Picha inayoonyesha
moja ya kifaa (kamera) nne zilizoagizwa na Serikali kupimia dalili za ugonjwa
wa Ebola maeneo ya viwanja vya ndege. Kifaa hicho kina uwezo wa kutunza picha na
kumbukumbu za msafiri, muda , joto la msafiri, tarehe aliyoingia nchini pia uwezo
wa kupata takwimu kutoka kwenye hali ya majimaji au jasho la Binadamu pindi
kinapoelekezwa kwake.
Naibu
Waziri wa Afya Dkt. Kebwe Steven Kebwe akiongea na waandishi wa habari eneo la
uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere wakati wa kupokea na
kukabidhi vifaa vya kupima dalili za ugonjwa wa Ebola. Wengine ni Mkurugenzi
Msaidizi wa Kitengo cha Dharula na Maafa (kulia) na Kaimu Mkurugenzi wa Bohari
ya Dawa (MSD), Cosmas Mwaifani.
Naibu
Waziri wa Afya Dkt. Kebwe Steven Kebwe akiangalia kwa karibu taarifa
zilizorekodiwa na moja ya kifaa (kamera) nne zilizoagizwa na Serikali kupimia
dalili za ugonjwa wa Ebola maeneo ya viwanja vya ndege.Picha na Aron Msigwa –MAELEZO.
Sehemu ya vifaa vya kubaini hatua za awali za
ugonjwa wa Ebola kwa kupima hali ya joto la mwili kwa wasafiri kutoka nje nchi wanaotumia
viwanja vya ndege vilivyokuwa vimeagizwa
na Serikali vimewasili jijini Dar es salaam.
Vifaa hivyo
vinavyohusisha kamera 4 zenye uwezo wa kubaini joto la mwili wa msafiri kwa
umbali wa mita 100 bila kumgusa muhusika
vimewasili leo katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere
jijini Dar es salaam kutoka nchini Afrika ya Kusini vilikonunuliwa.
Akikabidhi vifaa hivyo
kwa wataalam wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Naibu Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii, Dkt. Kebwe Steven Kebwe amesema kuwa kuwasili kwa vifaa hivyo
ni moja ya juhudi za Serikali za kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa salama kwa
kuuzuia ugonjwa huo kuingia nchini.
Amesema vifaa hivyo vitapelekwa
katika maeneo ya viwanja vya ndege na maeneo yanayotumiwa na raia wa kigeni
kuingia nchini vikiwemo vya Dar es salaam, Zanzibar, Kilimanjaro,Mbeya na
Mwanza.
Ameongeza kuwa Serikali
inaendelea na mpango wa kuagiza vifaa zaidi vya kuwezesha shughuli ya upimaji
wa afya kwa wasafiri wanaotembea (scanners) zitakazowezesha kubaini afya za
wasafiri wengi zaidi kwa wakati mmoja bila kulazimu kuwasimamisha.
Aidha, amewataka
wataalam hao wa afya kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa kwa kuhakikisha
wanawapima abiria wote wanaotoka nje ya nchi bila kujali hadhi walizonazo ili
kuweza kubaini kama wana maabukizi au dalili za ugonjwa wa Ebola.
“Nataka mfanye kazi
yenu kwa kuzingatia weledi wa taaluma yenu na kwa kuzingatia yale
mliyojifunza,mvitumie vifaa hivyo kupima kila abiria ili kubaini joto lake bila
kujali cheo wala hadhi yake maana janga hili ni kubwa” Amesema Dkt. Kebwe.
Kuhusu utunzaji wa
vifaa hivyo amewataka wataalam hao kuhakikisha wanavitunza vifaa hivyo ili
viweze kudumu na kutimiza malengo yaliyokusudiwa ya kuwasaidia wananchi kutokana
na vifaa hivyo kugharimu fedha nyingi kila kimoja.
Katika hatua nyingine
Mh. Kebwe amefafanua kuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inaendelea na
shughuli ya utoaji wa Elimu ya Afya kuhusu ugonjwa wa Ebaola ili kuwawezesha
wananchi kuchukua tahadhari na kuzielewa dalili za ugonjwa huo na namna ya
kujingika endapo utagundulika nchini.
Amesema tayari kamati mbalimbali za wataalam zimeshaundwa ili
kuwezesha zoezi la utoaji wa elimu na mafunzo kwa wataalam wa ndani ili
kuwajengea uwezo wa kukabiliana na janga hilo.
Kwa upande wake Kaimu
Mkurugenzi wa Bohari ya Dawa nchini (MSD), Cosmas Mwaifwani ambaye ofisi yake imehusika
katika uagizaji wa vifaa hivyo nchini Afrika ya Kusini amesema kuwa mahitaji ya vifaa hivyo kwa sasa
yameongezeka kutokana na umuhimu wake na jinsi vinavyofanya kazi kwa ufanisi
mkubwa.
Amesema upimaji kwa
kutumia vifaa hivyo unatumia teknolojia ya kubaini mionzi ya joto kutoka katika
mwili wa binadamu pindi vinapoelekezwa katika maeneo ya macho na masikio ya
mwili wa binadamu.
Amefafanua kuwa vifaa
hivyo vinauwezo wa kutunza picha na kumbukumbu za msafiri, muda , joto la
msafiri na tarehe aliyoingia nchini na kuongeza kuwa vifaa hivyo vina uwezo wa
kupata takwimu kutoka kwenye hali ya majimaji au jasho la Binadamu pindi
kinapoelekezwa kwake.
Mwaifwani ameeleza kuwa
MSD inaendelea kuimarisha uwezo wake kwa kuongeza vifaa zaidi kutoka Ubelgiji
na China na kufafanua kuwa Bohari hiyo imejiandaa kukabiliana na ugonjwa wa
Ebola kwa kujenga uwezo wa kuwa na dawa za kutibu hali ya magonjwa
yanayoambatana na homa hiyo.
Naye Mkurugenzi wa
Viwanja vya ndege nchini, Moses Malaki akizungumza kwa niaba ya Viwanja vya
ndege nchini ameielezea hali hiyo ya upatikanaji wa vifaa katika maeneo hayo kuwa itaongeza ufanisi wa
uchunguzi wa afya kwa wasafiri na kuondoa usumbufu kutokana na uwezo wa vifaa
hivyo kumpima msafiri akiwa mbali.