezo wake kama kikundi kinacholenga maendeleo ya kujivunia.
COMNETA inavisaidia vituo ambavyo ni wanachama wa mtandao kuwa mfano wa kuigwa katika kushughulikia matatizo yao yanayofanana. Miongoni mwa changamoto hizo, kubwa zaidi ni ile ya kukuza haki na uwakilishi wa kijinsia kati ya wanawake na wanaume, kuendeleza usawa wa jinsia nje na ndani ya utangazaji.
Utafiti wa hivi karibuni umebaini kwamba redio nyingi za jamii zimepiga hatua mbele katika kuweka uwiano wa kijinsia kwa idadi miongoni mwa wafanyakazi wake. Lakini tukizichambua namba hizi, tunabaini kuwepo kwa pengo kubwa lisilowiana ambalo linaonyesha dhahiri kwamba wanawake bado hawana uwakilishi mkubwa katika viwango vya ufundi na utawala.
Pamoja na changamoto zinazochangia mapungufu hayo, tumeshuhudia pia matokeo ya kuwapa motisha viongozi walioweza kumudu changamoto hizo.
Kwa mfano, Adelina Lweramula, ni meneja wa FADECO FM ambae leo hii atazungumza nanyi. Mama huy amesaidia uanzishwaji wa dawati la kwanza Tanzania la Jinsia katika kituo cha redio jamii,maalumu kwa ajili ya kushughulikia matukio ya ukatili wa kijinsia
yanayojitokeza na kutishia maisha ya wananchi wa wilaya ya Karagwe.
Khadija Abdallah, aliyekuwa meneja wa ORS, Simanjiro, ameonyesha umahiri wake katika utayarishaji wa vipindi vya kitamaduni kwa kuishirikisha jamii ya Kimasai wanawake na wanaume kuleta majadiliano yanayolenga kuondoa ubaguzi wa kijinsia na mila potofu zilizopitwa na wakati katika jamii ya Kimasai. Hiyo ni baadhi tu ya mifano ya kujivunia na kuigwa.
Changamoto
Mabibi na mabwana, wageni waalikwa, hadhara hii inaadhimisha wakati ambapo kuna mambo mengi yanaendelea katika historia ya taifa letu, tunapoelekea kwenye sehemu muhimu ya mchakato wa kupata Katiba mpya ambayo ni Bunge la Katiba na Kura ya Maoni. Vilevile Ttunakaribia kipindi cha uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu. Wakati mambo hayo yanaendelea ni vema kutafakari na kutambua changamoto ambazo zinaweza kwa namna moja au nyingine kukwamisha mchakato mzima wa kutekeleza demokrasia nchini.
Changamoto zetu ni nyingi na zinaogopesha kidogo. Wakati Tanzania imeridhia Protokali ya SADC Habari na Maendeleo(SADC----- na ahadi nyingine, sheria zetu za vyombo vya habari bado
zimekaa kimya kuhusu vyombo vya habari na jinsia, na kuhusu maendeleo ya vyombo vya habari jamii.
Redio Jamii kwa upande wake zimeendelea kuchukua hatua za kutayarisha na kutekeleza SERA ZA JINSIA kwa ajili ya vituo vyao. Redio hizo kwa msaada wa UNESCO, na mashirika mengine hususan GEMSAT na TAMWA, zimeweza kuongezeka idadi ya kutumia sera za jinsia kutoka asilimia 20% mwaka 2012, hadi kufikia 60% leo hii. COMNETA inaendelea kushawishi matumizi ya sera moja ya Uhariri na Jinsia, na ni matumaini yetu kwamba idadi itaongezeka na itazidi kuongezeka hapo baadae.
Mwaka huu wa 2014 UNESCO inaendesha mafunzo maalumu yatakayowanufaisha waandishi wa redio jamii 250 nchi nzima kwa lengo la kukuza uwezo wa kutayarisha vipindi vya jinsia vinavyohamasisha ushiriki wa wanajamii.
Pamoja na juhudi hizi, hatuna budi pia kuzungumzia vikwazo vinavyoendelea katika jamii ambavyo kama havitachukuliwa hatua muafaka vinaweza kurudisha nyuma malengo yaliyowekwa. Pamoja na sababu mbalimbali hususani elimu, imani za mila na tamaduni, kukosekana kwa usawa kiuchumi pamoja na mchakato wa kufanya maamuzi kulikotawaliwa na wanaume; takwimu zinaonyesha kwamba wanawake bado hawana uwezo wa kupata, kutumia na kufaidika na teknolojia mpya (ICT). Wakati tunaainisha vikwazo hivyo, tumeshuhudia ni kwa jinsi gani matumizi ya teknolojia mpya yanavyoweza kuwanufaisha na kuwapa uwezo wanawake kupata
nguvu na kudai haki sawa katika maamuzi, na kupata taarifa inayohitajika ili kufanya maamuzi sahihi sio tu kwa faida yao bali kwa watoto wao, familia, jamii na taifa kwa ujumla.
Kwa kuelewa hivyo, hatuna budi kuendelea kufanya kazi na waandishi wa habari wa redio jamii ili waweze kueleza mambo muhimu yanayotakiwa kwa wasikilizaji wao ambao ni wanawake na wanaume, huku tukitoa mafunzo kwa vitendo kwa wanawake ili waweze kufikia kiwango cha uongozi katika vyombo vya habari na sekta za kiufundi. Ipo haja ya kuendelea kutumia fursa ya redio kuunganisha vizazi- kwa kuwajengea ujuzi wa kutayarisha vipindi vya redio kwa kuwalenga wasichana kama watangazaji, wasimamizi na maripota ukizingatia kuwa wasikilizaji wengi wa redio jamii ni vijana. Kwa kufanya hivyo, tutawajengea uwezo wa ushiriki wa makundi ambayo yana dhamana na taifa letu la baadae.
Hitimisho
Nihitimishe kwa kuweka msisitizo kwetu sote tuliopo hapa, ni kwa namna gani tunaweza kuchangia kutimiza wajibu wetu. Wakati vyombo vya habari na redio vinaendeleza na kusisitiza uwiano usiolingana wa usawa wa kijinsia, vinaweza pia kuupiga vita. Redio inaweza kusaidia kukomesha migogoro ya nyumbani. Redio inaweza pia kusaidia wasichana kuendelea na masomo na kupata misaada mashuleni. Redio zinaweza kuwashawishi wanaume kuwa
baba wazuri na mifano ya kuigwa. Redio zinaweza kuwajenga wanawake wajiamini ili waweze kujikwamua na vikwazo mbalimbali vinavyowakabili, kugombea na kushinda nafasi za uongozi katika siasa kwa lengo la kuisaidia jamii inayowazunguka. Redio inaweza kufanya hayo yote, na kwa msaada wetu itafanya hivyo.
Kwa kufanya kazi pamoja, tunaweza kutumia fursa ya redio, kuvunja vikwazo vinavyowazunguka wanaume, wanawake, wasichana na vijana ili kila mmoja ajitambue na kuishi kulingana na uwezo alio nao. Hilo ni lengo letu, na hatutasita kuziendeleza ili tuweze kufikia lengo hilo. Ni kwa namna hii tu tunaweza kutumia fursa ya redio ili kukuza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake kushiriki katika uongozi.
Ahsanteni sana!