MWANAMUME aliyemshambulia kiongozi wa
Cord, Raila Odinga na Gavana wa Jimbo la Kwale, Salim Mvurya ameshtakiwa
juzi katika mahakama ya Kwale nchini Kenya.Bwana Lengo Karisa Mudzomba
(40), alishtakiwa mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi wa Kwale, Christine Njagi
kwa kuwashambulia viongozi hao wawili na kuvuruga mkutano wao katika
soko la Kinango Jumatatu ya Septemba 29, mwaka huu. Baadaye mtuhumiwa
aliachiliwa kwa dhamana.
Bw Mdzomba alikiri mashtaka hayo na
kuomba mahakama impe muda wa kuomba msamaha kutoka kwa wanasiasa hao.
“Nimekubali mashtaka dhidi yangu ila naomba mahakama hii inipe muda wa
kuomba msamaha kwani kosa si kosa ila kurudia kosa ndiyo kosa,” alisema
Lengo.
Mtuhumiwa huyo alidai atahitaji muda wa wiki mbili kufanya hivyo akisema familia yake iko mbali.
Kiongozi wa mashtaka George Mungai alikubali ombi hilo akisema litatoa fursa kwa waathiriwa kujitokeza.
Mahakama iliamua kutaja kesi hiyo Oktoba 14, 2014 na Bw Mudzomba hakupinga.
Mwajiri wa mshtakiwa, Bi Nassim Issa, alisema alishangazwa na tukio hilo kwani hakulitarajia.
Bi Issa alimtaja Bw Mdzomba kuwa mtu mpole, mnyenyekevu na mwenye akili timamu.
“Nimekuwa nikiishi naye kama mfanyakazi
wa nyumbani kwa muda wa miezi mitatu na hakuonyesha dalili zozote za
upungufu wa kiakili,” alisema Bi Issa.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 60
alifichua kuwa siku ya tukio hilo alimkuta Bw Mdzambo ameketi nje ya
nyumba yake akionekana mwenye hasira nyingi.