MY ADVERT EA SHOWBIZ

MY ADVERT EA SHOWBIZ

SIX OFFICE SOLUTION

MOCHRISPO

DARDY FASHION

Oct 8, 2014

BINGWA WA SPANEST CUP 2014 APATIKANA

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Dk Leticia Warioba akimkabidhi kombe la ushindi wa ligi ya SPANEST, kapteni wa Itunundu Fc

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Dk Leticia Warioba akikagua timu kabla ya mechi ya kumtafuta bingwa wa mashindano hayo
Mabingwa wa michuano ya Spanest Cup Itunundu FC wakisherekea ushindi wao
Na Mathias Canal, Iringa
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Leticia Warioba, kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Iringa, Dkt Christine Ishengoma, amehitimisha Mashindano ya SPANEST CUP 2014 katika Tarafa ya Pawaga na Idodi yaliyoanza kutimua vumbi mwanzoni mwa mwezi Julai 2014.
Mashindano hayo ambayo kauli mbiu yake ilikuwa ni PIGA VITA UJANGILI, PIGA MPIRA, OKOA TEMBO yalishirikisha vijiji 21 kutoka tarafa ya Idodi na Pawaga, vijiji ambavyo vinavyozunguka hifadhi ya taifa ya Ruaha.
Katika mashindano hayo timu ya Itunundu kutoka Pawaga ndiyo waliyoibuka washindi kwa ushindi mwembamba wa goli 1 dhidi ya timu ya Kinyika ambayo ilikuwa tegemeo la wengi Tarafa ya Pawaga.
Akizungumza wakati wa kufunga mashindano hayo Warioba aliwataka viongozi kutenga maeneo kwa ajili ya kujenga viwanja vya vijana ili kukuza na kuendeleza michezo mkoa wa Iringa.(P.T)
 Warioba alitoa Pongezi kwa mradi wa kulinda na kuhifadhi maeneo yaliyohifadhiwa kusini mwa Tanzania (SPANEST) kwa kuandaa
mashindano hayo kwa kushirikiana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, na Chama cha mpira Wilaya ya Iringa. Alisema kuwa Kampeni hiyo ni muhimu kwa kuwa imeweza kuwaweka vijana na jamii kwa pamoja, katika jitihada za kutokomeza ujangili kupitia michezo.
"Ni ukweli usiopingika kwamba Janga la ujangili limekithiri Tanzania, hivyo hali hiyo kutishia kutokomea kwa wanyama hususani tembo ambao ni urihi, fahari na sehemu kubwa ya uchumi wa Taifa letu, pamoja na doria ambazo zimekuwa zikifanywa na vikosi maalumu lakini mwitikio wa vijana bado umekuwa sio mzuri, hivyo kupitia mashindano ya mpira wa miguu yaliyoandaliwa na SPANEST imekuwa ni njia mwafaka ya kuwaleta karibu vijana kupitia elimu na hamasa katika vita ya kupambana na ujangili" Alisema Warioba Hata hivyo Thamani ya Tembo mmoja anayeuwawa na majangili leo, huliondolea taifa na jamii faida kubwa ambayo ingeweza kuendelea kupatikana kupitia sekta ya utalii kwa hata zaidi ya miaka 70 ijayo ambayo tembo anaweza kuishi.
Mapato yatokanayo na utalii katika hifadhi husaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya ujirani mwema ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa, mabweni, Miradi ya maji na hifadhi ya mazingira. Warioba alisema kuwa serikali itaendelea kuuunga mkono jitihada zinazofanywa na SPANEST katika kukabiliana na vitendo vya ujangili na jitihada za kuelimisha na kushirikisha jamii katika masuala ya uhifadhi, utalii na pia kuhakikisha kuwa faida na manufaa ya wanyamapori inawafikia wananchi hususani wale wanaoishi karibu na maeneo yaliyohifadhiwa.
Naye Mkurugenzi wa mipangio na miradi ya maendeleo Tanapa, Dkt Ezekiel Dembe,alisema kuwa anaamini siku moja Pawaga na Idodi watashiriki ligi kuu hivyo kuna kila sababu yakuendeleza vipaji hivyo. Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi wa sheria, utawala na wanachama (TFF), Eliud Mvela akimuwakilisha rais wa (TFF), Jamali Malinzi alisema kuwa mashindano hayo yameingia kwenye ratiba ya
TFF, hivyo ameahidi kushirikiana na SPANEST ili kuboresha mashindano hayo. Sawia na hayo amechangia mipira 5 kwa ajili ya kuimarisha na kuboresha zawadi kwa washindi wa SPANEST CUP 2014.
Naye Mratibu wa mradi wa kulinda na kuhifadhi maeneo yaliyohifadhiwa kusini mwa Tanzania, Godwell Ole Meing'ataki aliwaomba wananchi kutoa taarifa za usahihi kwenye namba 0800751212 iliyozinduliwa na mgeni rasmi baada ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa SPANEST CUP 2014. Huku akisema kuwa taarifa zote hizo watakazotoa wananchi zitakuwa za siri.
Meing'ataki alisema vijana wengi hukamatwa na kufungwa kwa kuwa ndio ambao wanahusika na ujangili, hivyo alitoa wito kwa vijana zaidi ya 150,000 waliojitokeza kushuhudia mashindano hayo kuacha kutumiwa kwenye ujangili kwani jambo hilo limekuwa likiathiri familia zao pale wanapofungwa.
Aliwaahidi wakazi wa Pawaga na Idodi kuwa mashindano hayo yataendelea kufanyika kila mwaka ili kuokoa tembo ambao idadi kubwa ya ujangili imeanza kupungua ukilinganisha na takwimu za mwaka jana.
Katika mashindano hayo mshindi wa kwanza ambaye ni timu ya Itunundu kutoka Tarafa ya Pawaga amepata; Kikombe, Medali ya Dhahabu, Jezi seti moja, mipira mitatu, Cheti, na Fedha shilingi 300,000/=, Kutembelea hifadhi ya Ruaha na kulala siku moja hifazini, kucheza mechi ya kirafiki wakiwa Ruaha.
Kwa upande wa timu ya Kinyika ambayo imeshika nafasi ya pili imepata Medani ya Fedha shilingi 200,000/=, Mipira 2, pamoja na Cheti. 
Timu ya Kitisi kutoka Tarafa ya Idodi imejinyakulia Fedha taslimu shilingi 100,000/= , Medani ya Shaba na Cheti kwa kuwa nafasi ua tatu. Pia timu ya Kitisi ilipata zawadi ya shilingi 100,000 kwa kuonyesha nidhamu mwanzo hadi mwisho wa mashindano hayo.
Kwa upande wake mfungaji bora ambaye ni Siani Mkadange, kutoka timu ya itunundu Tarafa ya Pawaga, alijipatia jumla ya Tsh 100,000/=