Idadi ya
watu waliolazwa hospitalini kwa kunywa togwa inayosadikiwa kuwa na sumu
katika Kijiji cha Litapwasi, Kata ya Mpitimbi mkoani Ruvuma imeongezeka
kutoka 270 hadi 340.
Tukio
hilo lilitokea Jumapili baada ya watu kushiriki sherehe ya Kipaimara
ambako walikula, kunywa pombe na togwa na baadaye wale waliokunywa togwa
walianza kuumwa matumbo, kuhara na kutapika.
Hadi
jana, watu
102 walikuwa bado wamelazwa katika Zahanati ya Lyangweni,
Hospitali ya St. Joseph Peramiho na Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma.
Tayari
watu watano wanashikiliwa na Polisi kwa upelelezi kuhusiana na tukio
hilo, akiwamo Baba Mzazi wa mtoto Dickson aliyepata kipaimara, Enes
Nungu (47).(P.T)
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Mskhiela aliwataja watu wengine
wanaoshikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Songea kwa mahojiano kuwa
ni Benedict Nungu (76), Esebius Komba (36), Sadiki Masodi (65) na John
Kaulangudidi. Mtu anayedaiwa kukabidhiwa ufunguo chumba cha vinywaji
kabla ya kugawiwa kwa wananchi, Ridhiwani Shawa haijulikani alipo.
Mabaki ya chakula, togwa na pombe ya kienyeji vilichukuliwa juzi na kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi.
Kamanda
Mskhiela alitoa wito kwa wananchi wanaoandaa sherehe kuhakikisha
wanafanya hivyo katika mazingira mazuri na yenye usalama ili kuepuka
athari kama hizo.
Mganga
Mkuu wa Hospitali ya Peramiho, Dk Vanace Mushi alisema hadi jana, watu
waliokuwa wamelazwa katika hospitali hiyo walikuwa 34 na hakukuwa na
mgonjwa aliyeruhusiwa kurudi nyumbani.
Kaimu
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, Majuto Mlawa alisema
wagonjwa tisa wa rufaa walipokewa na kupatiwa matibabu huku hali zao
zikiwa mbaya.
Akizungumzia
tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu alisema: "Jambo hili
limenisikitisha sana, nimeumizwa sana nawapa pole wote waliopatwa na
tatizo hilo naamini Mwenyezi Mungu atawasaidia na watapona na kurejea
katika hali zao za kawaida."
Hata
hivyo, Mwambungu alisema hiyo ni ajali kama nyingine, hivyo anaviachia
vyombo vya usalama na wataalamu wa afya kupata ukweli. Pia aliwataka
wananchi kuwa makini pindi wanapoandaa vyakula na pombe za kienyeji
katika sherehe mbalimbali.
Chanzo:Mwananchi