Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkaribisha Balozi wa Tanzania, nchini Rwanda, Mhe. Ali Said Siwa, wakati alipofika ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Septemba 22, 2014. Picha na OMR |
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Balozi wa Tanzania, nchini Rwanda, Mhe. Ali Said Siwa, leo Septemba 22, 2014. Picha na OMR |
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Hanne
Marie Kaarstad, (wa pili kulia) na ujumbe wake baada ya mazungumzo yao
yaliyofanyika ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Septemba 22,
2014. Picha na OMR
|
MHESHIMIWA MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA MABALOZI WA NORWAY NA RWANDA
Mheshimiwa
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib
Bilal leo amekutana na mabalozi wa Norway na Balozi mteule wa Tanzania
nchini Rwanda na kufanya nao mazungumzo ofisini kwake ikulu jijini Dar
es Salaam.
Balozi
wa Norway nchini Tanzania mheshimiwa Hanne Marie Kaarstad ndiye alikuwa
wa kwanza kufanya mazungumzo na mheshimiwa Makamu wa Rais ambapo licha
ya kufika kujitambulisha alimueleza mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa
atajitahidi kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizi mbili katika kipindi
chake kama Balozi na kwamba Tanzania ni nchi rafiki kwa Norway na
akasisitiza kuzidi kuimarisha uhusiano hasa katika masuala ya utunzaji
wa mazingira.
Kwa
upande wake mheshimiwa Makamu wa Rais alimuelezea Balozi Hanne kuwa,
Tanzania inajivunia uhusiano wake na Norway na kwamba uhusiano huo kwa
sasa unazidi kuimarika na tena Tanzania inategemea kujifunza mengi toka
Norway kutokana na nchi hiyo kuwa miongoni mwa nchi zenye teknolojia ya
juu katika masuala ya gesi na mafuta.
Balozi
Hanne ambaye aliwahi kufanya kazi nchini Tanzania pia alionesha
kufurahishwa kwake na maendeleo ambayo Tanzania inapiga na akafafanua
kuwa mji wa Dar es Salaam ni kiashiria kimojawapo kinachoonesha wazi
kuwa Tanzania inakuwa kwa kasi.
Pia,
Mheshimiwa Makamu wa Rais alimpokea Balozi Ali Said Siwa aliyepangiwa
kuwa Balozi wa Tanzania nchini Rwanda na akamtaka Balozi huyo
kuhakikisha anasaidia mahusiano baina ya nchi zetui kuzidi kuimarika
huku akimsisitizia kuhusu uhusiano wetu kama majirani na pia wananchi wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Balozi Siwa alitumia nafasi hiyo
kumshukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais kwa uteuzi wake na akaahidi
kuiwakilisha vema Tanzania nchini Rwanda.
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Ikulu, Dar es Salaam Septemba 22, 2014