Waziri wa Afya wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,Mh. Rashid Seif Suleiman akionyesha moja
ya funguo za gari ya Ambulance zilizotolewa na Shirika la Umoja wa
Mataifa la Idadi ya watu (UNFPA), alieshikana mkono ni Mwakilishi wa
Shirika hilo Dkt. Natalia Kanem.
Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mh. Rashid
Seif wakati akilijaribu moja ya gari hilo zilizotolewa na UNFPA katika
hafla ilizofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Gari nne za Ambulance zilizotolewa na Shirika la UNFPA zikiwa zimeegeshwa mbele ya Ofisi ya Wizara ya Afya Mnazimmoja.
Na RAMADHANI ALI /HABARI MAELEZO ZANZIBAR
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu (UNFPA) limekabidhi msaada wa magari manne ya Ambulance kwa Wizara ya Afya ya Zanzibar ambayo yatatumika katika Hospitali nne visiwani hapa.
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu (UNFPA) limekabidhi msaada wa magari manne ya Ambulance kwa Wizara ya Afya ya Zanzibar ambayo yatatumika katika Hospitali nne visiwani hapa.
Mwakilishi wa UNFPA
Tanzania Dkt. Natalia Kanem alimkabidhi Waziri wa Afya Rashid Seif
Suleiman magari hayo katika sherehe fupi zilizofanyika Wizarani Mnazi
mmoja.
Dkt. Natalia alitaka
magari hayo yatumike kwa uangalifu ili kufikia malengo ya millennia ya
kupunguza idadi ya vifo vya mama wajawazito na watoto wanaozaliwa hasa
katika maeneo ya vijijini.
Alisema moja ya
sababu inayopelekea vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga ni
tatizo la usafiri ambalo linachangiwa na uwezo mdogo wa baadhi ya
familia hasa katika maeneo ya vijijini.
Aliongeza kuwa msaada
huo ni sehemu ya Mpango maalum wa Shirika la Umoja wa Mataifa ulioanza
mwaka 2011 na kumalizika Juni 2015 ambao huenda ukaendelea hadi mwaka
2016 kusadia masuala ya Afya na Lishe.
Amesema mpango huo wa
miaka minne ambao unahusisha maeneo makuu saba unaendeshwa kwa pamoja
na Mashirika manne ya Umoja wa Mataifa ambayo ni WHO, UNFPA, UNICEF na
WFPA.
Mwakilishi huyo wa
UNFPA amewapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete na Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein kwa juhudi
kubwa wanazochukua katika kuimarisha huduma za mama wajawazito na watoto
wachanga.
Aliesema UN
inathamini juhudi hizo na juhudi za kuimarisha uchumi hivyo aliahidi
kuwa wataendelea kuunga mkono kuhakikisha mama wajawazito na watoto
wanaozaliwa wanaendelea kuishi katika mazingira yaliyo salama.
Waziri wa Afya Rashid
Seif Suleiman, alilishukuru Shirika la UNFPA kwa misaada mbali mbali
inayotoa kwa Wizara hiyo na ameahidi kuwa magari hayo yatatumika katika
malengo yaliyokusudiwa.
Amekiri kuwa tatizo
la usafiri kwa mama wajawazito Zanzibar limekuwa likiwasumbua wananchi
wengi na inafikia wakati akinamama hujifungua wakiwa kwenye gari wakati
wa kupelekwa Hospitali ambazo hazina stara wala hazifai kwa kazi hiyo.
Alieleza matarajio
yake kuwa tatizo hilo kwa sasa litapungua kwa kiasi kikubwa baada ya
kupatiwa msaada huo ambao umekuja wakati muwafaka ambapo Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar inaelekeza juhudi zake kuimarisha huduma za afya
mijini na vijijini.
NA MJENGWA BLOG